Hifadhi ya Taifa ya Saadani, kituo cha kihistoria, utamaduni cha kipekee nchini

Mbuyu wenye picha Hifadhi ya Saadan.
Muktasari:
- Mbali na mandhari ya kipekee ya pwani inayokutana na pori, Saadani inahifadhi kumbukumbu muhimu za kihistoria, hasa kuhusu enzi za utumwa na ujio wa dini mbalimbali.
Bagamoyo. Hifadhi ya Taifa ya Saadani, iliyoko mkoa wa Pwani, si tu kivutio cha wanyamapori na mandhari ya kuvutia, bali pia ni hazina ya historia na utamaduni wa Taifa.
Mbali na mandhari ya kipekee ya pwani inayokutana na pori, Saadani inahifadhi kumbukumbu muhimu za kihistoria, hasa kuhusu enzi za utumwa na ujio wa dini mbalimbali.
Historia ya Saadani imeelezwa leo Juni 27, 2025 na muongoza watalii wa hifadhi hiyo, Fred Nelsoni, kwa waandishi wa habari waliopo kwenye ziara ya kujifunza na kuendeleza utalii wa ndani.
Kwa mujibu wa Nelsoni, miongoni mwa vivutio vinavyochochea hisia na fikra za kihistoria ndani ya hifadhi hiyo ni mti uliotumika kutoa adhabu ya kunyonga watumwa, waliotajwa kuwa wazee au watukutu enzi za utawala wa kikoloni.
Amesema mti huo, ambao bado upo, ni ushuhuda hai wa historia ya mateso ya watumwa katika ukanda wa pwani. Aidha, ndani ya hifadhi hiyo kuna jengo lililowahi kutumika kama soko la watumwa, ambapo waliuzwa na kununuliwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Nelsoni, vivutio vingine vya kipekee ni pamoja na mti maarufu unaoonyesha taswira ya Bikira Maria. Taswira hiyo huonekana kwa mbali lakini hupotea ukiukaribia, jambo linalozidi kuibua maajabu kwa watazamaji na kufanya eneo hilo kuwa kivutio cha utalii wa kiimani.
Sanamu hiyo isiyo ya kawaida huvutia waumini na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Hifadhi ya Saadani pia ni kitovu cha tamaduni za wenyeji, ambapo kuna eneo maalumu la mikutano lijulikanalo kama Shilawadu. Hapa ndipo wanakijiji hukutana kujadili masuala ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Ngoma za asili, nyimbo, michezo ya kitamaduni na burudani mbalimbali huandaliwa, na hivyo kuhifadhi na kuendeleza urithi wa mila na desturi za pwani.
Maeneo haya ya kihistoria na kitamaduni yanatoa fursa ya kipekee kwa Watanzania na wageni kujifunza kuhusu historia ya taifa, chimbuko la dini nchini, na maisha ya jamii za pwani. Hii husaidia kukuza uzalendo na uelewa wa thamani ya urithi wa taifa letu.
Nelsoni pia amezungumzia makaburi yaliyopo katika Kijiji cha Saadani yanayodaiwa kuwa ya baadhi ya watu wa kwanza waliowasili katika ukanda wa pwani kwa lengo la kueneza dini ya Kikristo nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Nelsoni, katika Kijiji cha Saadani, kilicho karibu na Hifadhi ya Taifa Saadani, kunapatikana makaburi ya kihistoria tunayoyaita mali kale.
Waliowekwa katika makaburi haya ni James Redman, kiongozi wa taasisi ya Society Mission Trust aliyekuwa akisaidia kufikisha ujumbe wa dini katika maeneo mbalimbali; W. Siege, msaidizi wake, pamoja na maaskari waliokuwa pamoja nao wakati wakitekeleza kazi yao ya kueneza neno la Mungu.
Uamuzi wa kuwazika katika kijiji hiki ulitokana na changamoto za mawasiliano na ugenini wakati huo, na makaburi haya yamekuwa kivutio cha mali kale ndani ya Hifadhi yetu ya Saadani.