Dk Biteko ataka taasisi za umma zijitathmini

Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ameagiza kuhakikisha sera ya taifa ya ufuatiliaji na tathmini inakamilika haraka ili ianze kutumika kama nyenzo muhimu ya kuongoza mwelekeo wa serikali na wadau katika kutekeleza jukumu la ufuatiliaji na tathmini nchini.
Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ameagiza kuhakikisha sera ya taifa ya ufuatiliaji na tathmini inakamilika haraka ili ianze kutumika kama nyenzo muhimu ya kuongoza mwelekeo wa serikali na wadau katika kutekeleza jukumu la ufuatiliaji na tathmini nchini.
Aidha amezitaka taasisi za umma nchini kujifanyia tathmini ya utayari ili kubaini changamoto na fursa walizonazo katika utekelezaji wa mfumo huo.
Dk Biteko ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 12, 2023; akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, katika kongamano la pili la kitaifa la wiki ya ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.
"Tujifanyie tathmini ili tusije kesho kugeuka watu wa kuduwaa hili limetokeaje, lakini pia mtu asiyejifanyia ufuatiliaji atakuwa mtu wa hasara wakati wote, niwahakikisheni kazi ya kujifuatilia wenyewe inatufanya tubaini matatizo mapema kabla hayajaleta hasara na hivyo kuyarekebisha.
Kwa upande mwingine, Dk Biteko amesema: “Maandalizi ya mfumo jumuishi yaende sambamba na mkakati wa matumizi ya Tehama ili taasisi zote za Serikali ziwe na uelewa wa pamoja kuhusu dhima na tija ya mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini.”
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk Jim Yonazi, amesema lengo la kongamano hilo lililoandaliwa na ofisi hiyo ni kuimarisha utamaduni wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mipango, program na miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini.
Amesema mikakati ya serikali katika kuimarisha ufuatiliaji na tathmini imelenga kupima utendaji kazi kuhakikisha mipango mbalimbali ya dira ya Taifa ya Maendeleo, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na program mbalimbali.