Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biteko: Polisi tendeni haki, msibambikie watu kesi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akikagua gwaride katika sherehe ya mahafali ya Maofisa na Wakaguzi waliohitimu mafunzo katika chuo cha Polisi jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Polisi wametakiwa kutenda haki, kusimamia weledi na nidhamu wanapokuwa kwenye kazi ya kuwatumikia wananchi.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutenda haki, kutobambikia watu kesi na badala yake wahusike katika kutatua shida na matatizo yanayowakabili Watanzania.

Ameyasema hayo katika mahafali ya kufunga kozi ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi namba 1 2022/23 yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam.

Kauli ya kutenda haki na kutobambikia watu kesi imekuwa ikizungumzwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa kwenye hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Septemba 4, 2023.

"Najua mkitoka hapa na kuanza majukumu yenu, wako watu watakaowalaumu na wengine wataonyesha kutoridhishwa na utendaji wenu, msivunjike moyo; mara nyingi watu wa aina hiyo huwa ni wahalifu...kuweni karibu na watu wema,” amesema.

Aidha, Dk Biteko amewaambia wahitimu hao kuwa wanatakiwa kutoa huduma Watanzania kwani wanahitaji jeshi lililoimara ambalo kwalo watajivunia kwa kuwa linawawezesha wananchi kuishi kwa salama likiwanda wao na mali zao.

Amewataka Polisi kutafakari kwa kina wimbo wao kama wanavyotafakari nyimbo za dini kwa kuwa umebeba kile wanachotakakiwa kukifanya wanapokuwa kazini.

Waziri Biteko amesema kuwa Serikali imetenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kumalizia majengo ya chuo hicho na kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuangalia namna ya upatikanaji wa fedha hizo.

Awali, Waziri Masauni alisema kuwa askari hao watakwenda kuzuia uhalifu katika ngazi ya kata pia wengine watatumika kuzuia uhalifu kwenye mitandao na kwamba kwa sasa wamepunguza uhalifu kwa kiasi ikiwepo uhalifu wa kutumia pikipiki.

"Tumekuwa na miradi ya kufunga mifumo ya kisasa ya kubaini uhalifu kwa miji mikubwa nchini ikiwepo Dar es Salaam na Dodoma," amesema Masauni.

Pia amesema ili kukabiliana na uhalifu watanunua magari kwa ajili ya kufuatilia usalama wa miji yote nchi ambapo zimetengwa Sh72 milioni za ununuzi wa pikipiki kwa ajili ya Polisi hadi ngazi ya kata.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameomba kuongezewa kwa askari katika mkoa huo kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliopo.

"Endapo mtaongeza ajira kipaumbele kiwe mkoa huu kutokana na hali halisi, pia mkoa huu una uhalifu wa kila aina licha ya uchache wa askari waliopo wameweza kudhibiti kwa kuweka ulinzi," amesema Chalamila.

Mkuu wa Polisi Tanzania (IGP), Camillius Wambura amewataka polisi waliohitimu mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi, kutekeleza waliyofundishwa kipindi chote cha mafunzo.

"Kwa sasa tumeongeza wakaguzi katika 234 katika ngazi ya kata na shehia kwa kuimarisha polisi jamii ambao wanashirikiana na wananchi katika maeneo husika, pia tumetengeza mfumo kidigitali ikiwemo ile ya haki jinai na kutoa mafunzo,” amesema Wambura.

Awali, Mkuu wa chuo hicho, Dk Lazaro Mambosasa, amesema kwa mara ya kwanza chuo hicho kimeweka historia ya kuwa na wanafunzi wengi wanaomaliza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961, ambapo idadi yao imefikia wanafunzi 952.

Alisema idadi hiyo inatwenda kupungua pengo la ukosefu wa usimamizi wa polisi ambapo watasaidia kutoa huduma hadi ngazi ya kata.

Wahitimu wa kozi ya maofisa walikuwa 696 wanawake wakiwa  124 na wanaume wakiwa 572 na wakaguzi wasaidizi walikuwa 256 wanawake wakiwa 47 na wanaume 216.

Pia amesema chuo kinahitaji Sh1 bilioni kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa miundombinu ya chuo ili kusaidia wanafunzi kuishi katika mazingira mazuri kwa kujifunzia.

Alisema kumekuwa na ongezeko la wakufunzi 18 wanaosoma nje ya nchi ambapo anaamini baada ya mafunzo yao wataleta kile walichojifunza kwenye nchi walizokwenda kwenye taaluma husika.