Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HESLB yafungua dirisha la mikopo kwa wanafunzi, Sh900 bilioni zimetengwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji, Profesa Carolyne Nombo

Muktasari:

  • Dirisha hilo litafunguliwa rasmi Juni 15 hadi Agosti 31, 2025. Jumla ya Sh916.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi 252,773 watakaonufaika na mkopo huo.

Dodoma. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua dirisha la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kati na ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/26 ambapo jumla ya Sh916.7 bilioni zimetengwa kuwanufaisha wanafunzi 252,773.

Aidha, bodi hiyo imezindua miongozo ya utoaji wa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/26 na kuwataka wanafunzi, wazazi na walezi kusoma na kuelewa kabla ya kuomba mikopo.

Dirisha hilo litafunguliwa rasmi Juni 15 hadi Agosti 31, 2025.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa miongozo hiyo leo Ijumaa Juni 6, 2025 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amewataka wanafunzi, wazazi na walezi kusoma miongozo hiyo na kuielewa kabla ya kuomba mikopo.

Amewataka wanaotumia vituo vya mtandao (internet cafe) kuhakikisha kuwa wanakuwa na taarifa zote kuhusu mikopo yao badala ya kuwaacha wenye vituo hivyo kumiliki taarifa zao na wakati waombaji hawana taarifa hizo.

Profesa nombo amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imeweka kipaumbele na kuongeza bajeti ya fedha za mikopo ya elimu kutoka Sh464 bilioni mwaka 2021 hadi Sh787 bilioni mwaka unaomalizika wa 2024/25.

“Katika mwaka mpya wa masomo 2025/26 utakaoanza Oktoba 2025, bajeti iliyoidhinishwa ni Sh916.7 bilioni ambayo imeongeza idadi ya wanufaika kutoka 145,000 mwaka 2021 hadi wanufaika 252,773 mwaka 2025/26 kati ya idadi hiyo, wanafunzi 88,320 watakuwa wa mwaka wa kwanza, wakiwemo wanafunzi wapya wa stashahada, wanafunzi wa shahada za awali, wanafunzi wa stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo, wanafunzi wa shahada za juu, na Samia Skolashipu.

“Aidha, wanafunzi wanaoendelea na masomo katika mwaka 2025/26 watakuwa 164,453. Mtakumbuka kuwa katika mwaka wa masomo 2022/23 Serikali ilianzisha Samia Skolashipu kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi katika masomo ya sayansi katika mitihani ya kidato cha sita ambao wanadahiliwa na kuendelea kusoma Shahada za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au Afya,” amesema.

Amesema mpaka sasa wanafunzi 3,186 wa shahada za awali na wanafunzi 80 wa shahada ya umahiri wamenufaika na skolashipu hizi zenye thamani ya Sh16.8 bilioni huku wanafunzi 18,000 wanatarajiwa kupangiwa mikopo ya stashahada yenye thamani ya Sh64 bilioni.

Profesa Nombo amesema mwaka 2023/2024, Serikali ilianzisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada katika maeneo sita ya kipaumbele ambayo ni tiba na sayansi shirikishi, elimu na ualimu, madini na sayansi ya ardhi, usafiri na usafirishaji, uhandisi wa nishati na kilimo na ufugaji ambapo kwenye bajeti ya mwaka huu mikopo hiyo itaendelea kutolewa.

Naye Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya Mikopo, Elihuruma Lema amesema mikopo itakayotolewa ni kwa astashahada, shahada za awali, ruzuku (Samia Scholarship), sheria kwa vitendo na shahada za uzamili na uzamivu.

Amesema kila mwaka bodi hiyo imekuwa ikizindua miongozo ya mikopo kutokana na mahitaji ya mikopo kubadilika kila mwaka hivyo kuwawezesha wanufaika wote wenye sifa kuomba mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Geofrey Gilagu amesema mikopo inayotolewa na Serikali imewawezesha wanafunzi wengi ambao hawakuwa na fedha za kulipia ada kusoma elimu ya juu.

Amesema bodi ya mikopo nchini imekuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye hali duni kwani imewazesha kusoma kwa kutumia mikopo inayotolewa na bodi hiyo.

Gilagu amesema watakwenda kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao namna ya kuomba mikopo ili muda utakapofika wasikose mkopo kwa kutojua vigezo na masharti vya kupata mikopo hiyo.