Hatima ya mahujaji 35 bado haijajulikana, vifo vyafikia nane

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuberi aliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo kuwa ofisi yake ilipata taarifa za watu wanne zaidi waliofariki katika tukio hilo lililotokea takriban majuma mawili yaliyopita wakati wa ibada takatifu ya kuhiji.
Dar es Salaam. Idadi ya Watanzania waliofariki kwa ajali ya kukanyagana wakati wa hija katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia imeongezeka na kufikia watu nane huku wengine 35 wakiripotiwa kutoonekana.
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuberi aliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo kuwa ofisi yake ilipata taarifa za watu wanne zaidi waliofariki katika tukio hilo lililotokea takriban majuma mawili yaliyopita wakati wa ibada takatifu ya kuhiji.
Mahujaji hao waliothibitishwa kufariki kwa mujibu wa Sheikh Zuberi ni Shafi Khamisi Ali, Hadija Shekali Mohammed, Athumani Mateso Chaulana na Ahmed Said Bawazir.
“Mpaka sasa bado tuna mahujaji wetu ambao hawajapatikana na jitihada za kujua kama wako hai au la zinaendelea kwa ushirikiano mkubwa sana kati ya ubalozi wetu wa Tanzania, Tume ya Hajj na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) waliopo Saudi Arabia,” alisema Sheikh Zuberi.
Alisema mpaka sasa ni vigumu kuthibitisha waliopotea kuwa wamefariki hadi hapo itakapothibitika na mamlaka zilizopo huko na hasa baada ya zoezi za kuwatafuta kukoma.
Kiongozi huyo aliyekuwa Makka wakati wa tukio hilo, alisema orodha ya walioripotiwa huenda ikabadilika kutokana na baadhi ya mahujaji kupatikana au kurudi kimyakimya nchini bila taarifa kwa mamlaka na kuonekana bado wamepotea.
Alitolea mfano wa mahujaji, Maimuna Ruwaly na Jalia Mushule amabo awali waliripotiwa kutoonekana wakati tayari walikuwa wamekwisha patikana.
“Hadi juzi usiku (Jumamosi iliyopita) ninavyotoka Saudia Arabia Serikali ya nchini humo ilikuwa inaendelea na zoezi la utambuzi wa miili ya marehemu lakini hata alama za vidole zinakataa kwa sababu waliofariki ni wengi na miili imekaa muda mrefu. Hivyo wanaendelea kutumia mbinu nyingine za utambuzi wa miili hiyo ili kuwabaini ndugu zetu,”alisema.
Mapema Septemba 24 mwaka huu mahujaji wapatao 769 na wengine zaidi ya 900 walijeruhiwa baada ya kutokea mkanyagano katika eneo la Minna ambako Waislamu hukusanyika wakati wa tukio takatifu la kumpiga mawe shetani.