Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

EAC yaombwa kutunga sheria, sera zitakazotatua kero za wananchi

Baadhi ya washiriki wa Wiki ya Azaki wakiwa katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jijini Arusha leo, walipotembelea jumuiya hiyo. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Sheria, kanuni na sera zinazotungwa na kutekelezwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinapaswa kujibu matatizo ya wananchi wake.

Arusha. Asasi za kiraia nchini zimeiomba Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutunga sheria na sera zitakazosaidia kutatua changamoto zinazokabili jamii kwenye jumuiya hiyo.

Ombi hilo limetolewa leo na baadhi ya wajumbe wanaoshiriki Wiki ya Azaki inayoendelea jijini Arusha ambao wametembelea makao makuu ya jumuiya hiyo.

Mmoja wa wadau hao, Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help, Amani Golugwa amesema nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha sheria, sera na kanuni zake zinajibu matatizo ya watu.

"Jumuiya ya watu kwa ajili ya watu kwa hiyo unapokuwa na sheria ambazo hazitokani na watu au hazijibu matatizo ya watu zinakua sio sawa, kwa sababu unapotengeneza sheria pamoja na sera na miongozo yake ni ili kutatua matatizo au changamoto walizonazo ikiwemo uhuru wa biashara zifanyike kwa wepesi na changamoto zote za kimtangamano," amesema

Mwakilishi kutoka Shirika la Vijana la Center for Youth Zanzibar, Hija Shamte amesema kuna umuhimu wa asasi zisizokuwa za kiserikali kuweka mipango yake kulingana na dira za taifa za maendeleo kwa kuangalia vipaumbele vilivyowekwa na kuwa hiyo ni fursa kujifunza kazi za jumuiya na kuangalia namna watakavyoshirikiana nayo katika maendeleo ya nchi.

"Tuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo hivi sasa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wadau mbalimbali ikiwemo sisi Azaki kuweza kutoa maoni yetu ili kuhakikisha tunatoa maoni na tunaamini dira yetu itaakisi maendeleo na dira ya EAC,"amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Asasi za Kiraia nchini, Dk Lilian Badi amesema wadau wengi hawakuweza kujua nafasi ya jumuiya hiyo kwenye sekta yetu ya lakini wameziona fursa nyingi ambazo ziko nje ya Tanzania ndani ya EAC.

"Tumejifunza mengi kuhusu teknolojia na wadau walikuwa wazi na kuonyesha mifano ikiwemo ya wengi kupenda kushirikishana taarifa ambazo hazina usahihi, bila kufahamu vyanzo vyake ukiipata wewe unarusha ili uonekane kwenye mtandaoni unajaribu kuelewa sheria zinasema nini ili tusiishie kwenye matatizo kwani hatuwezi kuikimbia teknolojia na teknolojia ni sehemu ya sisi na ni sehemu ya maisha yetu," amesema Dk Lilian.

Mkuu wa kitengo cha mauzo kwa masoko ya Kimataifa kutoka Benki ya Stanbic, Amal Baziad amesema benki hiyo ina mpango wa  kuboresha huduma za kifedha ili kuhudumia watu wenye ulemavu ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Amesema mapinduzi ya teknolojia hasa katika sekta ya fedha ni lazima yanufaishe makundi yote katika jamii ikiwemo watu wenye ulemavu na watu waishio maeneo ya pembezoni.

"Linapokuja suala la huduma na bidhaa za benki, watu wenye ulemavu mara nyingi wanahisi kutohudumiwa. Ikiwa tunafikiria kuleta mapinduzi ya ujumuishaji wa kifedha, tunahitaji pia kuwaleta watu wote," amesema.