EACOP na Washirika wafungua milango ya fursa kwa vijana Sekta ya Nishati

Zanzibar: Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kwa kushirikiana na Empower Limited na TotalEnergies Tanzania, imefanikiwa kuandaa Kongamano la Tatu la Nishati kwa Vijana, likiwa na kaulimbiu "Mwelekeo Unaoakisi Mustakabali wa Nishati na Fursa Zinazojitokeza."
Tukio hili liliwakutanisha jumla ya wanafunzi 130 wa vyuo vikuu kutoka taasisi mbalimbali za Zanzibar, pamoja na wadau muhimu katika sekta ya nishati. Lengo lilikuwa kuongeza uelewa kuhusu mabadiliko ya sekta ya nishati barani Afrika na kuwaonesha wanafunzi fursa za ajira na maendeleo ya ujuzi wa thamani wa nishati.
Mwanzilishi Mwenza wa Asilia Energy na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafutaji, Maendeleo, na Uzalishaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kenneth Mutaonga ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, aliwasihi vijana kukumbatia sekta ya nishati inayobadilika kila wakati huku ikiwa na fursa nyingi za ajira.
"Mahitaji ya nishati yanaongezeka duniani kote na Tanzania. Kuna fursa nyingi za ajira katika fani mbalimbali, kuanzia sheria hadi uuguzi. Kwa mahitaji ya umeme yanayoongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka, mipango kama Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere ni muhimu sana. Lakini tunahitaji uzalishaji endelevu wa muda mrefu, na hii inafungua milango kwa vijana wenye ujuzi kuingia na kuchangamkia fursa,” alisema Kenneth.
Naye, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Rasilimali Watu na Utawala kutoka TotalEnergies Tanzania, Getrude Mpangile alisisitiza kujitolea kwa kampuni yake katika kuwawezesha vijana: "Huu ni muendelezo wa dhamira yetu ya kusaidia jamii ya Watanzania. Kupitia majukwaa kama haya, tunawaandaa wanafunzi wa vyuo vikuu kuelewa mabadiliko yanayotokea katika sekta ya nishati ili wasiachwe nyuma wanapoingia sokoni. Tulianza majukwaa haya mwaka 2023 Dar es Salaam, kisha Dodoma mwaka 2024, na sasa Zanzibar ili kuwafikia vijana kote Tanzania."
Mpangile pia alitambulisha mipango mbalimbali ya TotalEnergies, ikiwemo nafasi za mafunzo kazini (internship), programu za mafunzo kwa wahitimu (za ndani na kimataifa), ufadhili wa masomo, na miradi ya nishati safi ya kupikia: "Tunawasaidia vijana kupata mafunzo ya viwandani, ufadhili wa masomo, na kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa. Mwaka jana, tulianzisha gesi ya kupikia majumbani kusaidia ajenda ya serikali ya nishati safi. Hivi karibuni, tutapanua mpango huu hadi Zanzibar."
Akiwawakilisha vijana wenzake, Swaumu Juma Ali, mwanafunzi wa uuguzi na ukunga, alizungumzia kuhusu athari kubwa ya jukwaa hili: "Nilidhani nishati haina uhusiano na afya, lakini nimejifunza jinsi ilivyo muhimu-kuanzia joto la ICU hadi uhifadhi wa chanjo. Kama wauguzi, nishati inagusa kazi yetu kila siku. Pia nimejifunza kuhusu fursa za ajira na TotalEnergies baada ya kuhitimu."