Dereva wa lori lililoua saba Morogoro atiwa mbaroni

Watu wakiangalia ajali iliyohusisha LORI la mizigo na gari ndogo aina ya Noah eneo la Dakawa, wilayani Mvomero. Picha na Johnson James
Muktasari:
- Ajali hiyo ilihusisha lori hilo lililokuwa linatokea Morogoro kwenda Dodona na gari aina ya Toyota Noah iliyokuwa inatokea Dumila kuelekea Morogoro mjini.
Morogoro. Dereva wa lori lililosababisha ajali iliyoua watu saba na kujeruhi wengine sita jana mkoani Morogoro amekamatwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 15, 2024, Mkama amesema Polisi wamemkamata dereva akiwa wilayani Mvomero alikokimbilia kwa lengo la kujificha.
Ajali hiyo ilihusisha lori hilo lililokuwa linatokea Morogoro kwenda Dodona lililogongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Noah iliyokuwa inatokea Dumila kuelekea Morogoro mjini.
Kamanda Mkama amesema wanaendelea kumhoji dereva huyo na uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yake.
"Baada ya ajali kutokea jana, huyu dereva alikimbia kusikojulikana akalitelekeza gari kake, lakini kwa jitihada za askari wetu tumefanikiwa kumkamata na yuko kwenye mikono ya Polisi. Kinachofanyika sasa tunaendelea na mahojiano sambamba na uchunguzi na vyote vikikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,” amesema kamanda huyo.
Wakati huohuo, miili saba ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo imetambuliwa na ndugu na baadhi imeshachukuliwa kwa taratibu za maziko.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero, Francis Paul amesema miili hiyo ilianza kutambuliwa jana na leo mitano imechukuliwa na ndugu.
“Maiti tano zimeshachukuliwa na mbili zimetambuliwa na ndugu zao lakini bado ziko chumba cha kuhifadhia maiti, familia zinaandaa utaratibu wa kuja kuzichukua,” amesema Dk Paul.
Kuhusu hali za majeruhi, Dk Paul amesema watano wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kuimarika na mmoja aliyepelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoani Morogoro anaendelea na matibabu.
Amesema majeruhi huyo alikuwa na mumewe na mtoto kwenye ajali hiyo, mume pia alijeruhiwa lakini alitibiwa na kuruhusiwa jana na mtoto ambaye ana umri wa miezi minne hakupata madhara yoyote.