Diwani wa CCM wilayani Wanging'ombe afariki dunia

Muktasari:
- Diwani wa Kata ya Luduga iliyopo wilayani Wanging'ombe, Hassan Ngella amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya rufaa mkoani mbeya baada ya kuugua ghafla.
Njombe. Diwani wa Kata ya Luduga iliyopo wilayani Wanging'ombe, Hassan Ngella amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya rufaa mkoani mbeya baada ya kuugua ghafla.
Hayo yamethibitishwa leo na katibu wa siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Wanging'ombe, Ruben Nyagawa alipozungumza na gazeti la Mwananchi.
Amesema taarifa ya kifo cha diwani huyo ameipata usiku wa kuamkia leo akisema diwani huyo aliugua na kukimbizwa hospitali ya Ilembula iliyopo wilayani Wanging'ombe.
Amesema baadaye alihamishiwa katika hospitali ya rufaa iliyopo mkoani Mbeya ambapo aliendelea na matibabu licha ya jitihada zote za madaktari usiku wa kuamkia leo alifariki dunia.
Amesema taratibu za kichama zinaendelea ili kuona kwamba namna ambavyo chama hicho kitashiriki mazishi ya diwani huyo.
"Kwa mujibu wa ratiba na taratibu chama na wanandugu mazishi yanatarajiwa kufanyika hapo kesho," amesema Nyagawa.
Amesema tukio la kufa sio zuri sana katika maisha ya binadamu lakini diwani huyo ameacha pengo wilayani humo kwani huwezi kuzungumzia chama hicho wilayani Wanging'ombe bila ya kumtaja diwani huyo.
Amesema chama hicho kimepoteza mtu mahiti, mchapakazi na mwaminifu kwakuwa alikuwa akikipenda chama hicho na kufikia kutumia gharama zake binafsi kwa ajili ya chama.
Amewapa pole wananchi wa kata ya Luduga kwa kuondokewa na diwani wao ambaye alikuwa anawapenda wananchi wake kwa kutoa muda wake mwingi ili kuwatumikia.
"Nafahamu ameitumikia kata ya Luduga kwa miaka mingi ingawa kuna muda aliondoka na baadaye alirudi na mwaka jana aliweza kushindana udiwani wake," amesema Nyagawa.
Amewaomba wananchi wa kata hiyo kushiriki maandalizi ya mazishi ya diwani huyo huku wakichukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona.