Daraja la mto Wami kukamilika Septemba

Muktasari:
- Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 ambalo limezingatia sehemu ya barabara za magari, watembea kwa miguu na vizuizi kwa ajili ya usalama hivyo linatarajiwa kupunguza ajali katika eneo la Mto Wami na kuhuisha huduma za usafiri na uchukuzi katika barabara kuu ya Chalinze - Segera.
Dar es Salaam. Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Pwani, Yudas Msangi amesema daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 linalounganisha miji ya Chalinze na Segera mkoani Tanga litakamilika Septemba mwaka huu.
Msangi ameyasema hayo leo Aprili 24, wakati akimpa taarifa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara aliyefanya ziara ya kutembelea daraja hilo linalogharimu Sh67 bilioni litakalokuwa na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 3.8.
Taarifa ya wizara hiyo, imeeleza kuwa Msangi amesema ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 50.05 huku akimuahakikisha utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Waitara alisema uijenzi wa daraja la Wami ni mkakati wa Serikali katika kuongeza ufanisi katika barabara ya Chalinze - Segera na kupunguza adha kwa abiria nawasafirishaji wanaotumia daraja la zamani lenye urefu wa mita 88.75.
“Kutokana na umuhimu wa daraja hili Serikali imeamua kujenga daraja jipya ili kuondoa adha katika daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 kutokana na kutokidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa sasa.
“La zamani ni jembamba na lina njia moja na barabara zake unganishi kupita katika miinuko mikali na kona mbaya na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara”,amesema Waitara.
Waitara alimtaka mkandarasi wa Power Construction Corporation ya China, msimamzi wa mradi huo, kushirikiana na Tanroads kuongeza vifaa na wafanyakazi ili kazi ikamilike kama ilivyopangwa na kusisitiza akisema Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kwa wakati.
“Zaidi ya wafanyakazi 280 kati ya 300 wanaojenga daraja hili ni watanzania, hivyo hakikisheni wingi wenu mnautumia kubaki na ujuzi na kufanya kazi kwa uzalendo”, ameeleza.