Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FCC yaahidi kuendelea kulinda wazalishaji wa ndani

Meneja Uendeshaji wa Alaf Limited, Aditya Chaturdevi akitoa maelezo kwa wawakilishi kutoka Tume ya Ushindani (FCC) kiwandani hapo kujionea uzalishaji wa mabati ya rangi.

Muktasari:

  • Wananchi wametakiwa kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini kuna bidhaa zisizokidhi viwango zilizo kwenye masoko hapa nchini

Dar es Salaam. Tume ya Ushindani nchini (FCC) imeahidi kuendelea kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani usio wa haki ili waendelee kuwekeza hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 23, 2025 na Mkurugenzi wa Uthibiti wa Mienendo ya Biashara Iliyokatazwa na FCC, Magdalena Utouh aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, William Erio alipotembelea kiwanda cha kuzalisha mabati cha Alaf jijini Dar es Salaam.

Amesema moja ya majukumu ya tume hiyo ni kuhakikisha ushindani wa haki unakuwepo kwa wawekezaji hasa wazalishaji wa bidhaa aina mbalimbali hapa nchini.

"Alaf imewekeza sana kwenye teknolojia mpya ya uzalishaji mabati ya rangi; inazalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu, hivyo hatutakuwa tunatenda haki iwapo tutaachia wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza bidhaa hafifu na zisizo na viwango zitakazoathiri masoko ya zile zinazolishwa na kampuni za hapa nchini,” amesema.

Magdalena ametoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini kuna bidhaa zisizokidhi viwango zilizo kwenye masoko hapa nchini.

Hata hivyo, amewataka Watanzania kuhakikisha wanatumia bidhaa zinazozalishwa nchini zenye ubora wa hali ya juu.

Akizungumzia ziara hiyo kiwandani hapo, amesema huo ni mwendelezo wa ushirikiano mwema ulioko kati ya FCC na wadau wa uzalishaji hapa nchini.

"Kupitia ziara kama hizi, uongozi wa FCC hupata fursa ya kupata maoni kutoka kwa wazalishaji zikiwamo changamoto. Tumejionea uzalishaji hapa Alaf na tumeridhika,”amesema Magdalena.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf Tanzania, Hawa Bayumi amesema, "kunapokuwa na uwanja mzuri na wenye haki katika uwekezaji, hili linatoa mwanya kwa wawekezaji kuwekeza zaidi hapa nchini.

“Mazingira hayo yametuwezesha Alaf kufanya uwekezaji mkubwa ukiwamo wa mtambo wa kisasa wa kuzalisha mabati ya rangi, mtambo huo tayari umeanza uzalishaji.”

Hawa ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia mabati ya rangi yenye ubora ambayo sasa yanazalishwa hapa nchini kwa takribani tani 130,000 kwa mwaka.

Amesema watu watakaponunua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kutachangia kuongezeka kwa fursa za ajira, sambamba na kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kwa jumla.