Gazeti Mwananchi lashinda tuzo, Samia aahidi neema

Muktasari:
- Tuzo za Samia Kalamu Awards 2025 zilitolewa kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari ili kutambua mchango wao katika kuelimisha umma.
Dar es Salaam. Gazeti la Mwananchi limeshinda tuzo ya gazeti linalopatikana kwa uhakika Tanzania, huku Julius Maricha wa The Citizen akishinda tuzo ya mwandishi bora wa habari za nishati safi ya kupikia.
Tuzo hizo za Samia Kalamu Awards 2025 zilitolewa usiku wa Mei 5, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan, zikiwa zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Mbali na Maricha aliyeshinda tuzo hiyo, Juma Issihaka naye alikuwa miongoni mwa walioingia katika kinyang’anyiro hicho akiwania tuzo ya mwandishi wa habari mahiri Tanzania.
Akizungumza baada ya kukabidhi tuzo, Rais Samia amesema Serikali iko tayari kujenga uwezo na kuondoa changamoto za sekta ya habari hatua kwa hatua.
“Serikali iko pamoja nanyi. Kadri uwezo wetu utakavyokua basi tuko tayari tuzungumze, tuone changamoto ni zipi tuzifanyie kazi ili sekta hii ya habari iendelee vizuri,” amesema Rais Samia.
Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, amesema unazidi kukua siku hadi siku, lakini akataka utumike vyema bila kuondoa uzalendo kwa nchi.
“Uhuru wa vyombo vya habari… zungumza, sema, chambua, lakini uzalendo uwepo. Hapa ndiyo ulipozaliwa, hapa ndipo ulipotoka na utakapomalizikia. Na wengine hata ukienda nje ukamalizikia huko, tunakuja kuchangishwa huku jamani arudishwe na utarudi. Tanzania ndiyo baba, ndiyo mama, ndiyo kila kitu. Niombe sana tupende kila kitu,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuhakikisha wananchi wanapata taarifa, huku akigusia vyombo vya habari vya jamii, ikiwemo redio jamii na televisheni zilizopo vijijini zinazotoa taarifa kwa wananchi, kuangaliwa kwa ukaribu kwani ni muhimu katika kufikisha taarifa kwa wananchi.
“Hivi vikubwa vinaweza kuandika vinavyotaka, lakini vile... kuna maeneo ukimwambia kwa lugha anayoijua anaelewa zaidi kuliko Kiswahili na lugha nyingine yoyote. Kutumia vyombo vile vitatusaidia kufikisha taarifa tunazotaka zifike kwa wakulima, wajasiriamali, taarifa kwa wananchi za kisiasa na kijamii,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi tuzo ya gazeti linalopatikana kwa uhakika Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia (wa pili kulia) katika hafla ya utoaji wa tuzo za Samia Kalamu Awards iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
Kwa sababu wakati mwingine wananchi hawawezi kujua katika eneo lao kuna hospitali kubwa imejengwa ambayo anaweza kupata vipimo na kila kitu, lakini kupitia vyombo hivyo wananchi wanaweza kujua wapi wakimbilie.
Amesisitiza matumizi ya takwimu katika utoaji wa taarifa, huku akitolea mfano wa ukuaji wa uchumi akisema kuandika umeongezeka bila takwimu watu wanakuwa hawajui, tofauti na pale unapotaja.
“Unaposema umekuwa kwa asilimia 5.5, maana yake nini? Inamgusaje mwananchi wa chini, mkulima, kijana aliye kijijini? Ni kazi yenu,” amesema.
Matumizi ya Kiswahili sahihi kwa ajili ya vyombo vya habari ni muhimu kuzingatiwa ili wananchi waweze kukisikia na kukielewa, jambo litakalosaidia kukuza lugha.

Wageni mbalimbali wakiwa katika usiku wa utoaji tuzo za ‘Samia Kalamu Awards’ zinazofanyika jana Jumatatu Mei 5, 2025 katika Ukumbi wa Super Dome Masaki, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mabadiliko ya teknolojia, Rais Samia amesema uwepo wake umeifanya tasnia ya habari kushuhudia maendeleo mengi, ikiwemo kuwapo kwa televisheni mitandaoni zinazokuwa kwa kasi, jambo linalochangia mabadiliko katika namna za kupeana habari na vifaa vinavyotumika kupokea habari zenyewe, ikiwemo simu janja za mikononi.
“Maendeleo ya Tehama yanatakiwa kuwa chachu ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati, ikiwemo bei za bidhaa, masoko, fursa za kibiashara, ubunifu mpya unaoongeza tija katika uzalishaji. Hizi ni muhimu kwa Serikali, sekta binafsi na wananchi,” amesema.
Amesema taarifa hizo zinasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu uchumi na biashara, na kuiwezesha Serikali kuboresha utawala bora na uwajibikaji.
Hili linafanyika wakati ambapo Tanzania ina dhamira ya kutoka kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini na kuwa ya uchumi wa juu ifikapo mwaka 2050.
Lengo hilo limewekwa wakati ambapo idadi ya watu inatarajiwa kufikia milioni 140, ambayo ni mara mbili ya sasa, huku nusu ya watu hao watakuwa vijana.
“Ili kufikia malengo hayo, inahitajika mageuzi makubwa kimipango, mageuzi na kifikra. Katika hili, wanahabari mna mchango mkubwa kubadili mitazamo ya watu, kuwaonyesha yale ambayo yanatarajiwa kwao, yale ambayo nchi yetu inatarajia mbele yetu, yale ambayo Serikali inapanga kwa ajili ya nchi yetu. Haya yanapaswa kuelezwa kwa wananchi,” amesema.
Amesema huko nyuma, kwa kutokujua au kwa kuona kinachofanyika ni sawa, baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikiongoza kwa kuandika makala zinazobomoa nchi na kuisema.
Tofauti na sasa, makala nyingi zinajenga nchi, zinasifia nchi, zinaeleza ukweli wa yanayotokea Tanzania. Pale yanapoelezwa mabovu basi ni yale yanayohitaji kuelezwa ili Serikali ione, kila mtu aone, na hatua zichukuliwe.
“Nawapongeza kwa hilo, lakini nisisitize neno uzalendo. Wenzetu nje, zile habari ambazo wana uhakika zinakwenda kubomoa taifa lao – huzioni wala hazitoki. Lakini sisi huku, wanataka kujua kila kitu kilicho kwetu, na wanaotumika ni waandishi wa habari wetu. Semeni kuna nini, pengine kuna incentives ndogondogo tu zinazokufanya uandike na uwape,” amesema.
Amesema baada ya kupeleka kazi hizo na kurushwa katika vyombo vya nje vikubwa kama BBC, mtu hujisifu, huku akihoji: mwandishi anajisikiaje kuona nchi yake ikisemwa katika vyombo hivyo vikubwa, na ulimwengu mzima ukiona?
“Lakini, kwa sasa hatua tuliyofikia – nawapongeza sana. Mmekuwa mkiandika vitu vizuri kuhusu nchi yenu.”
Akizungumzia mchakato wa tuzo ulivyokuwa, Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe, amesema jumla ya kazi 1,131 zilipokelewa kutoka kwa waandishi wa habari mbalimbali, ambazo ziliwasilishwa kwa majaji.
Kazi hizo zilichujwa na kubakia kazi 85 ambazo ziliwekwa katika mfumo maalumu wa kupigia kura.
“Kupitia mfumo huo, kura 60,638 zilipigwa na wananchi na kupata washindi 38 katika makundi ya tuzo, ambapo wananchi walipewa asilimia 60 na majaji wakipewa asilimia 40,” amesema Shebe.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari amesema uwepo wa tuzo hizi utakuwa ni kielelezo cha kuinua hadhi na heshima ya tasnia ya habari nchini.
“Kama TCRA, tutaendelea kuhakikisha mazingira ya kazi kwa vyombo vya utangazaji yanaendelea kuboreshwa, teknolojia mpya inatumika kwa vyombo vya habari, na uhuru wa vyombo vya habari unaendelea kuimarika,” amesema.