Dawasa kufunga pampu kumaliza mgao wa maji Kinyerezi, Segerea na Bonyokwa

Dar es Salaam. Katika uboreshaji wa upatikanaji wa maji katika eneo la Segerea, Kinyerezi, Kifuru na Bonyokwa, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) inaanza kunjenga miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa maji maeneo hayo ili kuondokana na mgao wa maji.
Hayo yalisemwa jana Jumamosi, Septemba 22, 2023 na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu wakati wa ziara ya kutembelea na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo.
Alisema wamejipanga katika uboreshaji wa maji ili kuhakikisha kila mwananchi anapata maji kwa wakati na kuondokana na mgao wa huduma hiyo.
Kingu alisema wameweza kupata pointi katika eneo la King’azi B kwa ajili ya kujenga Pampu ya kusukumia maji itakayojengwa kwa wiki mbili itakayowezesha upatikanaji wa maji katika maeneo ya Kifuru na Bonyokwa ili wananchi waweze kupata maji kwa uhakika.
Akizungumza na wananchi wa Kisukuru, alisema changamoto iliyokuwepo katika eneo hilo ni kutokana na tatizo la ufungaji wa transifoma hivyo baada ya Shirika la Umeme Tanzanka (Tanesco) kumaliza kazi hiyo wataweka pampu ya kusukumia maji itakayosaidia kuleta maji kwa uhakika.
“Niwatoe hofu wananchi wa Kisukuru changamto zote ninazichukua na sisi kama Dawasa tunakwenda kuzifanyia kazi hivyo ili upatikanaji wa maji katika eno hili iwe historia,” alisema Kingu
Naye Meneja wa Mkoa wa Kihuduma Dawasa Kinyerezi, Burton Mwalupaso alisema wanataka kuweka pampu ya kusukumia maji ya kuongeza msukumo wa maji na kuyapeleka katika maeneo yote yanayohudumiwa na hili bomba ambayo ni Mtaa wa King’azi, Kifuru, Msingwa, Kibaga na Kanga.
Alisema kumalizika kwa ujenzi wa pampu ya kusukumia maji itapunguza mgao wa maji ambapo wananchi watapata maji kwa wakati kwani mkusumo wa maji utakuwa ni mzuri.
Kwa upande wake, Joachimu Minja, mwananchi wa Mtaa wa King’azi B aliishukuru Dawasa kwa kuja na wazo la kufunga pampu ya kusukumia maji kwani itakuwa ni mwarobaini wa mgao wa maji unaoendelea katika maeneo yao kwani wananchi wa eneo hilo wanateseka na pia wanafunzi hawawezi kwenda shule kwa wakati kutokana na upatikanaji wa maji kuwa haba.