Dk Biteko aipigia debe sekta ya nishati China

Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amefanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen na kugusia miradi mbalimbali ya sekta ya nishati huku akiwaalika wawekezaji kutoka taifa hilo kuja kuwekeza nchini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amefanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian huku akigusia miradi mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo ile ya kwenye sekta ya nishati.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa Novemba, 24, 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Ubalozi wa China nchini, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Katika mazungumzo yao, Dk Biteko amemweleza Balozi Mingjian kuwa kwenye Sekta ya Nishati na Madini ina wawekezaji na wakandarasi wengi kutoka China.
“Sisi Tanzania tunaufurahia na kuuthamini uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yetu Tanzania na China na hapa kuna kampuni nyingi kutoka China zinazofanya kazi kwenye uchimbaji madini ikiwemo madini ya viwandani na uchenjuaji madini,” amesema
“Miradi ya nishati kuna kampuni za kichina zinafanya kazi, mfano kampuni ya TBEA inayojenga laini ya umeme ya KV 400; kutoka Chalinze hadi Dodoma na mradi wa kusafirisha umeme wa KV 400 kutoka Tanzania kwenda Zambia,” amesema
Dk Biteko ametumia fursa ya mzungumzo hayo kutoa wito kwa Serikali ya China kuiwezesha kifedha kampuni inayotekeleza mradi wa usafirishaji umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma na mradi wa TAZA, ili itekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati kutokana na umuhimu wake.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesema Tanzania bado ina uhitaji wa umeme utakaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo maji hivyo amekaribisha kampuni kutoka China kuja kuwekeza kwenye eneo hilo.
Dk Biteko amemweleza pia Balozi, Mingjian kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kuwa Uganda na Tanzania zinauthamini mradi huo na zinaendelea na utekelezaji wake unaosimamiwa na kampuni kutoka China ya CNOOC ikiwa kama moja ya wabia.
Kwa upande wake, Balozi Chen Mingjian ameeleza jinsi China inavyouthamini ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania huku akisema ni kielelezo cha uwepo wa ushirikiano huo mzuri, ni ujio wa Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping, nchini Tanzania mwaka 2013.
Kuhusu suala la kampuni za China kuja kuwekeza Tanzania kwenye miradi ya nishati amesema, atazikaribisha kampuni hizo huku akitolea mfano kampuni ya Synohydro ambayo inafanya vizuri katika ujenzi wa miradi ya uzalishaji umeme wa maji.