Biteko apiga marufuku kununua vifaa vya umeme nje ya nchi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko (watatu kulia) akiongea na wananchi wa kijiji cha Nachenjele kata ya Mbawala Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko ameonya manunuzi ya vifaa vya umeme nje ya nchi ambavyo vimekuwa vinafifisha viwanda vya ndani vinavyotengeneza bidhaa hiyo, huku akiagiza makarandarasi REA kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Mtwara. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko ameonya manunuzi ya vifaa vya umeme nje ya nchi ambavyo vimekuwa vinafifiisha viwanda vya ndani vinavyotengeneza bidhaa hiyo huku akiagiza makarandarasi wa Wakala wa Umeme Vijiji (Rea) kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini huku akipiga marufuku ununuzi wa vifaa vya umeme nje ya nchi.
Akizungumza leo katika vijiji vya Nachenjele pamoja na Pachota vilivyopo katika Wilaya ya Mtwara, Naibu Waziri Mkuu amesema miradi ya maendeleo inapaswa kukamilika kwa wakati na kuwataka Rea kutocheza na makandarasi.
Amesema kuwa makandarasi waliopewa kazi hiyo wanaenda vizuri jambo la muhimu ni kuhakikisha kuwa wanaongeza kasi ya kuunganisha umeme vijijini.
“Niwaambieni Rea msicheze na mtu mkicheza nao hawa watu hawatatuelewa wasipotuelewa hawa ndio wenye serikali yao sisi ni watumishi wao lazima tufikie kwenye mahitaji yao” amesema Biteko.
“Ndio maana sitaki kusikia mchezo wa kununua vifaa nje ya nchi wakati tuna viwanda hapa hapa nchini tabia ya kununua nayo ni zilipendwa eti jamani tuna kiwanda cha waya hapa nchini alafu unaenda kununua huko nchi fualani huko unataka nini,” amesema.
“Hivi viwanda tukauze wapi hivi vifaa lazima bidhaa zinazopatikana ndani ya nchi zinunuliwe hapa na zile ambazo hazipatikani ndani zinaweza kununua nje ya nchi kwanza tutakuza viwanda vyetu na kuvipa thamani na ajira kwa watoto wetu,” amesema Biteko.
“Makandarasi heshima yetu iko mikononi mwenu tumekubaliana na watu wa rea tutafanya tathmini ya kila mkandarasi kama haufanyi vizuri tutasitisha mkataba tutafute mtu mwingine. Mkandarasi mwenye nguvu ni yule ambaye asubiri mpaka alipwe ndio afanye kazi we si una hela, fanya kazi tutakulipa tumelipa mabilioni ya fedha sitaki kusikia kisingizio kuwa sijalipwa wewe huna uwezo acha watu wengine wafanye kazi,” amesema.
“Sisi tutakulipa kwa wakati ambao hautachelewa kupata fedha yako nitarudi hapa baada ya miezi mitatu kama siyo mimi atakuja naibu wangu kuangalia miradi hiii inavyoendelea,” amesema Biteko.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rea, Jones Olotu amesema kuwa zaidi ya vijjiji 401 vimeshaingia kwenye mpango ambapo vijiji 193 tayari na vijiji 208 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa laini na vimeshafikiwa na makandarasi.
Amesema kuwa zaidi ya Sh170 bilioni zimetengwa kwa Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya miradi mitano na pia kabla ya mwezi wa Juni, tutakuwa tumekamilisha mkoa mzima kuweka umeme.
“Pia tunao mradi maalumu kwa ajili ya kupelekea kwenye miradi ya maji vituo vya afya na taasisi pamoja na kueleka kwenye kilimo na migodi midogo pamoja na maeneo ambayo yapo kati ya mji na vijijini ambapo tulifanya tathmini na kubaini kuwa hayana tofauti na vijijini za ambapo miradi mitano imetekelezwa,” amesema.
Diwani wa Kata ya Naliendele, Masoud Dali amesema kuwa changamoto kubwa ni uhaba wa nguzo katika kata hiyo, hivyo kuomba serikali iweze kuwaongezea nguzo na kukamilisha kazi ya kusambaza umeme.
“Tunashukuru tumepata umeme lakini changamoto zipo tunaomba baadhi ya maeneo nguzo hazijatosha tunaomba ziongezwe ili kuweza kuwasaidia wananchi wa kijiji hiki,” amesema Dali.
Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa makandarasi wanafanya kazi nzuri ambapo kasi yao ni ndogo hivyo wakiongeza wanaweza kufanikiwa.
“Kikubwa makandarasi waongeze kasi kubwa bado tuna vijiji ambavyo bado muda ni mfupi wakandarasi wanapaswa kusikia kauli ya serikali wannchi hawataki maneno wanataka kuona umeme ukiwa unawake yaani ukisema mwezi wa tatu basi huduma inapatikana tunaomba mkamilishe kazi yenu,” amesema Chikota.