Dar yatangaza usafi kila Jumamosi mwisho wa mwezi

Muktasari:
Mkoa wa Dar es Salam umetangaza Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi itakuwa siku maalumu ya kufanya usafi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam (RC), Amos Makalla ametangaza kuwa kila Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi itakuwa siku maalumu ya kufanya usafi kwa wakazi wa mkoa huo.
Makalla ametoa agizo hilo leo Jumatatu Novemba 22, 2021 kwenye uzinduzi wa mkakati wa usafi na uhifadhi mazingira wa mkoa huo uliopewa jina la 'Safisha Pendezesha Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo watendaji kuanzia ngazi ya Serikali za mitaa wamesaini mkataba wa utekelezaji wake kwa kusaini fomu maalumu kila mmoja.
Katika mkakati huo Makalla amesema moja ya mambo yaliyopo ni kuifanya siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku rasmi ya kufanya usafi.
Makalla amesema katika siku hiyo, kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kuanzia ngazi ya kaya, ili wananchi kujumuika katika kufanya usafi.
'Wewe Mwenyekiti Serikali ya Mtaa, Mtendaji hamasisha watu wako kufanya usafi na Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kwa kuwa ndio itakuwa rasmi ya kufanya usafi katika mkoa huu,
"Pia Mkuu wa Wilaya ndio atakuwa mratibu wa shughuli hiyo na kuwa mgeni rasmi katika shughuli mbalimbali za ufanyaji usafi katika maeneo yake kwa namna watakavyojipangia"amesema Makalla.
Katika mkakati huo pia amesema baadhi ya nyumba za watu binafsi, mashirika na kampuni yanapaswa kupakwa rangi na tayari ameshawapa baadhi barua ya kufanya hivyo.
Amewaonya watu ambao wamekuwa wakingoa na kuondoa urembo mbalimbali zilizowekwa kupendezesha mji na kueleza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
RC Makalla amewataka mameya na wakurugenzi kwenda kuziangalia upya sheria ndogondogo za usimamizi wa mazingira na usafi kuona namna gani wanaziboresha ili ziweze kufanya kazi kulingana na wakati wa sasa.