Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mpango awapa wasomi kibarua upatikanaji wa Dira ya Maendeleo

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati akifungua kongamano la kwanza la kitaifa kuhusu maandalizi ya dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Juni 8, 2024.

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametaja mambo matano akiwataka wasomi na wananchi kuyafanyia tafakuri ili kujumuishwa katika dira hiyo kwa maendeleo ya Taifa.

Dar es Salaam.  Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametaja mambo makuu matano, ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana akisema ni muhimu yakafanyiwa tafakuri na wanazuoni pamoja na wananchi ili kuingizwa katika maandalizi ya dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

 Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Juni 8, 2024 wakati akifungua kongamano la kwanza la kitaifa kuhusu maandalizi ya dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, lililofanyika  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema dira ya mwaka 2050 inapaswa zaidi kuwa ya vijana kwa ajili ya vijana, kwa sababu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 imebainisha wazi kuwa asilimia 77 .5 ya Watanzania ni vijana na watoto kati ya miaka 0-35. Huku kundi la vijana kuanzia miaka 15-35 wakiwa asilimia 34.5.

“Kwa maana hiyo dira ya 2050 lazima itambue mahitaji yao na ibebe matamanio ya kundi hilo kubwa la watu wetu, ni muhimu dira hiyo ikabainisha fursa na changamoto za muundo na mwenendo wa idadi ya watu katika Taifa letu.

“Sasa fursa hizo ni pamoja na kutambua nguvu kazi ya vijana katika kuharakisha maendeleo, pamoja na mambo mengine itatulazimu kama Taifa kuweka nguvu katika maendeleo ya kujenga ujuzi, stadi za kazi, upanuzi wa shughuli zinazogusa vijana na teknolojia, sanaa na burudani, kilimo janja na biashara changa,” amesema Dk Mpango.

Dk Mpango, aliyewahi kuwa Katibu wa Tume ya Mipango, amesema dira ya 2050 ni muhimu ikajengwa kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa dira inayofikia ukomo mwaka 2025, kwa kuimarisha na kutumia kama nyenzo ya kuongeza kasi ya mabadiliko makubwa.

“Ni muhimu dira ikabainisha fursa za uwezo na fursa kubwa ya nchi kwa kuzingatia mahitaji ya  ndani na nje ya nchi, eneo moja la kutazamwa ni rasilimali za madini zilizopo, itakuwa vema uvunaji wa madini hasa ya kimkakati upangwe kwa uwezo mkubwa ili kunufaisha Taifa, kwa kuweka viwanda vya uchenjuaji wa madini hayo hapa nchini.

Amesisitiza kuwa ni muhimu madini yakachakatwa nchini ili kuwa na uwezo wa kutengeneza bidhaa mbalimbali badala ya kusafirishwa yote nje ya nchi.

Pia, Dk Mpango amesema dira mpya ijikite katika kubadilisha mfumo wa uzalishaji katika sekta za kilimo na mifugo ili kuinua tija maradufu na Taifa kunufaika na matunda ya uchumi wa buluu kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za maji.

“Ni muhimu wadau kutoa maoni ya namna mabadiliko makubwa katika kilimo na ufugaji yanayoweza kufanyika,”amesema.

Mbali na hilo, amesema dira 2050 itapaswa kubainisha kwa undani changamoto kuu za ndani na nje pamoja na zile za zamani zinazoibukia ambazo ni kikwazo kikubwa katika nchi yetu, katika kupata maendeleo haraka.

“Itakuwa vema zikibainishwa kwa ukweli na uwazi, changamoto kubwa ninayoiona ni kuhusu upungufu katika utawala bora na uwajibikaji katika ngazi mbalimbali, masuala ya maadili na utamaduni,” amesema.

Dk Mpango amesema pamoja na kutambua mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utawala bora, lakini bado kuna tatizo la utawala kama linavyobainishwa katika taarifa za Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Kama maeneo haya hatutayapatia mikakati sahihi kwenye dira na mikakati ya utekelezaji wake, kwa maoni yangu hata dira ya 2050 ingeandikwa kiasi gani, mafanikio yake yatakuwa madogo.

“Hivyo dira ya 2050 itafaa kutupatia mwelekeo kuhusu kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, kufanya mageuzi ya utamaduni ambayo kwa hali ya sasa yanatukwamisha. Mathalani tabia iliyojengeka kwa jamii ya kulalamikiwa kutofanya kazi kwa bidii,”ameeleza.

Amesema tabia nyingine ni matumizi mabaya muda, kupenda anasa, kukosa uaminifu, kulaumu Serikali pekee, kutojali mali ya umma, kukithiri kwa ubinafsi, mmomonyoko wa maadili, ikiwemo tatizo sugu rushwa.

“Haya yote yanatupasa tuwe na mwelekeo mpya katika dira ijayo, sambamba na kujenga kada ya uongozi, inayojikita kuchochea maendeleo ya nchi.

Sambamba na hilo, Dk Mpango ameshauri ni vema dira mpya ikajenga uelewa wa pamoja wa misingi ya mikakati endelevu ya kuhakikisha ulinzi wa Taifa letu, mipaka, watu wake na rasilimali za taifa zikiangaliwa kama mboni ya jicho.

“Katika hili ujenzi imara wa jeshi la nchi yetu upewe kipaumbele katika dira ya 2050 sambamba na kuongeza utafiti, ili kuendana na mabadiliko yaliyopo,” amesema Dk Mpango

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema hadi sasa wameshakusanya maoni kutoka wananchi zaidi ya 800,000 kwa njia mbalimbali, simu za mkononi na tovuti.

“Watu wengi wamejitokeza hasa vijana kati ya 15 hadi 35 ambao ni sawa na asilimia 85 waliotoa moani yao, Lakini pia tulifanya utafiti wa kaya wa zaidi 7,000 nchi nzima, lakini timu yetu ya dira itaendelea kukutana na makundi mbalimbali,” amesema Profesa Kitila.