Dk Biteko ataka watendaji serikalini kufikia wananchi vijijini

Muktasari:
Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka watendaji wa Serikali kuwatumikia wananchi kama ambavyo maelekezo ya Serikali yanavyosema ikiwemo kufika hadi vijijini kutatua kero na changamoto zao.
Sengerema. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka watendaji wa Serikali kuwatumikia wananchi kama ambavyo maelekezo ya Serikali yanavyosema ikiwemo kufika hadi vijijini kutatua kero na changamoto zao.
Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 23, 2023 alipokuwa akiwasalim wananchi wa Sengerema waliojitokeza kumlaki akielekea kufungua maonesho ya sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya madini yanayofanyika mkoani Geita.
Amesema Serikali imewaweka watendaji wake kwenye maeneo mbalimbali ili huduma za kiserikali ziwafikie wananchi kwa wakati hivyo wanatakiwa kwenda vijijini kuwatumika wananchi na siyo kukaa maofisini.
“Serikali haitaki kusikia wananchi wanalalamika kwa kukosa huduma kwenye maeneo yao kila mtu kwa nafasi yake na eneo alilopangiwa anatakiwa kuchapa kazi,”ameseme Dk Biteko
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesifia utendaji wa Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu akidai anawapigania wananchi wake anapokuwa Bungeni hivyo wanatakiwa kumuunga mkono.
Naye Tabasamu licha ya kumpongeza Dk Biteko kwa nafasi aliyonayo sasa, amesema Serikali imelitendea haki jimbo lake kutokana na miradi ya maendeleo kutekelezwa na mingine kuendelea kutekelezwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Marco Makoye amesema Sengerema iko salama katika nafasi ya utendaji wa chama akiwataka watendaji wa Serikali kuendelee kutekeleza ilani ya chama hicho.