Prime
DCEA: Hatuyumbishwi na vitisho vita dhidi ya dawa za kulevya
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa Mwananchi
Muktasari:
- Asema vitisho havijawahi kuyumbisha dhamira ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Aeleza maofisa wamepewa mafunzo na wana uzalendo.
Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretus Lyimo, amesema jumbe za kutishiwa maisha kutoka kusikojulikana ni miongoni mwa mambo anayokumbana nayo katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, amesisitiza vitisho hivyo havijawahi kuyumbisha dhamira yake na mamlaka hiyo katika kudhibiti na kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini, akisema maofisa wake wana mafunzo na uzalendo wa kutosha kuhimili matishio, wakiwa na dhamira ya kumaliza biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Amekwenda mbali zaidi na kueleza rushwa ni eneo lingine hatari katika vita dhidi ya dawa za kulevya, akidokeza tayari DCEA imeshakubaliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushirikiana kulikabili hilo.
Lyimo ameeleza hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
Amesema wengi waliopambana na wahusika wa dawa za kulevya walilalamikia kufuatiliwa, kutishiwa kuuawa, na wengine walishasema wanaogopa.
“Kuna mmoja alisema ametafutwa na ndegenyuki (drone) imemfuata hadi nyumbani kwake, wanataka wamlipue. Akaomba awekewe ulinzi, lakini ukienda nchi za nje huko, jeshi kabisa limeundwa kupambana, lakini wanauawa,” amesema.
Amesema vitisho kutoka kwa wafanyabiashara hao wa dawa za kulevya vipo hata nchini, lakini mamlaka imejipanga na maofisa wake wana mafunzo na wamejitoa katika kuilinda nchi bila woga.
“Matishio yanakuja, watu wanatishia. Unaweza kutumiwa message (ujumbe mfupi wa maandishi) hapohapo, ukiitafuta ile simu kwenye mtandao haipo,” amesema.
Amesema baadhi ya jumbe za vitisho hutumwa kwa njia za simu zisizobainika, huku wahusika wakibadilisha laini na vifaa ili kuficha utambulisho wao.
“Anakutishia, anakwambia kwamba hili jambo usipoliacha, labda mwezi fulani haufiki, tutakuwa tumekuua. Au mtu anakwambia hakikisha kwamba hili jambo unaachana nalo,” amesema.
Hata hivyo, amesema vitisho hivyo havijawahi na havitawahi kuyumbisha utendaji wake na maofisa wake katika kukabiliana na dawa za kulevya nchini, akisisitiza wana uzalendo wa kutosha kuyakabili hayo.
“Sisi ni wazalendo,hata vijana wetu walioko hapa, ambao ni watumishi wa mamlaka, tuliwaambia hakuna kuogopa. Tumekubaliana kwamba tutafanya kazi bila woga. Tutahakikisha kwamba tunalilinda hili Taifa dhidi ya dawa za kulevya,” amesema.
Lyimo ameeleza anatambua mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaokoa roho za watu na Taifa, kwa sababu dawa hizo zinaathiri uchumi, afya, usalama, ustawi wa nchi na kila sekta ya binadamu.
Amesema iwapo mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayataimarika, utafika wakati Afrika au Tanzania haitakuwa na vijana, na hivyo nchi itakosa maendeleo.
Kwa sababu hiyo, amesema lazima wahakikishe wanapambana na dawa za kulevya ili kuokoa vijana wasiathiriwe, lakini rasilimali za nchi zilindwe.
“Taifa lolote bila vijana haliwezi kukua, maana vijana ndiyo wanaorithisha kuendeleza Taifa na ndiyo wanaoleta uchumi wa nchi, hivyo DCEA tumejipanga kupambana na dawa za kulevya, ndiyo maana tumeifanya kazi yote.
“Vigogo wa dawa za kulevya wako magerezani, lakini hakuna ofisa wetu hata mmoja aliyedhuriwa kwa namna yoyote kwa sababu tunaamini tuna mbinu mbalimbali za kuifanya hii kazi,” amesema kamishna huyo.
Usalama kwa watoa taarifa
Katika maelezo yake, Lyimo amesema woga ulikuwepo kwa Watanzania kutoa taarifa za dawa za kulevya, kutokana na historia ya baadhi yao kuwahi kuuawa na wafanyabiashara wa dawa hizo.
Ili kulidhibiti hilo, amesema kila anayetoa taarifa kwa sasa analindwa kuhakikisha hakuna anayemjua, na kama italazimika kuhamishwa kutoka katika eneo analoishi, mamlaka hiyo inafanya hivyo kwa gharama zake.
Kuimarishwa kwa ulinzi kwa watoa taarifa, amesema ndiko kulikosababisha mafanikio ya mamlaka hiyo kukamata kilo milioni 5.4 kwa miaka mitatu, kiwango ambacho hakikuwahi kufikiwa katika historia ya nchi.
Amesisitiza Serikali imeweka kipaumbele katika kuwalinda watoa taarifa kwa kuwa inafahamu kuwa wafanyabiashara hao, kuna wakati, wanatishia au kuhatarisha maisha ya raia.
“Ikiwezekana, tukiona kuna hatari, tunampangia hata awe anakaa hotelini, awe anakaa eneo nje ya lile ambalo ametoa zile taarifa kuhakikisha maisha yake yanaendelea kama kawaida bila kupata shida. Watanzania watoe taarifa,” amesema.
Rushwa katika dawa za kulevya
Lyimo amesema siri yoyote ya kumaliza tatizo la dawa za kulevya ni uzalendo, uaminifu na kukataa rushwa, na kwamba haiwezekani biashara hiyo ifanyike bila kuhusisha rushwa kubwa.
“Tanzania hilo tumelishinda kwa kuepuka rushwa, lakini kwa kuhakikisha uzalendo zaidi, kutokuwa na woga, ukishakuwa na woga, ukikimbiza mbawa zako eti kwamba nitadhuriwa, hutaweza kudhibiti,” amesema.
Amesisitiza kwa kawaida biashara ya dawa za kulevya huambatana na rushwa kubwa, ama katika uzalishaji wake au usafirishaji.
Katika hilo, amesema wapo watumishi wa Serikali waliofukuzwa kazi hadi sasa kwa kupokea rushwa na kuruhusu dawa za kulevya ziingie nchini.
“Wapo watumishi wa Serikali wamefukuzwa kazi na kuchukuliwa hatua kutokana na kuchukua rushwa na kuruhusu dawa za kulevya ziingie nchini,” amesema.
Kamishna huyo amesema haiwezekani katika eneo kuwe na shamba la dawa za kulevya bila kiongozi wa eneo hilo kujua, bila shaka anakuwa amechukua rushwa kuruhusu kilimo kifanyike.
“Huwezi kuniambia kwamba tani 10 au 20 zimeingia nchini, zimepita kwenye mipaka yetu, useme kwamba mtu hajaona tani 20, kuna rushwa inatumika pale,” amesema.
Ili kutatua changamoto hiyo, amesema wamesaini mkataba wa makubaliano na Takukuru, ili panapoonekana dalili za rushwa, taasisi hiyo itapewa jukumu la kufuatilia na kuchukua hatua.
“Kwa sababu sisi tunashughulika na dawa za kulevya, wao washughulike na rushwa, kwa kuwa biashara ya dawa za kulevya inaambatana kwa ukaribu na rushwa, kwa hiyo tumekubaliana,” amesema.
Amesema kila mamlaka ndani ya Serikali, kuanzia ya kijiji, mtaa, kata na vyombo vyote vya dola, vinatakiwa kudhibiti dawa za kulevya zisiingie nchini, na zinapoingia kuna mtu amekula rushwa, ameisaliti Serikali.
Kibano kwa watumishi wa Serikali
Hata hivyo, amesema hilo wanaendelea kulidhibiti, na tayari kuna watumishi wa Serikali waliokamatwa, wamefunguliwa kesi za uhujumu uchumi na wengine kuchukuliwa hatua za kufutwa kazi kwa tuhuma hizo.
“Tumewakamata watumishi wa Serikali, wengi wako gerezani na tumewafungulia kesi za uhujumu uchumi. Mtu anakwambia, kwa kuwa mimi nina gari lenye king’ora, nipe mzigo niupeleke, nitapiga king’ora polisi watanipisha njiani nitapita, tuliwakamata,” amesema.
Ameeleza wapo wanaoweka mifukoni wakidai hawakaguliwi, akisisitiza wote wanakaguliwa kwa sasa na wanakamatwa.
“Watumishi wenye nafasi zao wapo gerezani, tumewakamata na tunachukua hatua kubwa. Yeyote tutakayembaini, bila kujali cheo wala nafasi yake, tunamkamata na kumchukulia hatua,” amesema.
Katika mahojiano hayo, Lyimo amesema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumteua katika wadhifa huo akiwa na umri wa ujana, rika ambalo mara nyingi hutafsiriwa kuwa na tamaa, ni uthibitisho kuwa kiongozi huyo anawaamini vijana.
“Najitahidi kuhakikisha tunamdhihirishia mheshimiwa Rais kwamba vijana wanaweza, wapo vijana wengi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa uaminifu na kuifikisha nchi katika hatua ambayo haikuwahi kutarajiwa,” amesema.