Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gambo: Sina mgogoro na chama changu, tunatofautiana fikra

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na wahariri wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amesema hana mgogoro wowote na chama hicho Mkoa wa Arusha, lakini kuna baadhi ya watu wanatofautiana kwenye fikra katika kutatua changamoto za watu.

Gambo amebainisha hayo leo Alhamisi Januari 4, 2024 wakati wa mahojiano maalumu alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na mitandao ya kijamii.

Aprili 2023, Gambo alinukuliwa na vyombo vya habari akilalamika baadhi ya viongozi wa CCM wanampiga vita katika kutekeleza majukumu yake, jambo ambalo lilichochea uhasama baina yao.

Septemba 19, 2023, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Ibrahim Kijanga amesema Gambo amekuwa akitoa kauli mbaya za kukidhihaki chama hicho na viongozi wake, lakini hachukuliwi hatua zozote hali inayomtia jeuri na kiburi.

Kauli hiyo ya UVCCM ilifuata baada ya Gambo akiwa kwenye mkutano wa wakuu wa shule jijini Arusha, kusema yeye kama mbunge anafaa kuwasemea wananchi na hayuko kwenye nafasi hiyo kwa ajili ya kumfurahisha mtu wala kiongozi yoyote.

Itakumbukwa Gambo aliwahi kumtuhumu hadharani aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba anajihusisha na vitendo vya rushwa kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya Arusha.

Kufuatia tuhuma hizo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwasimamisha kazi watendaji sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwamo mkurugenzi mtendaji, Dk John Pima.

Hata hivyo, leo amebainisha hakuna mgogoro kati yake na viongozi wa chama, bali kuna  watu wanatumia fursa ya kuwa kwenye Serikali kukwamisha mambo yanayowahusu wananchi.

“Kwa maana ya chama hakuna mgogoro, lakini wapo baadhi ya watu ambao tunatofautiana kwenye fikra katika kutatua changamoto za wananchi,” amesema Gambo wakati wa mahojiano hayo na Mwananchi.

Amesisitiza Tanzania iko kwa mujibu wa Katiba na Katiba imeelekeza kila mhimili na majukumu yake, kuna Serikali ambayo kazi yake ni kusimamia shughuli za kila siku za Serikali, Mahakama kazi yake kutafsiri sheria na Bunge ambalo kazi yake ni kupitisha bajeti, kutunga sheria na kuwatetea wananchi.

“Wakati mwingine, katika kuwatetea wananchi, mtu anaweza akaona kama ni mgogoro, lakini siyo mgogoro, ni kutimiza wajibu wangu na mbunge ambaye unaogopa kutetea watu kwa sababu utaonekana unaleta mgogoro basi hiyo kazi itakuwa ni mtihani kwako,” amesema Gambo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha

Kuhusu suala la ufisadi, Gambo amesema ni changamoto kubwa kwenye Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa sababu walifanya ukaguzi maalumu na kubaini upande wa risiti feki peke yake ilikuwa ni zaidi ya Sh900 milioni.

“Kuna fedha zilitolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Arusha kama vile machinga…tulivyopaza sauti wakaanza kusema tunataka kutengeneza mgogoro, lakini Serikali ilituma timu ya CAG na kagundua karibu yote tuliyoyasema ni ya kweli na hatua zimechukuliwa,” amesema.