Dk Mpango: Nikistaafu, nitaingia rasmi kwenye kilimo

Muktasari:
- Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) kimeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, huku Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango akitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini.
Iringa. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema muda wake wa kulitumikia Taifa kupitia nafasi za uongozi unafikia mwisho na sasa anajiandaa kwenda kwenye kilimo.
Tayari Dk Mpango ameshaomba kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupumzika, naye akamkubalia na mkutano mkuu CCM wa Januari 18 na 19, 2025 ulimpitisha Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
Dk Nchimbi atakuwa bega kwa bega na mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye naye alipitishwa na mkutano huo.
Kabla ya Rais Samia kumpendekeza Dk Nchimbi, aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Dk Mpango mara kadhaa alimwomba kupumzika, lakini alikuwa hamjibu na sasa wakati umefika kusikiliza ombi lake.

Leo Jumatano, Mei 14, 2025 katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho mkoani Iringa, Dk Mpango amesema baada ya kufanya kazi serikalini kwa muda mrefu, sasa ni wakati wake wa kupumzika na kutoa nafasi kwa vijana kuongoza nchi.
“Nimefanya kazi kwa bidii kwa miaka mingi nikilitumikia Taifa. Sasa naona ni wakati wa kupumzika na kushika jembe. Nataka nijikite kwenye kilimo, ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wetu,” amesema Dk Mpango.
Amesema hatua hiyo haimaanishi ameachana na uzalendo au dhamira ya kulitumikia Taifa, bali ni mabadiliko ya uwanja wa kutolea mchango wake, kwani kupitia kilimo ataendelea kusaidia Watanzania kwa njia tofauti, huku akihamasisha vijana kuliona shamba kama sehemu ya fursa, si adhabu.
"Tanzania ina vijana wengi wenye uwezo mkubwa na mawazo mapya, hivyo ni muhimu wakapewa nafasi zaidi ya kushika hatamu za uongozi na maendeleo ya nchi," amesema Dk Mpango.
Katika hatua nyingine, Dk Mpango amewataka vijana nchini kutumia elimu, maarifa na teknolojia kubadilisha maisha yao na ya Taifa kwa ujumla.

Aidha, Dk Mpango ametoa rai kwa viongozi wa mikoa kushirikiana na taasisi mbalimbali za misitu na utafiti kuanzisha bustani za mimea zitakazosaidia kutoa fursa kwa vijana kutafiti na kutengeneza dawa zitakazowasaidia Watanzania.
Amesema utafiti na utengenezaji dawa kutokana na miti ya asili ni jambo muhimu, hivyo kila mkoa una wajibu kuhakikisha unalinda miti ya asili na kufanya uhifadhi kwa manufaa ya Watanzania.
“Katika Taifa letu kunahitajika sana kuwa na tafiti zinazolenga kukabiliana na changamoto zilizopo katika jamii, hususan teknolojia duni na tija ndogo katika sekta za uzalishaji.
“Tuna changamoto nyingine ya uongozi wa maslahi, badala ya viongozi kujali maslahi ya wanyonge na walio wengi, basi wanajali maslahi ya matumbo yao. Tuna changamoto ya siasa chafu, ukatili dhidi ya wanawake na watoto… tujielekeze kufanya tafiti zitakazojibu changamoto hizo,” amesema.
Katika kusisitiza hilo, amesema wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanaanzisha miti dawa kwani inapotea.
“Viongozi wote wanaohusika waanzishe bustani maalumu kwa ajili ya kupanda miti dawa katika kila mkoa, na vijana wetu watapata sehemu nyepesi zaidi za kufanya tafiti,” amesema Dk Mpango.
Pia, amesema katika kukabiliana na uhaba wa walimu kwenye vyuo vikuu, ni muhimu taasisi za vyuo kuendelea kufundisha na kufanya jitihada mahsusi kuwatumia wanafunzi bora wanaopatikana ili wawe wakufunzi katika vyuo hivyo.
Vilevile amewasihi kufanya ushirikiano na vyuo vya nje ya nchi kwa ajili ya kupunguza uhaba wa walimu katika vyuo vikuu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema Serikali wakati wote imetoa kipaumbele kwa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na utoaji wa huduma mbalimbali, ikiwemo elimu.
Amesema katika kutimiza jukumu hilo, Serikali imeendelea kuwekeza katika kujenga mazingira rafiki, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya maji, umeme, barabara na mengineyo, ili kuhakikisha sekta binafsi zikiwemo taasisi za elimu zinafanya kazi katika mazingira ambayo ni wezeshi na hivyo kutoa elimu bora na ya ushindani.
Awali, Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa, Romanus Mihali amesema Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), linashukuru kwa dhati Serikali na wadau wengine waliosaidia kukamilika kwa mradi wa jengo la Science Park, ambalo linajumuisha kituo cha afya.
Amesema lengo ni kuhakikisha chuo hicho kinatoa mchango kwa jamii katika nyanja mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya, hivyo kuleta mabadiliko chanya kwa jamii kama taasisi inayohudumia wananchi.
Askofu Mihali amesema bado upo uhitaji wa vifaa tiba ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wanafunzi, wafanyakazi na wananchi wa mkoa wa Iringa.