Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa mara nyingine kimemuandikia barua Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kikimkumbusha kutekeleza wajibu wake wa kuwaondoa wabunge wa viti maalumu 19 akiwemo Halima Mdee.
Chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimedai hakuna zuio la mahakama linalomzuia Dk Tulia kuwaondoa wabunge hao, kikieleza hata uwepo wa rufaa zao Baraza Kuu la Chadema, bado hakumzuii kiongozi huyo wa Bunge kuwaondoa.
Wabunge hao 19, wakiongozwa na Mdee walivuliwa uanachama na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Novemba 27, 2020 wakituhumiwa kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu, wakati chama hicho kikieleza hakikuwateua kwenye kikao chochote kwenda kuwa wabunge.
Mbali na Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema(Bawacha), wengine ni Esther Matiko, Ester Bulaya, Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Cecilia Pareso, Agnestar Lambart, Tunza Malapa, Asia Mohammed na Felister Njau.
Wengine ni Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza ambao walikimbilia mahakamani kupinga hatua hiyo.
Wiki iliyopita Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa uamuzi wa kufuta uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema dhidi ya waliokuwa wanachama wake 19 wa kuwafukuza uanachama.
Hatua hiyo ilipokelewa kwa faraja na Mdee ambaye juzi, aliliambia Mwananchi kuwa hali hiyo inaonyesha matumaini kuhusu kumalizika kwa mgogoro huo.
Lakini, uamuzi huo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ni kama vile umekoleza joto ndani ya Chadema kupitia Katibu Mkuu wake, John Mnyika aliyemuandikia barua Dk Tulia akimkumbusha kuwaondoa wabunge hao 19.
Jana, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa barua hiyo yenye kichwa cha habari cha ‘Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu shauri la waliokuwa wanachama 19 wa Chadema’ iliandikwa Desemba 15.
Kwa mujibu wa Mrema, barua hiyo imeshafika katika ofisi husika kwa njia rasmi ya barua pepe ya Bunge siku hiyo hiyo, saa 10 jioni.
“Pia Spika wa Bunge (Dk Tulia) amefikishiwa barua hii na Mnyika kwa mawasiliano yake binafsi. Kwa hiyo, Dk Tulia ameshaipokea tayari, lakini kesho (leo) asubuhi saa mbili asubuhi ofisi za Bunge zikifunguliwa Jijini Dodoma tutawasilisha nakala ngumu.
“Kwa kuwa Bunge linatambua mawasiliano ya kidijitali, basi tangu Desemba 15 wameshapata barua hiyo. Ingawa sio utaratibu Chadema kusoma hadharani barua tulizowaandikia kwa ajili ya mawasiliano, ila leo (jana) tutaisoma kwenu,” alisema Mrema.
Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta kwa simu Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi aliyemtaka mwandishi amtume ujumbe mfupi, hata alipotumiwa hakujibu. Spika Tulia alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi hakupokea.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Gabriel Mwang’onda alisema ingawa uamuzi wa Mahakama ulikuwa na mkanganyiko, lakini hata Chadema wakienda kwa Dk Tulia, watapewa majibu kama waliyopewa kipindi cha nyuma.
“Kwa kuwa Spika anaongoza mhimili mmoja na ufafanuzi wa masuala ya utata wa kisheria yanafanyika mahakamani na Mahakama imeshatengua uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema, sidhani kama Dk Tulia atatoa uamuzi tofauti aliyoufanya hapo awali,” alisema Mwang’onda.
Mwang’onda alisema alidhani Chadema watakata rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama, ili kupata ufafanuzi zaidi kwa sababu mwisho wa siku hukumu ya mhimili huo ni kama vile inawabeba wabunge hao 19.
“Labda waanze upya lakini sijui kisheria ipoje, sidhani kama Dk Tulia atakuwa na uamuzi tofauti na hapo awali kwa sababu alikuwa anasubiria uamuzi wa Mahakama. Sidhani kama atakuwa na jipya lolote.
“Jambo la busara ni kumaliza suala hili nje ya mifumo ya Mahakama na Bunge, baadhi wa wabunge hawa 19 wamefanya kazi muda mrefu akiwemo Mdee kwa jasho na damu wamepambana kuijenga Chadema,” alisema Mwang’onda.
Alisema kama Chadema wamefanya maridhiano na CCM, si jambo baya kukaa na wabunge hao kuzungumza nao kuondoa sintofahamu miongoni mwao.
“Ni vitu vinavyoongeleka, lakini hatuelewi shinikizo gani linasababisha waonekana wabaya, zaidi kinachoniumiza ni kuendelea na mifumo hii ya Mahakama na Bunge badala ya kujikita kujenga chama. Kama unakaa meza na moja na CCM unashindwaje kukaa na watoto wako?” alihoji.
Mwang’onda alisema anamuamini Mbowe (Freeman -mwenyekiti wa Chadema) akisema hana shida, ila kuna watu wanaomshinikiza kwa mambo yao binafsi kuhusu sakata hilo, sio kwa mtazamo au masilahi ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Mrema, nakala ya barua hiyo imepelekwa pia kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Tunaendelea kushauriana na wanasheria wetu kuhusu utekelezaji wa agizo la Mahakama, lakini tutaendelea kuchukua hatua nyingine dhidi ya Dk Tulia ikiwemo kuwataarifu maspika wenzake endapo ataendelea kukaidi na kuvunja Katiba ya Tanzania.
“Tutawaatarifu kuwa Dk Tulia haheshimu Katiba ya Tanzania na tutashangaa kama ataendelea kuongoza vikao vya mabunge duniani, wakati Katiba aliyoapa kuilinda haitekelezi hapa nyumbani,” alisema Mrema.