Huduma za zaboreshwa Hospitali ya Katavi

Muktasari:
Msongamano wa wagonjwa hususani wajawazito wakati wa kujifungua katika Hospitali ya rufaa Katavi umepungua kwa kiasi fulani ikilinganishwa na hapo awali.
Katavi. Ongezeko la miundombinu bora ya kutolea huduma za afya na wataalamu wanaokidhi vigezo umesaidia kupunguza msongamano wajawazito wakati wa kujifungua katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi.
Mganga Mfawidhi hospitali hiyo, Yustina Tizeba akizungumza na Mwananchileo Desemba 7,2021 amesema awali walikabiliwa na changamoto ya msongamano wa wagonjwa hususani wajawazito.
Amesema kwa mwezi mmoja iliwalazimu kuhudumia akina mama wajawazito 500 hadi 600 wakati wa kujifungua ambapo kwasasa wamepungua na kufikia 180 hadi 200.
“Miundombinu imeongezeka na kuboreshwa,zahanati, vituo vya afya ikiwamo cha Ilembo kinatoa huduma za upasuaji kimetupunguzia sana,” amesema Tizeba akaongeza.
“Tunao madaktari bingwa wanne awali hawakuwapo, Madaktari wa kawaida walikuwa wanne kwasasa tunao 15,wauguzi wa degree, wataalamu wa meno na macho hawakuwapo kwasasa tunao,”
Aidha amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wameweka utaratibu wa kutoa huduma za uchunguzi bure ili wananchi wapime afya zao.
“Kuanzia Desemba 6 hadi 9, 2021 tutatoa huduma mbalimbali za uchunguzi wa kisukari,shingo ya uzazi,kinywa na meno,macho,presha na mengineyo,”
Hata hivyo zaidi ya wananchi 50 kutoka maeneo tofauti mkoani wamejitokeza kupima afya zao wakiomba utaratibu huo uwe endelevu.
“Hii fursa tuliyoipata tunashukru sisi wenye maisha duni kwasababu inatolewa bure,tunaomba waendelee kutoa bure wenye matatizo ni wengi,”wamesema Regna Revocatus na Francis Watosha.
Mwisho.