Mabadiliko ya tabianchi yanavyogusa afya, chakula

Muktasari:
- Wadau wa afya wamesema yanaathiri moja kwa moja sekta ya afya, utoaji huduma na lishe.
Dar es Salaam. Wadau wa afya wamesema mabadiliko ya tabianchi yanaathari za moja kwa moja kwa afya, utoaji huduma na lishe, hivyo jitihada za haraka zinahitajika kutatua matatizo hayo.
Hayo yameibuliwa jana Desemba 6, 2023 kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ngazi ya mawaziri wa afya kutoka nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wakati wa mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC – COP28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri wa Afya nchini, Ummy Mwalimu ameuambia mkutano huo kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ongezeko la magonjwa ya mlipuko na vifo, hususan kwenye nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Magonjwa kama kuhara, malaria, dengue na yasiyopewa kipaumbele kama usubi, chikungunya, kichocho, matende na magonjwa ya mfumo wa hewa yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ama ongezeko la joto na mvua kubwa au chache zinazoleta mafuriko au ukame,” amesema.
Kuhusu usalama wa maji, Waziri Ummy amesema asilimia 88 ya wakazi wa mijini ndiyo wanaopata huduma hiyo na kwa upande wa vijijini ni asilimia 77, wakati watu wenye vyoo vya aina yoyote ni asilimia 98.
“Majanga ya mafuriko yamesababisha kuharibu vyanzo vya maji na miundombinu iliyopo, hivyo kusababisha upungufu na hatimaye milipuko ya magonjwa," amesema Waziri Ummy.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema viongozi wengi wa nchi duniani wanatambua madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ipo haja ya kuwekeza katika eneo hilo.
Pia amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikishwa kwa karibu kutatua changamoto za majanga ndani ya maeneo yao.
“Mabadiliko ya tabianchi ni janga la afya,” amesema Dk Ghebreyesus.
Lishe na mabadiliko ya tabianchi
Ofisa Lishe na Mtafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Walbert Mgeni amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ukame na lishe kwa sababu upatikanaji wa vyakula vingi hutegemea maji.
Ametoa mfano wa sasa nchi kuwa katika upungufu wa vyakula kutokana na mvua chache msimu uliopita.
“Nina uhakika ukipima watu wengi, utakumbana na tatizo la ukondefu. Hili linasababishwa na ukosefu wa vitamini ‘A’ na chakula kisichotosha,” amesema.
Mgeni anasema ukame unasababisha kukosekana mboga za majani za kijani na matunda ambavyo ndivyo vyanzo vikuu vya vitamini ‘A’, lakini pia ukosefu wa malisho kwa wanyama.
Tatizo hili linapoendelea kwa muda, amesema husababisha aina nyingine za utapiamlo kwa watoto kama vile udumavu na uzito mdogo.
Akihusianisha mabadiliko ya tabianchi na lishe, Mgeni amesema yameathiri kilimo kwa kiasi kikubwa na mifumo ya vyakula kwa baadhi ya maeneo, hivyo lishe za watu kuathirika.
Ametaja maeneo yanayoathirika zaidi kuwa ni mikoa ya kati ya nchi, ingawa hali hiyo kwa sasa inaenda kwa mikoa mingi.
“Watu unakuta walizoea kulima na kula ndizi au wali tu, sasa wanatakiwa kuhama na kulima mihogo, mtama na mazao mengine yanayostahimili ukame, wengi wanashindwa na hapo ndipo madhara yanapotokea,” anasema.
Mgeni ameshauri kuzingatia makundi ya chakula ambayo ni nafaka, mizizi na ndizi. Kundi jingine ni asili ya wanyama, mbogamboga na matunda na kundi la mwisho ni mafuta, sukari na asali ambavyo hushauriwa kutumika kwa kiasi kidogo.
Mdau wa mazingira, Dk Philip Osano amesema tafiti zinaonyesha upo uwezekano mdogo wa kuongezeka tija kwenye kilimo, kwani tathmini inaonyesha kupungua mavuno katika mazao muhimu matano kati ya sita hadi 2025.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na chombo cha habari za mazingira, sayansi na afya (Mesha), Osano amesema mabadiliko ya tabianchi yanaleta wasiwasi kwenye usalama wa chakula na biashara.
“Mavuno ya mahindi yatapungua kwa asilimia 27, mpunga asilimia 8.1, maharage asilimia 7.2, miwa asilimia 58.5, kahawa asilimia 23 hadi 45 na ngano pekee inatarajiwa kuongeza mavuno kwa asilimia 13.9,” amesema.
Watoa mwelekeo
Waziri Ummy amesema Serikali inafanya jitihada za makusudi kuandaa mpango mkakati na miongozo ya kukabiliana na majanga katika sekta ya afya.
“Wizara imeandaa mfumo wa taarifa unaoweza kubashiri uwezekano wa kutokea milipuko ya magonjwa. Pia, inatafuta fedha za kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa,” amesema.
Ofisa lishe Mgeni ameshauri watu kubadili aina za kilimo na ufugaji kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na matunda kama vile mapapai.
Mgeni ameshauri kufanya kilimo cha viroba na kufuga wanyama wadogowadogo kama kuku, sungura na bata ambao ni rahisi kuwahudumia.
Dk Osano ametaja maeneo matano ya kufanyiwa kazi ambayo ni nishati, makazi, kilimo, usafirishaji na mifumo ya usimamizi taka kama mihimili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya afya.
“Kuna uchafuzi mkubwa wa hewa na mazingira, hivyo tunahitaji kuhakikisha tunawekeza kwenye nishati safi za matumizi ya nyumbani na viwandani, kufanya kilimo stahimilivu, kuwa na mifumo mizuri ya kuhifadhi taka na kuhakikisha matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi,” amesema.