Hospitali ya Rufaa Mbeya yapatiwa msaada kusaidia watoto njiti

Mbeya. Uhaba wa vitanda vya watoto njiti katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya umesababisha watoto wawili kulazwa kitanda kimoja hali ambayo inaweza kusababisha kupata magonjwa ya kuambukizwa.
Daktari bingwa wa watoto na Mkuu wa Idara ya magonjwa ya watoto, Dk Alinanuswe Kasililika amesema leo Jumatano Februari 22, 2023 mara baada ya Mkuu wa Mkoa, Juma Homera kukabidhi vitanda sita na mashine mbili za Oxygen vilivyotolewa na Taasisi ya Doris Mollel foundation vyenye thamani ya Sh13 milioni.
Dk Alinanuswe amesema kuwa wastani kwa wiki wanapokea watoto njiti watano mpaka nane huku kwa mwezi idadi inafikia watoto 25 mpaka 50 jambo ambalo ni changamoto kubwa katika kitengo hicho.
“Mahitaji ni makubwa kwani vitanda vilivyopo 37 huku mahitaji ni zaidi 50 tunashukuru taasisi hiyo kutoa msaada wa vitanda sita na mashine mbili za mashine ya upumuaji (Oxygen) ambayo itapunguza vifo visivyo vya lazima ”amesema.
Aidha amesema kipindi cha mwezi June mpaka Julai kila mwaka wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya vichomi na mifumo ya upumuaji na kuomba wadau kuchangia vifaa tiba katika kitengo hicho.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kulingana na mahitaji kuwa makubwa kwenye hospitali, vituo vya afya kuna ulazima wa taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia vifaa tiba.
“Hili lililofanyika hapa Mbeya leo ni tendo kubwa sana tumesikia taarifa ya daktari bingwa mahitaji ni makubwa yanayopelekea watoto wawili kulala kitanda kimoja tuombe tu wadau kuendelea kuunga mkono serikali kuchangia kulingana na mahitaji. ”amesema.
Aidha Homera amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwepo vituo vya afya ,zahanati na hosptali licha ya kuwepo kwa baadhi kuwa na changamoto ya vifaa tiba .
“Nashukuru sana taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuona umuhimu wa pekee kuchangia vifaa tiba katika kitengo cha watoto njiti naomba muendelee kujitoa katika hosptali zetu nyingine zenye shida ” amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Doris Mollel ,amesema kuwa wamewekeza zaidi kuisaidia serikali kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto njiti nchini kwa kutoa vifaa tiba.
“Tunaona hali halisi ya malezi na makuzi kwa watoto njiti Serikali inahitaji kuongezewa nguvu kutoka kwa taasisi, mashirika, na wadau mbalimbali ili kuokoa watoto wanaotoka katika familia za watu wasiojiweza kwani kutoa ni thawabu kwa Mungu” amesema.
Mwanamke mjamzito, Janeth Sanga ambaye alifika kupatiwa matibabu amesema wanaishukuru Serikali kupitia taasisi hiyo kwa kushawishi na kuwezesha upatikanaji wa mashine za oxygen na vitanda kwa watoto wenye uhitaji.
“Mimi ni mzazi uwa tunaona changamoto wodi wanalazwa watoto njiti zina joto sasa tena walale wawili kuna hatari ya kuambukizwa magonjwa ya mifumo ya hewa ikiwepo mafua na kifua ” amesema