Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DCEA, Veta waungana kuwajenga upya waraibu wa dawa za kulevya

Kamishna Jenerali wa Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Antony Kasore wakisaini mkataba wa makubaliano yatakayowezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kupata mafunzo ya ufundi stadi.

Muktasari:

  • Hatua hiyo inalenga kuwasaidia kujenga maisha mapya na kupunguza hatari ya kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.

Dar es Salaam. Katika hatua inayolenga kuunganisha tiba ya uraibu na uwezeshaji wa kiuchumi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) zimeingia makubaliano yatakayowawezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kupata mafunzo ya ufundi stadi na kujijenga upya kimaisha.

Taarifa iliyotolewa na DCEA leo Juni 4, 2026 imeeleza kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha waraibu waliopona hawarejei tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kukosa ajira, ujuzi na mitaji ya kujikimu.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema matumizi ya dawa za kulevya bado ni tishio kubwa kwa maendeleo ya taifa kutokana na athari zake za kiafya, kijamii na kiuchumi.

Amesema dawa za kulevya zimekuwa zikichangia ongezeko la uhalifu, migogoro ya kifamilia, kuporomoka kwa maadili na kupungua kwa nguvu kazi ya taifa.

“Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya, kutoa elimu kwa jamii na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu,” amesema.

Hata hivyo, Lyimo amesema uzoefu umeonyesha kuwa matibabu pekee hayatoshi iwapo hakuna mfumo wa kumjenga mhusika kiuchumi baada ya kupona.

“Watu wengi wanaopona uraibu hukumbana na changamoto za ajira, kipato na wakati mwingine unyanyapaa wa jamii. Hali hii inaweza kusababisha kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya kama hawatapewa shughuli mbadala,” amesema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, waraibu waliopata nafuu watapata nafasi ya kujiunga na vyuo vya Veta nchini kwa gharama nafuu ili kujifunza fani mbalimbali ikiwemo useremala, umeme, ushonaji, ufundi magari, teknolojia ya habari na upishi.

Baada ya mafunzo, wahitimu hao wataunganishwa na fursa za mitaji kupitia taasisi za fedha na pia kupewa vifaa vya kuanzia kazi kulingana na ujuzi walioupata.

Lyimo amesema DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi za fedha ili kuhakikisha wahitimu wanapata mikopo midogo midogo ya kuanzisha biashara.

“Mpango huu unalenga kuwajengea uwezo waraibu waliopona ili wawe sehemu ya maendeleo badala ya kubaki tegemezi. Mtu mwenye ujuzi na kipato halali ana nafasi kubwa ya kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa kituo kikubwa cha urejeshaji wa waraibu jijini Dodoma kitakachoshirikiana na Veta katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi.

“Waraibu watakaopata nafuu kupitia hospitali, kliniki maalumu na nyumba za usaidizi watapimwa kabla ya kuingizwa kwenye programu za mafunzo ili kuhakikisha wako tayari kisaikolojia na kiafya kujifunza,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema taasisi hiyo imepokea ushirikiano huo kama sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata ujuzi bila kujali historia zao.

Amesema Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi stadi katika wilaya mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa mafunzo nchini.

“Lengo letu ni kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi inayokidhi mahitaji ya soko la ajira. Kupitia makubaliano haya tutawapokea waraibu waliopata nafuu na kuwapatia stadi zitakazowasaidia kujenga maisha yao upya,” amesema Kasore.

Kasore amesisitiza kuwa jamii ina jukumu muhimu katika kusaidia vijana waliopitia uraibu, akisema unyanyapaa unaweza kudhoofisha mafanikio ya mpango huo.

“Tunawahamasisha vijana kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi. Ujuzi ni msingi wa ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.


Wasemavyo wadau

Wadau wa afya ya jamii na elimu wameeleza kuwa mpango huo unaweza kuwa mkombozi muhimu iwapo utatekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumza na Mwananchi, mchambuzi wa masuala ya afya ya jamii, Leticia Ngayoma, amesema mpango huo ni muhimu lakini changamoto kubwa imekuwa si kuokoa waraibu pekee bali kuwajengea mfumo wa maisha endelevu baada ya matibabu.

Amesema mara nyingi programu za urejeshaji hukwama katika hatua ya ufuatiliaji na uwezeshaji wa kiuchumi, jambo linalofanya baadhi ya waliopona kurejea katika mazingira hatarishi.

“Mafanikio ya makubaliano haya yatapimwa si kwa idadi ya waliofuzu mafunzo pekee, bali kwa uwezo wa waliopata nafuu kuendelea kuishi maisha yenye tija bila kurejea kwenye uraibu.”

Mtaalamu wa elimu ya ufundi, Yohana Joseph amesema ushirikiano kati ya DCEA na Veta unaweza kuzaa matokeo chanya iwapo utaendana na tathmini ya mahitaji ya kila mhitimu ili kuhakikisha mafunzo yanalingana na uwezo na hali ya mwanafunzi.

Amesema hatua ya kurasimisha mafunzo na kutoa vyeti itasaidia wahitimu kutambulika rasmi sokoni na kupata fursa za ajira na mikopo, lakini wamehimiza pia kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa kijamii ili kuhakikisha wanadumu katika ajira na miradi yao.

Baadhi ya waliopitia uraibu wa dawa za kulevya wamesema changamoto kubwa baada ya kupona si tu kujijenga upya, bali kukabiliana na mtazamo wa jamii unaowazuia kupata fursa za kiuchumi.

Said Makukula, mkazi wa Temeke, aliyeacha kutumia dawa za kulevya zaidi ya miaka minne iliyopita, amesema maisha baada ya kupona yamekuwa ya mapambano mapya ya kukubalika kijamii.

“Nilipomaliza tiba nilifikiri nitapata kazi kirahisi kwa sababu nilikuwa nimebadilika. Lakini kila sehemu niliyoomba kazi, historia yangu ndiyo ilizungumzwa zaidi kuliko uwezo wangu wa sasa. Nikaishia kukosa nafasi zote. Sasa kama kuna hiyo fursa ya kupata ujuzi, naomba pia wanajamii wawe tayari kutupokea,” amesema.

Muathirika mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema unyanyapaa unaoendelea baada ya tiba unawafanya baadhi ya waliopona kujihisi hawana thamani katika jamii.

“Unapokubali kwamba ulikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya, jamii haisahau. Hata ukibadilika kiasi gani, watu wanakuona kama bado unaweza kurudi nyuma. Hii inavunja moyo sana. Mpango huu unaweza kuwa suluhisho muhimu iwapo utaenda sambamba na kampeni ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu waliopona uraibu,” amesema.