Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Sweda: Walimu epukeni mikopo inayowadhalilisha

Muktasari:

  • Baadhi ya walimu mkoani Njombe huweka rehani vyeti vyao vya taaluma ili kuchukua mikopo ya kausha damu.

Njombe. Walimu mkoani Njombe wametakiwa kuthamini taaluma yao na kujiepusha na tabia ya kuiweka rehani kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kuchukua mikopo kandamizi, maarufu kausha damu.

Hili limeibuka baada ya kubainika kuna baadhi ya walimu hutoa vyeti vyao vya taaluma kama dhamana ya mikopo kutoka kwa watu binafsi au taasisi zisizo rasmi.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Aprili 23, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda wakati wa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Walimu (CWT) mkoani hapa.

Sweda amesema viongozi wa chama hicho wanalo jukumu la kuwasaidia walimu kuepukana na mikopo inayowadhalilisha hadi kufikia hatua ya kuweka rehani vyeti vya taaluma.

Amesema kuna walimu ambao walishindwa kuhudhuria uhakiki wa vyeti kwa kuwa, vilikuwa mikononi mwa wakopeshaji.

"Nilishuhudia mwalimu mmoja ambaye aliweka dhamana vyeti vyake vyote kwa mkopeshaji. Siku ya uhakiki akakosa vyeti kwa kuwa alikuwa anadaiwa kiasi kidogo cha fedha na mkopeshaji alikataa kutoa vyeti mpaka alipwe," ametoa ushuhuda mkuu huyo wa wilaya.

  • Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Njombe Shabani Ambindwile akizungumza na walimu mara baada ya kuchaguliwa kwa miaka mitano mingine kuwaongoza walimu mkoani Njombe.

Amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kutunza vyeti vyao kwa uangalifu kwa sababu ndiyo msingi wa maisha yao ya kazi, huku akiwashauri kujenga utamaduni wa kusaidiana badala ya kutegemea mikopo yenye masharti kandamizi.

Aidha, Sweda amewahakikishia walimu hao kuwa Serikali inaendelea kuboresha masilahi yao, ikiwa ni pamoja na kupunguza madeni yaliyopo katika Halmashauri na Serikali Kuu na kuwaagiza maofisa elimu kuhakikisha walimu wanalipwa stahiki zao kwa wakati.

Amesisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa walimu baada ya uchaguzi huku akiwataka kuacha kugawanyika na badala yake kushirikiana kwa maendeleo ya taaluma yao.

Katika uchaguzi huo, uliohusisha nafasi tisa za uongozi wa CWT Mkoa wa Njombe, Shabani Ambindwile alitangazwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 58 dhidi ya mshindani wake, Abubakari Kiya ambaye hakuambulia kura hata moja.

Msimamizi wa uchaguzi, Albert Ngendelo ambaye pia ni Ofisa Kazi Mfawidhi wa Mkoa wa Njombe, amesema uchaguzi ulikuwa wa amani na uwazi.

Ambindwile ameahidi kuendelea kushirikiana na walimu kwa kipindi kingine cha miaka mitano, akitaja kipaumbele chake kuwa ni kuhakikisha changamoto za walimu zinatatuliwa na kuwawezesha kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama cha walimu Mkoa wa Njombe wakiwa katika ukumbi uliofanyika uchaguzi mkuu wa chama cha walimu mkoa wa Njombe.

Kwa upande wake, mwalimu Rachel Atanas amesema wana imani kuwa viongozi waliowachagua watasaidia kutatua changamoto zao, akieleza kuwa Rais Samia ni kiongozi msikivu na mwenye kuwajali walimu.