Utata ma-DC wateule wakikacha kuapishwa

Wakuu wa wilaya wapya mkoani Geita, Grace Kingalame (Nyang’hwale), Deusdedith Katwale (Chato) na Cornel Magembe (Geita) wakila kiapo cha maadili katika hafla ya kuapishwa kwao iliyofanyika mkoani humo jana. Picha na Rehema Matowo
Geita/Tanga. Vigogo wawili wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), wameibua mijadala kutokana na kutohudhuria hafla ya kuapishwa kuwa wakuu wa wilaya na kuahidi kutoa taarifa ya nini kinaendelea juu ya nafasi zao hizo mpya za utumishi serikalini.
Janauri 25 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya (DC) kwa kuwahamisha baadhi, kuwatema na kuteua wapya 37 wakiwemo wawili ambao ni viongozi wa juu wa chama hicho cha walimu.
Viongozi hao ni Leah Ulaya, Rais wa CWT aliyeteuliwa kuwa DC wa Mbogwe, Mkoa wa Geita pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Mjadala wa wawili hao, uliibuka baada ya wawili hao kuonekana jijini Tanga katika Hoteli ya Regal Naivera, Mtaa wa Bombo wakishiriki kikao cha kamati ya utendaji wa CWT.
Alipoulizwa na gazeti hili kwa nini wapo hapo kwenye kikao badala ya kwenda kuapishwa, Ulaya alijibu kwa kifupi, “tutatoa taarifa rasmi fanyeni subira kwanza.”
Mwananchi lilimtafuta, Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki kutaka kufahamu endapo kuna taarifa za wawili hao kutokwenda maeneo yao ya kazi ambapo alisema,”mtafuteni msemaji mkuu wa Serikali.”
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipotafutwa saa 12 jioni alisema, “leo sipo ofisini, ngoja niulize kwanza, nijue nini kimetokea.” Timu ya Mwananchi ililokuwapo nje ya hoteli hiyo lilimshuhudia Maganga wakati wenzake wakiendelea na kikao, alitoka nje saa 4:36 asubuhi na kuanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.
Maganga alihojiwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga kwa zaidi ya dakika 50 hadi saa 5:24 asubuhi. Baadaye Mwananchi lilimuuliza Maganga sababu za kuhojiwa, hakueleza na hata walipoulizwa polisi nao hawakuwa tayari kueleza.
Alipoulizwa sababu za kutokwenda kituo chake cha kazi Kyerwa alisema, “kwa sasa nimeziba mdomo labda usubiri tutakapomaliza kikao ndipo nitazungumza kuhusu nafasi ya U-DC na CWT.”
Hata hivyo, kikao hicho kilikwenda hadi jana jioni na walipopumzika mchana kwa ajili ya chakula, bado hakuwa tayari kueleza chochote.
Mbali na Maganga, Rais wake, Leah Ulaya wakati wenzake mkoani Geita wakiapishwa na mkuu wa mkoa huo (RC), Martin Shigela yeye hakuwepo na ikielezwa hakuna taarifa yoyote ya udhuru aliyoitoa kwenye mamlaka ya mkoa.
Ingawa wawili hao wameshindwa kuweka wazi, taarifa ambazo gazeti hili linazo na zilizungumzwa katika kikao hicho kinachoendelea jijini Tanga ni wao kumwomba Rais Samia kuteua watu wengine kushika nafasi hizo. Kama hawatokwenda kuapishwa, hawatakuwa wa kwanza kufanya hivyo, kwani imewahi kushuhudia wakati wa utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kuna baadhi waliteuliwa nafasi za U-DC, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na katibu tawala wa wilaya (DAS) na hawakwenda kwa sababu mbalimbali na wakateuliwa wengine.
Akizungumza na gazeti hili lililohoji sababu ya mteule huyo, Ulaya kutoonekana ukumbini wakati wa uapisho, RC Shigela alisema uapisho huo ulipangwa kwa wateule wote, lakini Ulaya hakufika na hakutoa sababu za kutofika. Alisema hawezi kusema siku maalumu ya kumuapisha kwa kuwa hana taarifa zake na kwamba endapo ataripoti taarifa itatangazwa upya na atamuapisha kama alivyowaapisha wengine.
RC wa Kagera, Albert Chalamila alipoulizwa kutokuwepo kwa Mganga wakati akiwaapisha wengine alisema, “mimi naapisha waliokuwepo, ambaye hayupo sababu anazijua aliyemteua.”
Wakuu wa wilaya wateule walioapishwa na wilaya zao kwenye mabano ni, Grace Kingalame (Nyang’hwale), Deusdedith Katwale (Chato) na Cornel Magembe wa Geita.
Wakati Maganga na Ulaya wakishindwa kuripoti katika mikoa walikoteuliwa, aliyekuwa Makamu wa Rais wa CWT, Dinah Mathamani aliyeteuliwa kuwa DC wa Uvinza, Mkoa wa Kigoma anaapishwa leo na tayari tangu jana alikwisha kufika mkoani humo.