Dar es Salaam. Zimebaki siku chache kumalizika mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC – COP28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, utakaohitimishwa Desemba 12, 2023.
Maazimio na misimamo ya nchi imeonekana na mikataba mbalimbali kusainiwa kwenye ngazi za juu.
Mwananchi imefanya mahojiano na wanawake watatu wanaoshiriki mkutano huo kufahamu namna shughuli wanazofanya zinavyoweza kuchochea juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Upendo Mwakyusa, mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Call for Environmental Conservation (CFEC) anasema anatekeleza mradi wa wanawake, watoto na vijana unaoshughulika na haki na usawa wa makundi hayo kwenye mazingira.
Akifafanua miradi hiyo, anasema: “Tunalenga kuhakikisha makundi haya hayaachwi nyuma kwenye mabadiliko ya tabianchi. Mfano, mradi wa watoto tumeandaa vitabu vya lugha nyepesi vinavyozungumzia mazingira. Tulibaini lugha tunazotumia si shirikishi kwa watoto, hivyo vitabu hivi vinasaidia.”
Anasema kwenye mkutano huo unaokutanisha viongozi, watekelezaji, watunga sera, wafanya maamuzi na watu wanaotoka kwenye mazingira na jamii tofauti ni muhimu kwa vijana, wanawake na watoto kushiriki kwa sababu kila tendo ni muhimu.
Akizungumza namna ya kufikisha elimu kwa watoto, Upendo anasema: “Tunatembea kwenye shule tunafundisha kwa vitendo kufanya usafi, kutunza na kutenganisha taka, kupanda miti. Pia tunawapa fursa za kuchora picha inayozungumzia au kutoa ujumbe wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira.”
Anasema hivi sasa wanaandaa vitabu vya hadithi za mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambavyo vinaakisi uwezo na uelewa wa watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Human Dignity and Environment Care (Hudefo), Sarah Pima anasema licha ya kuwa na miradi mingi, alioupeleka Cop28 na kuusimamia ni wa Wajibu kwa Wazalishaji Taka (EPR), hasa za plastiki ambazo ni hatari kwa mazingira.
Mradi huo anasema unalenga kujenga uelewa kwa jamii na watunga sera kuja na mikakati itakayowapa jukumu la kusafisha mazingira wazalishaji wa plastiki, jambo ambalo halipo Tanzania.
“Dunia inalenga kupunguza hewa ukaa ili halijoto iendelee kuwa chini ya nyuzi joto 1.5 za sentigrade ifikapo 2030. Sasa ukiangalia mzunguko wa plastiki kila inavyojimeng’enya inazalisha hewajoto, hivyo ni muhimu kudhibiti taka za plastiki,” anasema.
Anasema taka za plastiki licha ya kuongeza hewajoto, zinaharibu bayoanuai katika mazingira, kuleta sumu kwenye maji, hasa baharini na madhara kwenye mazingira. Hivyo wamechagua suala hilo kwa kujifunza namna nchi nyingine zinavyofanya kudhibiti taka hizo na kugundua namna nchi inavyoweza kufanya, hivyo kusaidia katika suala la utoaji wa elimu.
Sarah alisema:
“Licha ya kwamba nchi yetu haina sheria ya kumlazimisha mzalishaji kurejeleza, lakini tunaendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kuhifadhi taka hizo, ijapokuwa kwa kiwango kidogo wapo wanaofanya suala hilo hasa maeneo ya mijini.”
Anasema miongoni mwa yaliyoamuliwa kitaifa nchini kwenye kudhibiti mabadiliko ya tabianchi (NDCs) ni udhibiti wa taka hizo, hivyo wanaunga mkono juhudi hiyo.
Katika hatua nyingine, Sarah aliwashauri wanawake kushiriki katika fursa mbalimbali zilizopo, akitoa mfano wa ushiriki kwenye mpango uliozinduliwa na Serikali kwenye mkutano huo wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake.
“Sisi tunaweza kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo. Vipo vitu mbalimbali tunaweza kufanya kwenye mnyororo wa thamani wa masuala haya na tukapata ufadhili wa Serikali au sekta binafsi,” anasema.
Ametoa mfano wa suluhisho kuwa ni matumizi ya majiko banifu, kutengeneza bidhaa nyingine kutokana na taka kama vile mkaa na urembo.
Amesema ili kufanikisha hayo, vijana na wanawake wanatakiwa kujiendeleza kwa kusoma na kushirikiana kutafuta watu wa kuwezesha kutekeleza mambo hayo ili kuongeza uelewa na uwezo wa kushiriki.
Pia lilizungumza na Shamim Nyanda, mwanzilishi wa Taasisi ya Milango ya Matumaini (DHF) inayojihusisha na utoaji elimu na uwezeshaji kwa kuonyesha fursa kwa makundi ya vijana na wanawake juu ya mabadiliko ya tabianchi.
Shamim alisema anachofanya kwenye Cop28 ni kuangalia namna vijana na wanawake wanavyohusishwa kwenye maamuzi mbalimbali na majadiliano, akiwa mwakilishi wa makundi hayo.
Alisema anafanya hayo kwa kuwa pia anafanya kazi kama mshauri wa vijana kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi kwenye sera za kimataifa, hivyo anatambua kundi kubwa zaidi la watu ni vijana na wanawake.
Alisema: “Jambo jingine ninalofuatilia ni kushiriki kwenye mijadala inayohusu fedha za ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania. Tunafahamu nchi imepata mafuriko ambayo unaweza kusema yamesababishwa na athari za jambo hili, lakini fedha za kukabiliana na majanga kama hayo hakuna,” alisema.
Alisema kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ni sehemu ya mfuko wa fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (GCA), wanashiriki kwenye mijadala kwa kuwa fedha hizo ni muhimu.
Shamim alisema pia ni mshiriki wa Youngo (wawakilishi wa vijana na watoto UNFCCC) hivyo anashiriki kwenye mijadali mikubwa inayoendelea, hususan inayohusu maamuzi ya mwelekeo wa dunia kwenye mabadiliko ya tabianchi na NDC.
Alisema pia ameshiriki mjadala unaohusu woga na wasiwasi wa mabadiliko ya tabianchi kwa vijana kujadili namna wanavyoshirikishwa na wanawaza mbeleni itakuwaje kutokana na majanga na madhara yanayotokea.
“Tunaangalia namna ya kupata nafasi ya kuwashirikisha vijana watoe hisia zao na kuzibadilisha hisia hizo kuwa mitazamo halisi na kuongeza ushiriki wao,” alisema.
Mjadala mwingine alisema ni kuhusu madeni kwa nchi za Afrika ambayo yapo juu, hivyo wanaangalia namna zinavyoweza kusamehewa madeni na si kubadilishiwa namna ya kulipa.
Hatua hiyo anasema itawezesha nchi badala ya kujikita kwenye kulipa madeni, fedha zitafanya juhudi za kupambana na madiliko ya tabianchi.
Shamim alisema anafanya kazi kuanzisha Kituo cha Tanzania Ocean Climate Innovation Hub, kitakachofanya kazi ya kuangalia haki ya uhifadhi wa bahari, sayansi na wajasiriamali wa shughuli za bahari.
Kutokana na hilo, alisema siku ya bahari kwenye Cop28 (leo), Desemba 9, 2023 kwenye jukwaa la Tanzania ataendesha mjadala unaohusu kituo hicho kinachotarajiwa kuanzishwa nchini.
Pia alisema atashiriki kwenye mjadala wa uhifadhi wa rasilimali za bahari.