Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawa ya wanaochukua kondomu nyingi yaja

Waziri wa nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama akizungumzia maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, (kushoto) Naibu Waziri Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndeliananga, (Kulia) ni Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dk Jim Yonazi

Muktasari:

  • Wakati wa kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, Serikali imezungumzia jitihada inazochukua katika kukabiliana na maambukizi mapya ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU), huku ikiandaa utaratibu kwa wale wanaochukua kondomu nyingi zilizowekwa maeneo ya umma.

Dodoma. Serikali inaandaa utaratibu wa kukabiliana na changamoto ya baadhi ya watu kuchukulia kondomu zote kwenye makasha yaliyosambazwa maeneo ya umma na hivyo kusababisha wasiokuwa na uwezo wa kununua, kuzikosa.

Meneja Programu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk Aneth Rwebembera ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 14, 2023 katika mkutano wa kuelezea maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani.

Mkutano huo uliitishwa na Tume ya Kudhibiti Ukumwi Tanzania (TACAIDS), ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Jenista Mhagama.

Akizungumzia suala hilo, Dk Aneth amesema mkakati wa Taifa wa kusambaza kondomu kwa jamii katika maeneo ya shule, vyuo, baa pamoja na maeneo mengine ya umma unaendelea japo kuna changamoto.

“Nikiri kuwa kuna tatizo ambalo limeanza kufanyiwa kazi, kondomu zikisambazwa na kuwekwa katika makasha sehemu mbalimbali za umma kama vile kwenye baa, vyuo, shule; kwakweli huwa zinachukuliwa zote kipindi kile kile zinapowekwa,” amesema.

Amesema hivi sasa wanaandaa mpango wa usambazaji mwingine ambapo kutakuwa na makasha ambayo huwezi kutoa kondomu zaidi ya tatu.

Amesema kwa kipindi walichoweka katika makasha hayo walijikuta kuwa mtu anaweza kuchukua kondomu zote lakini kwa utaratibu huo mpya utakapoanza, utawezesha jamii nzima kupata zana hizo wakati wanapohitaji.

Mhagama amesema upo mkakati wa Taifa ya Matumizi ya Kondomu ambapo ugawaji wa kondomu unafanyika bure bure katika maeneo ya jamii.

“Sasa ulikuwa unakuta kama zimewekwa 30 ama 40 mtu anachukua zote na kuondoka nazo. Na wakati mwingine akiondoka nazo yeye anakwenda kuziuza. Kwa hiyo matokeo yake wale ambao hawana uwezo wa kuzipata bure wanakosa hiyo fursa jamii,” amesema.

Amesema Tacaids kwa kushirikiana na Wizara ya Afya waandae makasha ambayo yatawezesha mtu kupata kondomu zisizozidi tatu.

Hata hivyo, amesema pia katika utafiti wao wanapaswa kuhakikisha kuwa hakuna uwezekano wa mtu kurudia mara kwa mara hadi kasha lisiishe.

Kuhusu upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Jerome Kamwela amesema uhamasishaji wa wanaume kupima unatokana na tafiti zilizofanywa mara nne mfululizo kuonyesha wako nyuma kwenye suala hilo.

“Wanaume kwa ujumla huwa ni wavivu sana kwenda kupata huduma za tiba na kwa msingi huo hata matokeo ya tiba kwa wanaume ni mabaya kuliko kwa wanawake, wote tunajua kuwa kiwango cha maambukizi kiko juu kwa wanawake kuliko wanaume. Wanaume ndio wanakufa zaidi na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi kuliko wanawake,” amesema.

Akizungumzia maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yanayofanyika kila Desemba Mosi, Mhagama amesema maadhimisho hayo yatafanyika Kitaifa mkoani Morogoro ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema maadhimisho hayo yatafanyika ndani ya wiki moja ambapo shughuli mbalimbali zinazohusu utoaji wa taarifa za udhibiti wa VVU na Ukimwi, pamoja na huduma ya upimaji wa hiari wa VVU zitafanyika kuanzia Novemba 24, 2023 hadi siku ya kilele ya Desemba, Mosi 2023.

Amesema pia katika kilele cha maadhimisho hayo Utafiti wa Viashiria vya VVU na Ukimwi (THIS) wa mwaka 2022/23 utatangazwa huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Jamii Iongoze Kutokomeza Ukimwi.”