Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dengue yatikisa Dar, Pwani, Wizara ya Afya yatoa tahadhari

Muktasari:

  • Mbali na dengue, Wizara ya Afya imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayoongezeka wakati wa baridi na kipupwe, ikiwamo influenza, nimonia na mafua ya kawaida

Dar es Salaam. Homa ya dengue imeendelea kuongezeka nchini, huku wagonjwa 360 wakiripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kati ya Januari na Juni mwaka huu, ikilinganishwa na 229 walioripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Mwenendo wa ugonjwa umeonesha ongezeko la kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni 24, 2026.

Imeelezwa kuwa, mabadiliko ya tabianchi yameongeza kasi ya kuenea kwa makundi makuu mawili ya magonjwa, yakiwamo yanayoenezwa na wadudu, maji au chakula.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Juni 25, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dk Otilia Gowelle amesema ongezeko hilo linahusishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto, unyevunyevu na vipindi vya mvua vinavyounda mazingira rafiki kwa mbu aina ya Aedes wanaoeneza virusi vya dengue.

"Kwa kipindi cha kuanzia Januari mosi hadi 24 Juni 2026 jumla ya wagonjwa 360 wametolewa taarifa kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ukilinganisha na jumla  ya wahisiwa 229 vilivyoripotiwa kwa muda huo mwaka 2025," amesema.

Dk Gowele amesema mwenendo wa homa ya dengue uomeonekana kuendana na misimu ya mvua za vuli na masika vikiambana na vipindi vya joto na kuongezeka kwa unyenvu  zimesababisha kuongezeka kwa mbu aina ya Aedes. 

Amesema maeneo ya mijini katika ukanda wa pwani kama vile Dar es Salaam, Tanga, na Pwani yamekuwa hatarini zaidi juu ya uwepo wa ugonjwa wa dengue.

Amesema maeneo ya mijini na ukanda wa Pwani yameendelea kuwa hatarini zaidi kutokana na mchanganyiko wa mvua na joto unaochochea mazalia ya mbu hao.

“Mwenendo wa homa ya dengue umeonekana kuendana na misimu ya mvua za vuli na masika, hasa zinapoambatana na vipindi vya joto na unyevunyevu mkubwa. Hali hii imeongeza mazalia ya mbu wa aina ya Aedes na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi,” amesema Dk Gowelle.

Mbali na dengue, Wizara ya Afya imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayoongezeka wakati wa baridi na kipupwe, ikiwamo influenza, nimonia na mafua ya kawaida.

Dk Gowelle amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanayohusisha vipindi vya baridi, mvua na unyevunyevu huongeza mazingira yanayochochea kuenea kwa magonjwa hayo, hususan kwa watoto, wazee na watu wenye kinga dhaifu.

Amesema wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu hatua za kujikinga, ikiwamo kuvaa nguo za kujikinga na baridi, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara, pamoja na kutumia vitakasa mikono katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

“Watu wenye mafua wanapaswa kuzingatia usafi wa mikono na kuepuka kuwaambukiza wengine. Magonjwa mengi ya mfumo wa upumuaji husababishwa na virusi na yanaweza kuzuilika kwa kuzingatia kanuni za afya,” amesema.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakichochea pia magonjwa yanayoenezwa na wadudu na yale yanayoenezwa kupitia maji au chakula.

Kwa upande wa malaria, Dk Gowelle amesema ongezeko la joto limefanya baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kama Njombe, Kagera, Arusha na Kilimanjaro kuwa rafiki zaidi kwa mbu wanaoeneza ugonjwa huo.

Hata hivyo, amesema jitihada za Serikali na wadau wa maendeleo zimewezesha kupungua kwa maambukizi ya malaria nchini kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7.

“Mafanikio haya yametokana na uwekezaji mkubwa katika elimu kwa umma, matumizi ya viuatilifu, usambazaji wa vyandarua vyenye dawa na udhibiti wa mazalia ya mbu,” amesema.

Akizungumzia magonjwa yanayoenezwa kwa maji, amesema Tanzania ilikumbwa na mlipuko mkubwa wa kipindupindu kati ya mwaka 2024 na Februari 2026 kulikuwa na wagonjwa 16,600 na vifo 207 viliripotiwa nchini.

Dk Gowelle amesema mikoa iliyoathirika zaidi ilikuwa Rukwa, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Katavi na Songwe.

“Lakini tangu Februari mwaka huu hatuna mgonjwa hata mmoja wa kipindupindu. Mafanikio haya yametokana na kampeni za elimu ya afya, upatikanaji wa maji safi na usimamizi wa mazingira,” amesema.

Amesema wizara imeimarisha mifumo ya kidigitali ya ufuatiliaji wa magonjwa kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa, hatua inayowezesha taarifa za dalili za milipuko kufika kwa wataalamu ndani ya saa 24.

Pia, amewataka wananchi kutumia namba ya dharura 199 kutoa taarifa za magonjwa yanayoshukiwa kuwa ya mlipuko ili hatua za haraka zichukuliwe.

Wakati huo huo, amezitaka sekta mbalimbali ikiwamo miundombinu, maji na Serikali za mitaa kujiandaa mapema kuelekea msimu ujao wa mvua kwa kusafisha mitaro, kuboresha mifumo ya maji taka na kuhakikisha barabara zinapitika ili kupunguza hatari za milipuko ya magonjwa.

“Udhibiti wa magonjwa yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi si jukumu la sekta ya afya pekee. Unahitaji ushirikiano wa sekta zote pamoja na wananchi,” amesema Dk Gowele.