Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Tulia atema cheche, ugawaji Jimbo la Mbeya Mjini

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiagiza Serikali kufanyika tathimini ya kina ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wakati wa kipindi cha maswali na majibu Alhamis Aprili 20,2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amezungumzia kugawanywa kwa jimbo la Mbeya Mjini analoliongoza, akisema haogopi mtu, na kwamba yeyote anayelitaka aende kupima kina cha maji kama kinamtosha.

Pia, amesema hahofii kukabiliana na aliyewahi kuwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu,’ endapo watakutana katika kinyang’anyiro cha kugombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliolalamikiwa na vyama vya upinzani, Dk Tulia alishinda kwa kura 75,225 dhidi ya Sugu aliyepata kura 37,591.

Kiongozi huyo wa Bunge, alitoa msimamo huo jana katika mahojiano maalumu na kituo cha Wasafi yaliyofanyika katika makazi rasmi ya Spika, jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, mahojiano hayo yalijikita kuhusu mgawanyo wa jimbo la Mbeya Mjini na maisha yake ndani ya Serikali hadi kuingia kwenye siasa.

“Ubunge wangu haijalishi jimbo limegawanya au halijagawanywa, mimi ndiye mbunge, kama nilimtoa mtu katika kata 36, ataweza kunitoa kata zikiwa chache kweli? Mbona itakuwa mtihani, zikibaki kata 36 nitawafyeka.

“Nisingeshangaa kujadiliwa na wao, tena napenda sana wao wameanzisha huo mjadala, nimefurahi na wanaposema watanifuata, nataka wajipime kama wanaona kina cha maji kinawatosha waje, kama niliwatoa na kata 36 wataniweza wapi na kata chache,” alihoji Dk Tulia.

Katika mahojiano hayo, Spika aliulizwa kama hatishiki kukabiliana na Sugu katika uchaguzi ukiwa huru na haki, hasa ikizingatiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wapinzani wengi waliamini kuna nguvu ya ziada ya dola iliyotumika kuwabeba washindi.

“Sihofii kupambana naye, niko vizuri, sina wasiwasi na hilo naomba Mungu aniweke. Nimefanya kazi kubwa, nyie nendeni Mbeya Mjini mtaamini,” alijinasibu Dk Tulia, aliyewahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aliongeza: “Hata yeye (Sugu) anajua hao wanaojadili mtandaoni nadhani hawajafika Mbeya wala hawapajui wala kuwasikia Mbeya, sasa nyie (waandishi) mnakaribishwa halafu mtawanyike na mkaulize hapa Mbeya Mjini mbunge ni nani, mtapata majibu.”

Pia, Dk Tulia alieleza sababu za kutaka jimbo hilo kugawanywa akisema suala hilo halihusu Mbeya Mjini pekee, bali katika majimbo mbalimbali makubwa na hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma karibu.

Hata hivyo, jitihada za kumpata Sugu kuzungumzia mpango wa mgawanyo wa jimbo hilo na kile alichokieleza Dk Tulia kwamba yuko tayari kuchuana naye katika uchaguzi mkuu ujao, hakuweza kupatikana kwani simu yake ya mkononi haikupokelewa wala kujibu ujumbe mfupi aliotumiwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote maarufu China akizungumzia hilo juzi, alisema watasimamisha wagombea majimbo yote yatakayogawanywa, likiwemo la Mbeya Mjini.

“Ni jambo jema sana alilowasilisha bungeni Spika wa Bunge, Dk Tulia lenye kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya, lakini sisi kama chama tunaona ni vyema kuongeza nguvu kusimamisha majimbo yote mawili, likiwemo la Mbeya Mjini,” alisema.


Ugawaji majimbo

Kauli hiyo ya Dk Tulia ilikuja baada ya juzi Bunge kutaarifiwa kuwa kiongozi huyo wa Bunge ni miongoni mwa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao ili kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu na hivyo kurahisisha shughuli za maendeleo.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Katika swali la nyongeza kwa Serikali, Mwakagenda aliuliza ni lini Serikali italigawa jimbo la Mbeya mjini kutokana na ukubwa wake.

Juzi baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, mjumbe wa kamati ya Chadema, Godbless Lema alisema hata jimbo la Mbeya Mjini likigawanywa watamfuata Dk Tulia huko huko anapogombea.


Jimbo la Mbeya

Dk Tulia ambaye Juni mwaka huu atafikisha miaka 20 ya ndoa yake, alieleza namna mchakato wa kuligawa jimbo la Mbeya Mjini lenye kata 36 unavyotakiwa kuwa endapo Serikali itaridhia.

“Kwa jiografia ya jimbo la Mbeya Mjini kuna bonde la Uyole ni kama vile maaeno yapo mawili, sasa kuna watu wa Uyole na wengine wa upande wa mjini. Ukiligawanya kata zilizopo bonde la Uyole zitaingia Uyole, zilizopo mjini zitaingia Mjini,” alisema.

Dk Tulia alifafanua Mbeya ya mjini haijanyooka kama Morogoro bali ipo kama bakuli kutokana na kuzungukwa na milima. Alisema kuwa namna ya kuligawa, inabidi watu wasifuate huduma, bali wasogezewe.

“Ningependa ligawanywe kwa watu kuwasogezea huduma wa mjini wahudumiwe mjini na Uyole wahudumiwe Uyole ili kupunguza umbali,” alisema.

Dk Tulia alisema ikitokea Mbeya Mjini ikagawanywa na kuwa majimbo mawili, basi jimbo la Uyole litakuwa na kata chache kwa kijiografia. Kutokana na hilo, Dk Tulia alisema kuna kata 14 zitaingia Uyole na 22 zitabaki Mbeya Mjini.

Hata hivyo, Dk Tulia alisema suala la kugawa jimbo la Mbeya Mjini sio jipya, kwa sababu hayati Rais John Magufuli alivyopita Mbeya Mjini wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi suala hilo.

Dk Tulia alisema hayati Magufuli aliwaambia wananchi kwamba endapo watakichagua CCM katika kata zote 36 na mbunge, basi jimbo hilo litagawanywa. Alisema kwa vile ahadi ilikuwa mwaka 2020, michakato yake ilishaanza na sio jambo jipya.

“Sio jambo jipya kwamba watu wanashtuka sasa hivi, kama vile ni jambo la ajabu hapana. Michakato ilishaanza, vikao vya halmashauri, kisha baraza la ushauri la wilaya na baraza la ushauri la mkoa,” alisema mwanasheria huyo mama wa watoto wawili.

Dk Tulia alijivunia mafanikio yanayotokana na kazi alizozifanya kwa kusema kuwa wakati wa kampeni ahadi zilikuwa nyingi, zikiwemo za Mbunge na Ilani ya CCM.

Kati ya ahadi hizo kwa mujibu wa Spika Tulia, ilikuwa ni kujenga barabara ya njia nne kuanzia Igawa hadi Tunduma kwa kilomita 218, ambapo wameomba awamu ya kwanza ya ujenzi ianzie Mbeya Mjini ili kupunguza changamoto ya foleni.


Siasa za Ukawa

Katika mahojiano hayo ya jana, Dk Tulia alisema yeye ni miongoni mwa watu waliokuwapo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioasisiwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Umoja huo ulioundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD pamoja na baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa na Rais akiwemo Dk Tulia, ulikuwa na lengo la kusikiliza maoni ya wananchi kisha kutoa mapendekezo katika rasimu ya Katiba.

“Baada ya Rasimu ya Katiba kuletwa na Ukawa ilivyoanza, ilikuwa lazima tukutane mahali kujadili na kuiboresha. Sasa tunapataje uhalali lazima tujiunde na Katiba inatengenezwa na wananchi, basi ikaitwa Ukawa.

“Yeyote aliyekuwa anataka jambo jema na kusikiliza wananchi wanachosema alikuwa anakwenda katika Ukawa, tofauti iliyokuwa ikitafsiriwa nje,” alisema Dk Tulia.

Hata hivyo, baadaye Umoja huo ulitoka ndani ya Bunge na kususia mchakato huo na kuwaacha wabunge wa CCM na baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa na Rais wakiendelea kuijadili rasimu ya Katiba hadi kupatikana kwa Katiba Pendekezwa.


Ripoti ya CAG

Kuhusu mapendekezo ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutofanyiwa kazi na Bunge kutochukua hatua za kuiwajibisha Serikali, Dk Tulia alisema ikitoka inakuwa jambo linalohusika na mapendekezo.

“Yale mapendekezo ya CAG haiambii Serikali bali analiambia Bunge, kwa sababu kikatiba Bunge ndilo limepewa kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali na sio chombo kingine. CAG anafanya ukaguzi kwa niaba ya Bunge.

“Sasa Bunge linaamua kuhusu taarifa ya CAG na linapeleka maazimio na sio mapendekezo kwa Serikali. Inapokuja taarifa ya CAG Bunge linapeleka Serikali maazimio ambayo ni uamuzi wa Bunge,” alisema

Alisema baada ya CAG kuwasilisha taarifa yake, kamati za Bunge zitaichambua na kuwaita waliotajwa kwa lengo la kutoa maelezo, akisema katika hizo kamati CAG anakuwa ni sehemu ya washiriki sio Bunge peke yake.


Aina ya Bunge analotamani

Alipoulizwa anatamani Bunge lijalo liwe la namna gani, Dk Tulia alisema ubunge ni uwakilishi wa watu waliochaguliwa na wananchi katika maeneo mbalimbali, hata hivyo wakati wa Bunge lililopita uamuzi uliokuwa ukifanyika hauna tofauti na Bunge la sasa.

“Lazima ujue lengo la chama chochote ni kushika dola, sasa nikiwa Mwana-CCM nisingependa tupoteze jimbo lolote. Nadhani watu wanataka kusikiliza mawazo ya wengine wanasemaje, lakini kuhusu uamuzi unafanywa na walio wengi bungeni, upinzani walikuwa wanasema hapana.

“Watu walichopungukiwa ni ile michango labda wanatamani kusikiliza mtu akitema cheche.Hakuna mvuto uliopotea, kama Spika naona wabunge wanachangia na kueleza hoja za majimbo yao,” alisema.


Alivyozima hoja ya Lissu

Alisema wakati anaanza kazi ya unaibu spika aliingia bungeni, kukiwa na upinzani wengi walijipanga kuzuia baadhi ya wageni wasiingie, akiwemo Rais wa wakati huo wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mwaka 2015 kutokana na uchaguzi wa Zanzibar kuahirishwa.

“Aliibuka Tundu Lissu (aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki) na vitabu vyake, akaifungua Katiba ya Zanzibar akiomba mwongozo… nikamwambia tulia kwanza. Lissu alisimama akasema kwa mujibu wa Katiba, Zanzibar hakuna Rais inakuwaje mnatengua kanuni ili Dk Shein aingie.

“Lissu alisema hakuna rais wa Zanzibar atakayeingia humu ndani kwa sababu hayupo, nikamwambia ili useme rais hayupo Zanzibar, niambie aliyeapishwa nani? Taabani, nikaahirisha shughuli za Bunge ili kuruhusu viongozi wakuu akiwemo Rais (hayati John Magufuli) kuingia ndani ya ukumbi.”


Miaka 20 ya ndoa

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa ni ana watoto wangapi na yupo katika ndoa kwa kipindi gani, Dk Tulia alisema ana watoto wawili na Juni mwaka huu atafikisha miaka 20 ndani ya ndoa huku akibainisha kwa sasa sio mtu anayependa kunywa chai kulingana na mazingira yaliyopo.

“Huwa sinywi chai asubuhi kwa sababu ratiba zangu zinakuwa ngumu, nikiamka asubuhi natafakari kwanza kwa kujiuliza nimemaliza majukumu au kazi zangu? Baada ya hapo namuomba Mungu, naelekea mazoezi.

“Nikamaliza mazoezi najiandaa na lazima ikifika saa mbili na nusu nianze safari kuelekea bungeni, kwa hiyo hakuna nafasi ya kunywa chai hapo, lakini familia inapata kifungua kinywa, ila kupika nipo vizuri, ingawa sipiki kulingana na ratiba zangu,” alisema Dk Tulia.


Mabasi kutembea saa 24

Alishauri kuwekwa kwa mazingira kwa madereva watakaofanya kazi wakati huo kupokezana huku akisema maeneo ambayo yana changamoto za barabara mabasi yazuiwe.

“Yale maeneo ambayo barabara hazina shida,yaani hapa Dodoma hadi Dar es Saalaam kutembea usiku kuna shida gani, kuna misitu barabarani inayotishia usalama?Maeneo yenye shida magari yasitembee


Katiba

Alipoulizwa msimamo wake wa Katiba mpya alisema,“Ukisema Katiba mpya sio yale yaliyopita unayatupilia mbali bali unayachukua, unayaboresha na kuongeza mapya yaliyojitokeza unapata Katiba Mpya. Nisingependa kusema tuendelee na viraka, bali yale yaliyokusanywa kuanzia mwaka 1977, tuongeze mapya tupate Katiba Mpya.

“Hoja kuwa Katiba iliyopo tunataka iwe mpya kwa kuboresha yaliyopo na kuongeza mapya. Mapya yapi tunataka yaongezwe, yaongezwe na zamani yapi yarekebishwe, yarekebishwe, ndio itakuwa Katiba yetu,” alisema Dk Tulia.