Dk Biteko awang’oa vigogo TPDC, Tanesco

Muktasari:
- Dk Biteko amechukua hatua hiyo baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wa Kata ya Msimbati mkoani Mtwara kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji gesi asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho.
Mtwara. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza kuondolewa kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana kwa kukutoa taarifa na kutofanya mikutano na wananchi wanaozunguka miradi ya gesi asilia.
Dk Biteko ametoa maagizo hayo leo Novemba 14, 2023 wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati mkoani hapa ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.
Akiwa kijijini hapo, wananchi wa Kata ya Msimbati walimweleza Dk Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji gesi asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba la gesi asilia.
“Changamoto kwenye miradi hii zinatokea lakini lazima awepo mtu ambaye ni daraja kati ya Serikali na Wananchi na mtu huyu analipwa mshahara kwa kazi hiyo, haiwezekani Waziri au Rais kuja kutoa taarifa kwa wananchi wakati kuna mtu kaajiriwa kwa kazi husika, wananchi hawa wanapaswa kupata taarifa,” amesisitiza Biteko.
Katika hatua nyingine, ameagiza Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na majibu yasiyo stahiki wanayojibiwa wananchi wanapopiga simu kwenye Shirika hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Vilevile, Dk Biteko ameagiza kuwa, miradi inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule, vituo vya afya, barabara na Maji.
"Changamoto zote mlizozieleza hapa nataka niwahakikishie kuwa zitashughulikiwa, nataka muone tofauti kuanzia sasa, kama gesi asilia inatoka hapa na inaendesha mitambo ya umeme kwa asilimia 65.
“Haiwezekani wala haiingii akilini, watu hawa wakalia kituo cha afya, Polisi, ubovu wa barabara, haiwezekani, nataka niwaeleze kwamba ushuru wa huduma unaokusanywa na halmashauri sehemu ya fedha lazima irudi hapa," amesema Dk Biteko.
Dk Biteko, amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja Mkuu wa Wilaya kukaa pamoja na wananchi wa eneo hilo ili mpango wa maendeleo wa kijiji hicho uandaliwe, hivyo fedha zinapotolewa zifanye maendeleo kulingana na mpango wa kijiji.
Aidha, ameiagiza TPDC kuweka mpango maalum wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Jamii (CSR) katika eneo hilo ili wananchi hao waone faida ya kuwepo kwa miradi kwenye maeneo yao na kuwaelekeza kuwaagiza wajenge kituo cha afya, taa za barabarani na Kituo cha Polisi.