Gambo akana kugombana na kila mtu Arusha

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo akizungumza na wananchi
Muktasari:
Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amewalalamikia baadhi ya viongozi ambao hakuwataja, akisema wanahujumu viongozi waliochaguliwa na wananchi kwa kubadilisha makubaliano ya bajeti katika jimbo hilo.
Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amewalalamikia baadhi ya viongozi ambao hakuwataja, akisema wanahujumu viongozi waliochaguliwa na wananchi kwa kubadilisha makubaliano ya bajeti katika jimbo hilo.
Gambo ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Machi 22, 2024 akizungumza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM Kata ya Lemara, akisema amekuwa akionekana akigombana na kila mtu kwa sababu ya kusimamia makubaliano.
Amesema walikaa kikao na kuwashauri madiwani wenzake waweke greda na vifaa kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), ila wakaja viongozi (ambao hakuwataja) wakatoa maelekezo mengine.
"Tulikwenda bungeni tukasimamia tukapitisha, tumekuja hapa viongozi wachache wa Serikali wanabadilisha kwenye zile kata 11 wanapeleka maeneo ambayo wana maslahi nayo. Unaona kabisa hawa viongozi lengo lao ni kuwachonganisha wawakilishi wa wananchi na wananchi wao.
“Leo mita 200 ya lami haijaanza pale wananchi wanapiga kelele wewe diwani hawawezi kukuelewa hata useme nini.
"Lakini wako viongozi wa Serikali kwa maslahi yao wamekwenda kubadilisha, tumekwenda kujenga hoja sisi bajeti iliyopita tulikaa kwenye kikao nikawashauri madiwani wenzangu tuweke greda na vifaa kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu,” amesema.
"Mwenyekiti umesikia hapa zaidi ya asilimia 80 ya changamoto za hapa ni barabara na siyo changamoto nyingine, barabara yetu kubwa na barabara za ndani na barabara nyingine Tarura hawawezi kwenda kwa sababu wao wanafanya kwa mujibu wa sheria.
“Barabara kama haijakidhi viwango wao hawawezi kuingia, lakini sisi kama jiji tukiwa na greda letu, magari yetu, milima ipo huko tukachukua vifusi tukatengeneza barabara, wakati Tarura inajipanva na barabara nyingine hali ingekuwa nzuri,’’ amesema.
Katika ziara yake hiyo, Gambo amekagua ujenzi wa madaraja, kugawa viti 60 na matofali 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za CCM katika matawi matatu kwenye kata hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa mtaa wa Korongoni, uliopo kwenye kata hiyo, Goodluck Lekajo, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni ubovu wa barabara za ndani ambazo kwa kipindi cha mvua ni changamoto hazipitiki.
"Changamoto kubwa ni barabara za ndani, zimekuwa mashimo hazipitiki wakati wa mvua na baadhi ya maeneo yanahitaji kalavati hii ni changamoto kubwa sana kwetu sisi na katika maeneo mengi ya kata hii," amesema.