Geita kutwaa, kugawa maeneo yaliyohodhiwa bila kuendelezwa

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella akisisitiza jambo wakati wa kongamano la vijana Wilaya ya Mbogwe. Picha na Rehema Matowo
Muktasari:
Kongamano la ‘Vijana Amkeni’ lililofanyika Wilaya ya Mbogwe ikishirikisha zaidi ya vijana 100 linalenga kuibua mabadiliko chanya miongoni mwa vijana kuanzia kwenye uthubutu na kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao kujiendeleza kiuchumi.
Geita. Uongozi wa Serikali Mkoa wa Geita umepanga kufanya uhakiki wa maeneo ya biashara na kilimo yaliyohodhiwa na watu bila kutumika ili yagawanywe upya kwa vikundi vya ujasiriamali lengo likiwa ni kutoa fursa kwa vijana kujiendeleza na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Msimamo huo umetangazwa leo Mei 31, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela wakati wa hafla ya kufunga rasmi kongamano la siku mbili la elimu ya ujasiriamali na kuibua fursa kwa vijana wa Wilaya ya Mbogwe.
‘’Naziagiza halmashauri zote mkoani Geita kusimamia uundwaji wa vikundi vya ujasiriamali ili pamoja na kutoa mikopo isiyo na riba, pia zitumike kama majukwaa ya kuelimisha vijana na kutafutia masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali,’’ amesema Shigelle
Mkuu huyo wa mkoa ametaja sekta ya kilimo kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kuwezesha vikundi vya vijana kwa kuvipatia ardhi, kuwatafutia hati miliki, mitaji na pembejeo za kilimo vijana wanaunda vikundi vya uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amewataka vijana wote wilayani humo kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali badala ya kukaa vijiwemo huku wakilalamikia maisha magumu.
‘’Vijana tuchangamkie fursa za kilimo, ufugaji na biashara zilizopo katika maeneo yetu; tusikae vijiweni kucheza pool table au kwenye vibanda umiza kuangalia mpira na filamu huku tukilalamikia maisha magumu. Kila mmoja ajishughulishe kwa kufanya kazi kwa bidii; iwe kwenye kilimo, ufugaji au biashara,’’ amesema Sakina huku akiahidi ushirikiano kutoka kwa viongozi kutafuta mitaji, fursa na masoko
Meneja wa Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF) Mkoa wa Geita, Winniel Lussingu amewataka wajasiriamali mkoani Geita kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwenye kila kipato chao kama njia ya kukuza na kuendeleza mitaji.
Mauld Mihayo, mmoja wa washiriki wa kongamano hilo ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo ya ujasiriamali, kutambua na kutumia fursa kwa vijana huku akiahidi kushirikiana na wenzake kuunda vikundi vya ujasiriamali kukidhi mahitaji ya kupata mikopo ya halmashauri kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.