CWT waviziana majibu viongozi wao waliokacha teuzi

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga akizungumza kwenye mkutano wa chama hicho, kushoto kwake ni Rais wa Chama hicho Leah Ulaya. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Viongozi wa CWT akiwemo Rais Leah Ulaya aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe lakini Katibu mkuu wake Japheth Maganga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.
Dodoma. Viongozi wa Baraza la Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wapo jijini Tanga kwa ajili ya kikao kesho, huku baadhi ya wajumbe wakitaka majibu ya hatma ya viongozi wakuu waliokacha nafasi za uteuzi.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga hakuthibitisha kikao hicho lakini ametuma ujumbe wa maandishi kuwa yupo kwenye kikao jijini Tanga.
Hata hivyo taarifa za ndani kutoka kwa wajumbe leo Jumapili Februari 5, 2023 zinaeleza kuwa kikao kitakuwa na mgawanyiko wa makundi kwani baadhi ya wajumbe wana shauku ya kujua kama wateule hao wamejibiwa barua walizoomba kutoendelea na taratibu za uteule.
Rais wa CWT, Leah Ulaya aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe lakini Katibu Mkuu wake Japheth Maganga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.
Hata hivyo wawili hao walikacha uteuzi huo kwa sababu kwamba wana majukumu ya kuwahudumia walimu ambao ni kundi kubwa huku Makamu wa Rais wa CWT, Dinah Mathamani akiapishwa na kuanza kazi katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Kikao cha Baraza la CWT Taifa watajadili bajeti ya mwaka na mipango mingine ndani ya chama ambapo kila mkoa wa Tanzania bara unawakilishwa na wajumbe saba.
Baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wanasema kesho watataka kujua ikiwa maombi ya kuacha uteuzi walishajibiwa au wamepotezea na kuendelea na majukumu.
"Kikubwa lazima tujue hilo maana chama chetu kitaangaliwa vibaya na Serikali kana kwamba kuna maslahi mapana huku, iwapo watakuwa wamejibiwa hatutasema kitu sisi mambo yatakuwa supa," alisema mmoja wa wenyeviti wa mikoa.
Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Njombe, Shaban Ambindule yeye amesema hajapokea ajenda za kikao ili alinganishe na hoja zilizo mbele yake ndipo atakuwa na jambo la kusema.