Euro milioni 15 kuhifadhi mazingira, kuongeza usalama Ziwa Victoria
Muktasari:
- Hii ni hatua muhimu inayoongeza usalama, uhifadhi wa rasilimali, na kuhakikisha Ziwa Victoria linabaki kuwa chanzo cha maisha na uchumi kwa wavuvi na jamii zinazolizunguka.
Kisumu. Baraza la Mawaziri wa nchi zinazozunguka Bonde la Ziwa Victoria limeidhinisha matumizi ya Euro milioni 15 kutoka Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na kuimarisha usalama wa Ziwa Victoria.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu katika kuongeza usalama, kulinda rasilimali za maji, na kuhakikisha Ziwa Victoria linaendelea kuwa chanzo cha maisha na uchumi kwa wavuvi na jamii zinazolizunguka.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa dharura wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) uliofanyika Kisumu, Kenya, uliolenga kujadili usalama wa wasafirishaji, wavuvi na wananchi wanaotumia ziwa hilo kwa shughuli zao za kila siku.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Caroline Karugu, Katibu wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nchini Kenya, amesema usalama wa Ziwa Victoria ni kipaumbele cha juu kwa nchi tatu zinazolizunguka.
“Takwimu za Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani zinaonyesha kuwa takriban watu 5,000 wa Afrika Mashariki hupoteza maisha kila mwaka kwenye ziwa hili. Hii ni idadi kubwa ya vifo vinavyoweza kuzuilika,” amesema Dk Karugu.
Amebainisha kuwa ujenzi wa vituo vikubwa vya utafutaji na uokoaji unaendelea katika maeneo mbalimbali ya ziwa hilo, ikiwemo Mwanza (Tanzania), Kisumu (Kenya) na Entebbe (Uganda).
Pia, vituo vingine 16 vya uokoaji vimejengwa kando ya ziwa, vikiwemo tisa nchini Uganda, vitatu Tanzania, na vinne Kenya, ili kurahisisha huduma za dharura na kuhakikisha watumiaji wa ziwa wanapata msaada wa haraka.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire, amesema idhini ya fedha hizo ni hatua muhimu inayowezesha utekelezaji wa malengo ya kamisheni, hasa katika kupambana na uchafuzi wa mazingira unaolikabili ziwa hilo.
“Tunashukuru kwa hatua hii ya kugawa Euro milioni 15 kwa ajili ya kupambana na uchafuzi wa Ziwa Victoria. Uchafuzi ni moja ya changamoto kubwa katika eneo hili,” amesema Dk Bwire.
Ameongeza kuwa ujenzi wa Kituo cha Uokoaji cha Mwanza, ambacho kwa sasa kimefikia asilimia 98 ya kukamilika, ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika juhudi za kuboresha usalama wa watumiaji wa ziwa.
Tanzania na Uganda zimetumia takribani Dola milioni 2 za Marekani kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, huku Tanzania pia ikijenga vituo vidogo vya uokoaji Musoma, Nansio (Ukerewe) na Kanyara.
Vituo hivyo vitakuwa na uwezo wa kutoa taarifa za dharura kwa wakati, huku minara miwili ya mawasiliano ikijengwa ili kusaidia uratibu wa shughuli za uokoaji na ufuatiliaji ndani ya ziwa.