Dar yaongoza waliokamatwa kwa dawa za kulevya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama akizungumza alipotoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2023, leo Mei 16, 2024 jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
Taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2023 yaonyesha hadi Desemba 2023, waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipatiwa huduma hospitalini.
Dodoma. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi ya watu wanaokamatwa na dawa za kulevya, Serikali ikieleza imejipanga kuweka jicho la ziada kudhibiti matumizi na biashara ya dawa hizo.
Maeneo ya kumbi za starehe na fukwe zimetajwa kutumika kuuza biskuti zenye bangi.
Hayo yameelezwa leo Mei 16, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama alipowasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2023 kwenye ukumbi wa habari wa Bunge jijini Dodoma.
“Mkoa unaoongoza hadi sasa ni Dar es Salaam, tutazunguka lakini ukirudi Dar es Salaam unakutana nao. Tunashukuru Mamlaka imejipanga vizuri na imefanya kazi nzuri, tutazunguka nchi nzima lakini kwa Dar es Salaam tumeweka kituo,” amesema.
Amesema idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini ni vijana, ambao kwa wastani ni asilimia 78, hali inayoathiri nguvu kazi ya Taifa.
Mhagama amesema hadi kufikia Desemba 2023, waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipatiwa huduma hospitalini.
“Hii ni hatua muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya kama vile, uraibu, VVU/Ukimwi, Kifua Kikuu, Homa ya ini, magonjwa ya akili na mengine yasiyoambukiza,” amesema.
Amesema kwa kipindi hicho mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola zilikamata kilo milioni 1.96 za dawa za kulevya zikihusisha watuhumiwa 10,522 ambao kati ya hao 9,701 ni wanaume na 821 wanawake.
Amesema dawa zilizokamatwa ni heroini kilo 1,314.28, kokeini kilo 3.04, methamphetamine kilo 2,410.82, bangi kilo 1.75 milioni na mirungi kilo 202,737.51.
Nyingine ni skanka kilo 423.54 na dawa tiba zenye asili ya kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672.
Mhagama amesema dawa zilizokamatwa ni takribani mara tatu ya kiasi kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilo 660,465.4.
Amesema dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi zilikamatwa katika kipindi hicho.
Waziri Mhagama amesema Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2024 inayolenga mambo kadhaa ikiwamo kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi.
“Sera inatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mbadala katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha mazao hayo ili wananchi wa maeneo husika wajihusishe na kilimo cha mazao halali badala ya bangi na mirungi,” amesema.
Amesema sera inaelekeza kuwajengea uwezo wadau katika udhibiti wa dawa za kulevya ili ushiriki wao ulete tija katika mapambano hayo.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema kesi zaidi ya 7,000 zimehukumiwa na Serikali imeshinda kwa asilimia 83 ya kesi zote.
“Asilimia 17 ya kesi tulizoshindwa inatokana na kesi kuondolewa mahakamani kwa ushahidi kutokamilika, lakini ukijaribu kuangalia kesi tulizoshinda ni asilimia kubwa. Hatua ni nzuri na mahakama inatenda haki,” amesema.
Akizungumzia biskuti zenye bangi, Kamishna wa Kinga na Tiba wa DCEA, Dk Peter Mfisi amesema bei yake ni kubwa kuliko iliyotengenezwa na unga na zinauzwa kwenye kumbi za starehe na ufukweni.
“Mtu akinunua siyo kwamba amenunua kwa bahati mbaya wanataka kumfundisha, watoto wetu ambao wazazi wana uwezo wa kuwapa Sh1,000 kwenda nazo shule ndio wanaolengwa sana, wale ambao hawazijui wanapewa kama kuwafundisha ili watumie,” amesema.
Amesema biskuti hizo zilizotengenezwa kwa bangi hazina lebo na hazina shepu nzuri kama zingine na wanaonunua wanajua.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii unapokuta biskuti lazima usome zimetengenezwa wapi, vitu vilivyotumika ukiona mtu amekuletea au hazina shepu utaingizwa kwenye utumiaji huo ili ukizoea uendelee kutumia kila siku,” amesema.