Maajabu ya mbuyu wenye picha ya sanamu wagunduliwa Hifadhi ya Saadani

Mbuyu wenye picha Hifadhi ya Saadan.
Muktasari:
- Ofisa Mhifadhi wa Saadani amesema watalii wa ndani na nje wameanza kutembelea picha ya sanamu inayofanana na ile ya Bikira Maria iliyopo ndani ya mbuyu wa kihistoria wenye umri wa zaidi ya miaka 100 ndani ya hifadhi hiyo.
Bagamoyo. Picha ya sanamu inayofanana ya ile ya Bikira Maria (Mariam), ambaye anatajwa na vitabu vitakatifu vya Biblia Takatifu na Qur’an Tukufu kuwa mama wa Yesu Kristo (Issa bin Mariam), iliyogunduliwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, imetajwa kuwa miongoni mwa maajabu mapya yanayovutia na kushangaza watalii, ndani na nje ya Tanzania.
Picha hiyo imeelezwa kuwa kivutio kisicho cha kawaida kwa macho na masikio ya wageni, na imeongeza upekee wa Hifadhi ya Saadani kama eneo la kipekee la utalii linalochanganya urithi wa kiroho, historia na mazingira asilia.
Akizungumza leo Juni 27, 2025 kuhusu picha hiyo iliyoonekana ndani ya eneo la hifadhi, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani (Sanapa), Daud Ngoro, amesema kuwa kivutio hicho kipya kinaweza kutumika kama nyenzo muhimu ya kukuza utalii wa kiimani, na hata kuwa sehemu ya hija kwa waamini, hasa wale wanaomwamini na kumheshimu Bikira Maria kulingana na mapokeo ya imani zao.
Ameeleza kuwa picha ya sanamu hiyo inaweza kuwapa wageni fursa ya kutafakari juu ya ukuu wa Mungu, uumbaji wake na imani wanazozishikilia, huku wakiwa katikati ya maajabu ya asili.
“Hili ni jambo la kipekee, si hadithi bali ni uhalisia. Picha ya sanamu hiyo, ambayo inaonekana ndani ya mti wa mbuyu, imeshuhudiwa na watalii mbalimbali wanaofika hapa, nanyi wanahabari mliotembelea hifadhi yetu,” amesema Ngoro na kuongeza.
Picha ya sanamu hiyo ipo ndani ya Hifadhi ya Saadani inayopatikana katika mikoa ya Pwani Wilaya ya Bagamoyo na Tanga, Wilaya ya Pangani ikiwa hifadhi pekee nchini inayopakana moja kwa moja na Bahari ya Hindi.”
Ngoro ambaye pia Ofisa Mhifadhi, akisimamia kitengo cha utalii alisema tayari watalii wa ndani na nje wameanza kutembelea sanamu hiyo, huku kihimiza watalii zaii hasa wa ndani kufika ili kujionea maajabu hayo pamoja vivutio vingine ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadan.
Kwa mujibu wa Mwongoza watalii katika eneo hilo, Fredy Nesto picha hiyo iligundulika mwaka 2019, ikiwa katika mbuyu wenye zaidi ya miaka 100 na ambao historia inaonyesha kwa kipindi fulani wakoloni waliutumia kunyongea watumwa.
“Sanamu hiyo ya Bikira Maria inaonekana vizuri zaidi mtu akiwa umbali wa wastani, lakini ukiwa karibu inapotea, hayo pia ni maajabu ya sanamu hiyo,” amesema Nesto.
Amesema tayari watalii kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika eneo hilo na kuitumia kwa maombi kwa shida mbalimbali walizonazo, baadhi wakirudi kueleza maombo waliyofanya eneo hilo yamefanikisha kuondoa shida zao.
Akielezea upekee wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Kaimu Mkuu wa hifadhi hiyo, Daud Ngoro amesema:
“Upkee wake hauishii tu kwenye mandhari ya kuvutia ya pwan, bali pia wanyamapori kama simba, tembo na pundamilia, huweza kuonekana wakifika ufukweni kupumzika, jambo ambalo ni adimu duniani.”
Amesema hifadhi hiyo pia ina mazalia ya kasa wa baharini, ambao huvutwa na mazingira ya hifadhi hiyo wakati wa msimu wa kuzaliana kutoka maeneo mbalimbali ya Bahari duniani.
Ngoro ametaja mchanganyiko wa maji kati ya Mto Pangani na Bahari ya Hindi kuwa unaongeza uzuri wa kiasili wa hifadhi hiyo, sambamba na uwepo wa aina nne kati ya tano za wanyama wakubwa wa Afrika, ambao ni tembo, simba, twiga na nyati, huku faru pekee akikosekana.
Amesema hayo yote kwa pamoja yanaifanya Hifadhi ya Taifa Saadani kuwa hifadhi ya kipekee nchini Tanzania na barani Afrika.