Prime
Dk Nchimbi: Kupindisha haki chanzo cha vurugu kwenye taasisi
Muktasari:
- Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (Tapsea) kimetakiwa kutambua uzito wa majukumu yao kama sura na lango la ofisi, hivyo kuhudumia kwa kuzingatia weledi, maadili pamoja na utunzaji wa siri.
Arusha. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema kinacholeta vurugu kwenye taasisi nyingi ni kupindishwa kwa haki pamoja na kukosekana kwa uwazi.
Pia , amekitaka Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (Tapsea) kutambua uzito wa majukumu yao kama sura na lango la ofisi, hivyo kuhudumia kwa kuzingatia weledi, maadili pamoja na utunzaji wa siri.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Alhamisi Mei 21, 2026 alipokuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa 13 wa kitaaluma wa chama hicho, uliokutanisha washiriki takribani 5,500 nchini.
Amesema kinacholeta vurugu kwenye taasisi mbalimbali ni kupindisha haki na kukosekana uwazi, hivyo kuwataka Tapsea ambao wanatarajia kufanya uchaguzi wao kesho, wahakikishe haki inatendeka.
“Mnapokuja kwenye uchaguzi wenu, chagueni viongozi makini watakaotoa taasisi yenu kwenye hatua moja, wapimeni kwa uwezo na sifa zao na siyo sura, makabila au dini zao, wanaosimamia uchaguzi, hakikisheni uwe huru na wa haki nasisitiza hapo.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA), Zuhura Maganga,akizungumza katika mkutano wa 13 wa kitaaluma wa chama hicho leo Alhamisi Mei 20, 2026 mkoani Arusha.
“Hakikisheni uchaguzi wenu hautengenezi malalamiko, kila mgombea apewe haki yake, kila mgombea aone haki imetendwa isiwe habari ya kificho, mtu akigombea akaona kura zinahesabiwa yeye mwenyewe au wakala wake na akapata kura mbili haimuumi,” amesema.
“Haimuumi kuliko akiambiwa kura ilibadilika na mtu anaanza kupewa maneno kuwa, kura ilibadilika kwa sababu hakuwepo kwenye chumba au hakuwepo mwakilishi wake. Kwepeni kama ukoma majaribio yoyote ya kugandamiza haki za wagombea na hizi ni haki za wapigakura, mpigakura akipiga kura yake lazima iheshimike.”
Makamu huyo wa Rais amesema: “ Serikali inatambua uzito wenu kama sura na lango la ofisi, hakuna mtu anafikia uongozi au menejimenti kabla hajapita, kwa hiyo zingatieni weledi, maadili na utunzaji wa siri.
“Mtu anaanza kutambua au kupata hisia ya umuhimu wa taasisi aliyoingia kuanzia tabia ya mwandishi mwendesha ofisi, mtu anafika kwenye ofisi analia machozi, inategemea mwandishi mwendesha ofisi kampokea vipi, akimwambia karibu, pole sana, anamshika anampa pole, anapata faraja kuwa hii ofisi aliyofika atasaidika.”
Amesema mgeni anapokuja kwenye ofisi apewe matumaini na siyo kila anayekuja lazima asaidiwe, lakini lugha nzuri na mapokeo mazuri ni tiba.
Kuhusu utunzaji wa siri na weledi, amesema kuna tatizo la watu wachache ambao wakiwa na siri inawapa tabu. Dk Nchimbi ameongeza kuwa vyuo viendelee kuzalisha watumishi mahiri wa kada hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imejikita kuboresha utumishi wa umma kwa kuweka mazingira ya kazi bora na wezeshi ili kuongeza tija kwa watumishi wa umma.
Amesema bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2025/26, iliidhinisha ajira mpya za watumishi wa umma 42,500 kwa kada mbalimbali, kupandisha vyeo watumishi wa umma 219,042 na kuwabadilishia muundo watumishi 6,198 na watumishi 18,093 wamelipwa malimbikizo ya mishahara.
Ridhiwani amesema mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imepanga kuajiri watumishi wapya 45,000 wa kada mbalimbali, imepanga kuwabadilishia muundo 5,865 na kuwapandisha madaraja 34,921.
“Serikali imedhamiria kukamilisha umaliziaji wa chuo cha umma kule Kange, Tanga lakini pia tunaendelea kuendeleza kule Singida, tumeendelea kununua vifaa bikiwemo baadhi ambavyo Mwenyekiti wa Tapsea ameeleza, kwa ajili ya maendelezo ya taaluma hii,” amesema Ridhiwani.
Mwenyekiti wa Tapsea, Zuhura Maganga amesema waandishi waendesha ofisi kwa sasa wana fursa ya kupata elimu ya juu ngazi ya shahada na uzamili kwenye baadhi ya vyuo kikiwamo Chuo cha Utumishi wa Umma Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hali inayofanya kuwa wataalamu wenye viwango vya kimataifa katika kada hiyo.
Kuhusu changamoto zinazoikabili kada hiyo, Maganga amesema ni upungufu wa vitendea kazi kama kompyuta, uhaba wa walimu wabobezi na ufinyu wa bajeti.
“Tunaiomba Serikali iongeze vitendea kazi katika vyuo vya kada hii, iajiri walimu wabobezi, kukifanya Chuo cha Uhadhili Tabora kuwa ‘centre of excellence’ (kituo cha umahiri),” amesema Maganga.