Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Digitali ilivyokuza biashara nchini

Muktasari:

  • “Ninahitaji kuwa na simu yenye chaji na kuhakikisha nina kifurushi cha kutosha ili biashara zangu ziende vizuri. Napokea oda na kutuma mzigo kwa wateja nikiwa nyumbani, sio lazima nitoke kila asubuhi,” anasema Ali Maulid, muuzaji wa vifaa vya kielektroniki kwa njia ya mtandao.


“Ninahitaji kuwa na simu yenye chaji na kuhakikisha nina kifurushi cha kutosha ili biashara zangu ziende vizuri. Napokea oda na kutuma mzigo kwa wateja nikiwa nyumbani, sio lazima nitoke kila asubuhi,” anasema Ali Maulid, muuzaji wa vifaa vya kielektroniki kwa njia ya mtandao.

Maulid anasema ni gharama kubwa kumiliki duka jijini Dar es Salaam hivyo anayo stoo ya kuhifadhia bidhaa zake nyumbani na hutumia mitandao ya kijamii hususan Instagramu, Whatsapp, Facebook na Telegram kutangaza anachouza.

“Nikishaweka insta (instagram) naongeza bei na mawasilino yangu, mtu akipenda ananipigia simu na tukiafikiana gharama za usafiri nampelekea, akipokea analipia,” anasema Maulid.

Ili kutanua wigo wa biashara, anasema amesajili laini za uwakala hivyo wateja wasioweza kutuma na ya kutolea huwaambia watoa fedha kwenye namba zake za uwakala ambazo mwisho wa siku hupata kamisheni kama mawakala wengine.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom, Roselyn Mworia anasema fursa za digitali kwa wafanyabiashara wa ndani na nje zinatoa jukwaa la kuonyesha bidhaa, kutangaza, kuuza, kununua na kulipia kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.

“Dijitali imeziwezesha biashara nyingi kwa kiasi kikubwa, zipo mpya zilizoibuka lakini pia zilizokuwepo zimeboreshwa na mipinduzi ya kidijitali na sasa zina namna mpya ya kuzifanya,” anasema Roselyn.

Anasema dijitali imekuja kitoa suluhu na urahisi wa kufanya mambo mengi katika biashara kwani kwani mbali na kutoa suluhu la kuuza na kununua kwani mfanyabiashara anaweza kulipa kodi na tozo za Serikali kwa urahisi na Serikali nayo ikikusanya mapato yake bila usumbufu.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo anasema mambo yote hayo yanawezeshwa na uwezo wa kuunganishwa kwenye mtadao kwani shughuli nyingi za kidijitali ukiachilia mbali vifaa vyenyewe, zinahitaji intaneti.

Anasema mapinduzi ya dijitali katika simu yametoa ajira nyingi kwa watu akitolea mfano huduma za fedha kwa njia ya simu ambazo zimetoa ajira kwa zaidi ya watu 75,000 wanaoingiza kipata kwa kufanya uwakala.

Kwa sehemu kubwa mapinduzi ya teknolojia ya dijitali nchini, yanachagizwa na kuimarishwa kwa huduma za simu na ubunifu unaorahisisha mtu kuwasiliana muda wowote.

Simu muhimu zaidi

Tekinolojia ya simu ya kiganjani ilitambulishwa mwishoni mwa karne ya 20 (1973), kampuni ya kwanza kuzindua simu ya mkononi ikiwa Motorola kutokana na ugunduzi John Mitchell, mhandisi wa umeme aliyeshirikiana na mtaalamu wa mawasiliano, Martin Cooper.

Mpaka mwaka 2000, simu za mkononi hazikuwa maarufu na muhimu kama ilivyo sasa kwani waliozimiliki walikuwa wachache lakini sasa, imekuwa lazima kuwa nayo ili kufanikisha mawasiliano ya aina tofauti.

Katika karne ya 21 hususan miaka 10 hadi 15 iliyopita, umuhimu wa simu umejidhihirisha maeneo tofauti na zimeongeza tija kwa kiasi kikubwa.

Kwa sasa mtumiaji wa simu anaweza kupata huduma tofauti na kufanikisha miamala ya fedha bila kuhitajika kwenda benki, kutizama luninga, na kupata habari au kununua bidhaa ilmradi simu yake ina intaneti.

Simu hizi kwa sasa ni nyenzo muhimu ya kumkutanisha mfanyabiashara na mteja kutokana na programu rafiki zilizopo kama inavyoshuhudiwa kwenye usafiri hasa teksi, nyumba za wageni bidhaa nyingine zinazouzwa mtandaoni mfano Amazon achana na maelfu ya wajasiriamali wadogo wanaotumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kujitangaza.

Miongoni mwa mambo yaliyorahisishwa ni ukataji tiketi, kuita taxi, kujua viwango vya kubadilishia fedha za kigeni, kufanya malipo, kuweka akiba au kulipa kodi za Serikali.

Wakati wa mlipuko wa janga la Uviko-19, teknolojia ya kidijitali ilichukua sura mpya na kutoa fursa zaidi katika ufanyaji biashara na mambo mengine ikiwamo mikutano bila kukutana, kufanyia kazi nyumbani huku biashara ya mtandaoni ikishamiri zaidi.

Katika Hotuba yake ya kwanza bungeni iliyoitoa Aprili 22 mwaka jana, Rais Samia Suluhu alisema Serikali itawekeza zaidi katika miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kuongeza kasi ya kuufikisha mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi nchini.

“Kama inavyofahamika, dunia ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda yanaongozwa na sekta ya Tehama, kwa maana hiyo, uchumi wa dunia na shughuli nyingi duniani kwa sasa zinafanyika kwa kutumia Tehama,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema mbali na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini, Serikali itaongeza kasi (broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 mwaka 2025.

“Tutaongeza watumiaji wa intaneti kutoka asilimia 43 ya sasa hadi asimilia 80 mwaka 2025 na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima,” alisema Rais Samia na kusisitiza kuwa kipaumbele kitakuwa ni utafiti, ubunifu na kuimarisha usalama katika mawasiliano.

Ripoti ya ukuaji wa sekta ya dijitali Tanzania (Digital Transformation in Tanzania) iliyotolewa Machi 2019 inaeleza namna huduma za simu zinavyochangia kukuza uchumi nchini na kufanikisha mpango wa Serikali wa kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo inaeleza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya simu kufanikisha mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Kiongozi wa utafiti wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na Shirikisho la Kampuni za Mawasiliano Duniani (GSMA), Kenechi Okeleke anasema sekta hiyo itaendelea kukua kwa miaka mitano ijayo na ukwekezaji wake kufika Sh6 trilioni.

“Kuna vikwazo vya miundombinu isiyojitosheleza na ujuzi lakini kwa kutumia teknolojia ya dijitali mpango wa Serikali mpaka mwaka 2025 kufikisha mawasiliano vijijini unaweza kufanikiwa kwa urahisi kuliko kawaida,” anasema Okeleke.

Ripoti hiyo inapendekeza kwamba, kama Serikali itaweka sera za kuvutia uwekezaji, uboreshaji wa miundombinu vijijini na kuyafanyia kazi malalamiko ya kodi, yataifanya sekta hiyo kukua zaidi na kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

“Sera thabiti na zinazotabirika zitasaidia kuwapa imani wawekezaji wenye nia katika sekta hiyo, wasimamizi wa sekta hii wanapaswa kuwa na mpango rafiki,” anasema.

Ripoti hiyo inapendekeza kuboreshwa kwa miondombinu maeneo yote nchini na uuzaji wa simu za kisasa kwa bei rahisi.