Hospitali ya Rufaa Mbeya yaboreshwa

Muktasari:
Wizara Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wazee na Watoto,kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia (Global Fund) inatekeleza mradi wa upanuzi Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Mbeya. Wizara Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wazee na Watoto,kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia (Global Fund) inatekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la upasuaji lenye idadi ya vyumba sita , na wodi ya wagonjwa yenye uwezo wa kuchukua vitanda 89 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na Mwananchi Leo Jumatano,Desemba 8,2021, Kaimu mganga mkuu wa hosptalin hiyo,Dk Ngwilo Mwakyusa amesema kuwa miradi hiyo imefikia asilimia 78 ya utekelezaji na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni ili ianze kutoa huduma.
Aidha amefafanua kuwa kati ya vitanda 89 katika jengo la upasuaji, vitanda vya kawaida ni 72 , vyumba maalumu 10, huku vitanda saba kwa wagonjwa mahututi ambao wako kwenye uangaluzi maalumu. Miradi yote ya jengo la upasuaji na wodi ina thamani ya Sh 4.469 bilioni .
Dk Mwakyusa amesema kuwa awali wizara kwa kushirikiana na mfuko wa dunia (Global fund)imetekeleza na kukamilika kwa mradi wa jengo la dharula (EMD) kwa gharama ya Sh 877.573 milioni.
Dk ,Mwakyusa amesema kuwa uwekezaji wa Serikali utaboresha huduma za kibingwa za upasuaji katika hospitali rufaa ya mkoa na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda .
Amesema katika kutimiza miaka 60 ya Uhuru Serikali kwa kutumia mapato ya ndani na kushirikiana na wadau imekamilisha miundombinu ya majengo ya maabara ya kisasa,Jengo la kulaza watoto , wagonjwa wa ndani ,mitambo ya uvunaji wa gesi , hususan jengo la kuhifadhia maiti kupitia mpango wa maendeleo ya ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya uviko 19.
Amesema uwekezaji huo umeongeza wigo wa utoaji huduma mbalimbali hususan uwepo wa jengo la dharula la wagonjwa ambapo miaka ilikuwa ni changamoto kubwa katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Idara ya wagonjwa na nje na Dharula ,Dk ,Abraham Ngonya amesema kuwa wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha ujenzi wa jengo la dharura kwani litakuwa mkombozi mkubwa kwa wagonjwa wanaofikishwa na kuhitaji msaada wa haraka.
Amesema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na tayari vifaa vimeshafika ambavyo vinatarajia kufungwa wakati wowote kuanzia sasa na kuanza kupokea wagonjwa na kutoa huduma
Matrida Joseph Mkazi wa Forest mpya jijini hapa amesema uwekezaji huo wa Serikali umekuwa kichocheo kikubwa cha upatikanaji wa huduma bora za Afya hususan kwa akinamama wajawazito wanapofika kujifungua kwa kupata huduma bora na salama.