Fanya haya unapomwandaa mtoto anayesoma maeneo yenye baridi

Muktasari:
- Wazazi wanashauriwa kuwakinga watoto dhidi ya baridi kali wanaporudi shule kwa uchaguzi wa mavazi ya joto, mafuta maalumu, huku wadau wakitaka kalenda ya shule izingatie mazingira ya hali ya hewa, ili kuhakikisha afya, usalama na ustawi wa wanafunzi.
Dar es Salaam. Wakati likizo ikiwa inaelekea ukingoni, wadau wa afya na elimu wameainisha mambo muhimu ya kufanya unapomwandaa mtoto kurudi masomoni, hasa wale wanaosoma maeneo yenye baridi kali, huku wakitoa ushauri kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Uchaguzi wa mavazi ya kumkinga na baridi, afya na kinga ni mambo yaliyotajwa kuzingatiwa na mzazi anapomwandaa mtoto kwenda shule (bweni), huku lishe inayofaa ikitajwa kuwa kipaumbele kwa wazazi wanaoishi na watoto maeneo hayo pamoja na uongozi wa shule za bweni.
Mei 22, 2025, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza baridi kali Juni hadi Agosti katika mikoa sita, wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya baridi.
Licha ya Nyanda za Juu Kusini, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali ilitarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na maeneo ya magharibi mwa Mkoa wa Dodoma.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Julai mosi, 2025, wadau hao wametaja umuhimu wa kumpeleka mtoto kliniki kwa uchunguzi wa afya kabla ya kurudi shuleni.
Ni muhimu kuhakikisha amepewa chanjo muhimu na ana vifaa vya dharura kama vicks, mafuta ya kupaka yenye joto (hasa ya mgando mazito) na kumpa elimu ya namna ya kujikinga na baridi kwa kutokaa na nguo zenye unyevunyevu.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo anataja hatua za kumwandaa mtoto ili kujihakikishia usalama wa afya yake, akisema shule husika inapaswa kuandaa vyakula vya moto kama uji, chai na vinavyozalisha nishati ya joto.
Amesema wazazi watafute nguo nzito hasa masweta ya kutosheleza kujisitiri, yanayoweza kuwakinga na baridi. Ni muhimu kumfungashia mafuta mgando mazito tayari kuwa bora zaidi kwake.
“Mzazi lazima umtafutie sare za kumkinga na baridi, mavazi ya ndani ya joto ili yasaidie kuhifadhi joto la mwili, sweta nzito angalau mbili ili awe na ya kubadilisha, soksi nene za pamba au sufu hasa wakati wa kulala au asubuhi.
“Kofia ya sufu na glovu ili kulinda kichwa, mikono na masikio pamoja na viatu vyenye joto na visivyopitisha maji ili kulinda miguu dhidi ya baridi na unyevunyevu,” amesema.
Dk Pedro amesema vifaa vya malazi vyenye joto ni muhimu kwa watoto wa bweni ikiwemo blanketi nzito au duvet, shuka za sufu, chupa ya maji ya moto (thermo) inaweza kusaidia jioni.
Amesema kwa watoto wanaotokea nyumbani, ni muhimu mzazi kuhakikisha mtoto anaondoka nyumbani akiwa ameshiba, akipewa vyakula vya joto kama uji wa lishe, uwele au uji wa viazi vitamu.
“Mfunze kubeba chupa ya maji ya moto au thermos ikiwa inaruhusiwa shuleni. Lishe yake iwe na vyakula vinavyoongeza nguvu na kinga ya mwili kama vile ndizi, viazi, mboga za majani, maziwa na protini,” amesema.
Pia amesema ili kuwe na usalama ni muhimu wazazi kuwasiliana na uongozi wa shule kujua kipi kinatakiwa na kipi hakitakiwi ili kutovuruga utaratibu wa shule husika.
Dk Pedro amesema kipindi cha baridi kuna magonjwa mengi ambayo mtoto anaweza kuyapata yanayosababishwa na virusi mbalimbali, hivyo kujikinga ni muhimu.
“Muhimu kuwafundisha pia kupendelea kula vyakula na vinywaji vya moto, chai au maziwa, kuhakikisha unabaki na joto la mwili linalotakiwa,” amesema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Magdalena Dennis amesema ni muhimu kwa watoto wenye changamoto za ngozi kuona wataalamu ili kupata ushauri ni mafuta yapi anapaswa kuyatumia.
“Tunashauri mafuta ambayo kila mmoja anaweza kumudu kununua, lakini aina ya ngozi kuna ambao hawaruhusiwi kupaka ya mgando. Huyu akimuona mtaalamu anaweza kusaidia. Kuna Vaseline, ya nazi pia ni mazuri, mafuta ya mimea,” amesema Dk Magdalena.
Mdau wa elimu, Benjamin Nkonya amesema katika baadhi ya maeneo ikiwemo Makambako na Lushoto, baridi imekuwa kali na hujirudia katika kipindi cha Juni mpaka Julai, hivyo ni muhimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhuisha mihula.
Amesema baridi hilo husababisha watu kupasuka mpaka uso na kuugua nimonia kwa sababu ya baridi. Maeneo ya Makete, Kitulo, Matamba, kulazimisha watoto kukaa darasani huteseka, huku baadhi ya shule zikikosa kuwa na madirisha.
“Shule ziachwe zipange mihula, Tanzania ni nchi kubwa ina mazingira tofauti sana. Sasa mwanafunzi anatakiwa kukaa darasani kwa siku 194, hapo umeondoa sikukuu zote, Jumamosi na Jumapili na likizo zote.
“Changamoto tunayoiona mpaka inatuletea matatizo, Serikali kulazimisha kuwa na kalenda moja nchi nzima, imechangia wanafunzi wa shule zetu kufeli. Wizara itoe siku 194 mwanafunzi awe darasani, shule zipange sisi wenyewe anaenda likizo lini,” amesema Nkonya.