Haya hapa majimbo mapya ya uchaguzi, yamo Chamazi na Chato

Muktasari:
- Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza majimbo nane mapya na kata tano mpya ambazo zitatumika katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Dodoma. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza majimbo mapya manane na hivyo kufanya jumla ya majimbo ya uchaguzi kufikia 272.
Aidha, INEC imeongeza idadi ya kata tano na hivyo kufanya idadi zitakazofanyika uchaguzi mkuu kufikia kata 3,960.
Mchakato wa kupokea maoni ya kubadilisha na kugawanywa kwa majimbo ya uchaguzi na kata za uchaguzi ulianza Februari 26,2025 na kuhitimishwa Machi 2, mwaka 2025.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema walipokea jumla ya maombi 34 ya kugawanywa kwa majimbo na 10 ya kubadili majina ya majimbo.
“Baada ya kupokea maombi, tume ilitembelea na kufanya vikao na wadau katika baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa na majimbo yote yaliomba kubadilishwa majina ili kujiridhisha na taarifa za maombi zilizowasilishwa tume,”amesema.
Jaji wa Rufaa Mwambegele amesema Tume iliizingatia vigezo vinne ikiwemo idadi ya watu katika jimbo husika na kwa majimbo ya mjini ilikuwa ni watu 600,000 na vijijini ni 400,000.
Pia amesema walizingatia uwezo wa ukumbi wa Bunge kwa sasa ukumbi wa Bunge una uwezo wa kuchukua wabunge wangapi, idadi ya viti vya wabunge wanawake na jimbo moja kutokuwa katika halmashauri mbili tofauti.
Amesema baada ya kuchakata majimbo nane yaligawanywa ambapo kwa Mkoa wa Dar- es- Salaam, jimbo la Ukonga limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Kivule huku Mbagala likianzishwa Chamazi.
Kwa mkoa wa Dodoma, jimbo la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa Mtumba huku Mkoa wa Mbeya, Mbeya Mjini, likigawanywa na kuanzishwa Uyole.
Jaji wa Rufani huyo amesema kwa Mkoa wa Simiyu, jimbo la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Bariadi Mjini.
Amesema katika Mkoa wa Geita, jimbo la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Katoro huku Chato likigawanywa na kuanzishwa Chato Kusini na Shinyanga jimbo la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Itwangi.
Kwa upande wa majimbo yaliyobadilishwa, Jaji wa Rufani Mwambegele amesema tume imebadilisha majina ya majimbo 12.
Amesema katika Halmashauri Chato baada ya kugawanya jimbo hilo sasa litaitwa Chato Kaskazini (Geita) huku Nkenge likiitwa Missenyi (Kagera).
Kwa upande wa Mkoa wa Katavi, jimbo ambalo lilikuwa likiitwa Mpanda Vijijini sasa litajulikana kwa jina la Tanganyika na Buyungu ambalo sasa litaitwa Kakonko, (Kigoma).
Wakati katika Mkoa wa Simiyu jimbo la uchaguzi la Bariadi sasa litaitwa Bariadi Vijijini.
Kwa Mkoa wa Singida, majimbo matano yamebadilishwa majina, Jimbo la Manyoni Mashariki sasa litaitwa Manyoni, Singida Kaskazini sasa litajulikana kama Ilongero huku Manyoni Magharibi litaitwa Itigi.
JImbo la Singida Mashariki litajulikana kwa jina la Ikungi Mashariki, Singida Magharibi litaitwa Ikungi Magharibi.
Tume imebadilisha majina ya majimbo ya Tabora Kaskazini sasa litaitwa Uyui na Mkoa wa Tanga, Handeni Vijijini litaitwa Handeni.
Kuhusu idadi ya kata, Jaji Mwambegele amesema kutakuwa na kata 3,960 kukiwa na ongezeko la kata mpya tano za Ngerenyani na Sinonik (Longido-Arusha), Mupi, Bwawani Mjini na Shera (Rufiji-Pwani).
Amesema kata hizo zimeanzishwa na Waziri mwenye na Serikali za Mitaa.
“Natumia fursa hii kuwataarifu wananchi kuzingatia mabadiliko haya ya maeneo ya uchaguzi ili kutumia haki yao ya msingi ya kushiri kugombea na kupiga kura siku ya kupiga kura,”amesema jaji huyo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika awamu ya pili kwa mikoa 16 iliyobaki, kuhakiki taarifa zao katika daftari la awali la wapiga kura linalowekwa wazi katika kila kituo na kujiandaa vyema kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2025.
Kutokana na ongezeko hilo la majimbo kutoka 264 na Tanzania itakuwana jumla ya majimbo 272, huku Zanzibar ikibakia na majimbo 50 yaliyokuwapo awali, na Tanzania Bara sasa inakuwa na jumla ya majimbo 222.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, majina ya mamjimbo hayo yatachapishwa kwenye Gazeti la Serikali.