Chongolo amwita Waziri Silaa kujibu kero Katavi
Muktasari:
- Silaa anakuwa waziri wa tano kuitwa mkoani Katavi kutoa majibu ya changamoto zilizoibuliwa na wananchi na viongozi mkoani humo.
Katavi. Ni mwendo wa mawaziri kuitwa kushughulikia matatizo ya wananchi na sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa anapaswa kutua mkoani Katavi.
Ni agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo alilolitoa mbele ya wananchi wa wilaya ya Mlele, mkoani Katavi leo Oktoba 5 katika mkutano wa hadhara uliofanyikia uwanja wa Shule ya Msingi Inyonga.
Silaa anakuwa waziri wa tano kuitwa mkoani humo kutoa majibu ya changamoto zilizoibuliwa na wananchi na viongozi mbalimbali katika ziara ya Chongolo ya siku tano itakayohitimishwa kesho kwa mkutano mkubwa wa hadhara.
Chongolo amemwita Waziri Silaa kufuatilia malalamiko yaliyoibuliwa na Mbunge wa Katavi (CCM), Isaac Kamwelwe na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mlele, Geofrey Pinda.
Pinda amesema kuna migogoro mikubwa ya ardhi ambayo imekuwa kero kwa wananchi huku Kamwelwe akimwomba kulifanyia kazi kwani wananchi wamekuwa wakipata maswaibu.
Kamwelwe aliyewahi kuwa Waziri wa Ujenzi amesema, alama za mipaka ya hifadhi zimewekwa hadi kwenye mashamba ya wananchi na kuwafanya waishi kwa hofu na akisisitiza alama za awali ziliwekwa tangu miaka ya 1950 idadi ikiwa ndogo ukilinganisha na sasa.
Akijibu hilo, Chongolo amesema yeye si mtaalamu wa masuala ya ardhi lakini, "tarehe 7 (kesho) nitakuwa na mkutano wa hadhara Mpanda Mjini, nimemwita waziri wa ardhi aje pale akae na wataalamu wake atueleze hili atalimaliza vipi."
Hoja nyingine aliyoijibu ni ya ujenzi wa chuo cha afya iliyotolewa na Kamwelwe kuwa chuo hicho kitawezesha kuwa na wataalamu wengi.
"Nimekichukua, nakwenda nalo ili vijana wetu wapate mafunzo ya afya huku na kutawanya nchini kote na eneo la chuo kiwe karibu na hospitali. Kikubwa hakikisheni eneo linapatikana zaidi ya ekari 40 au 50."
Mbali na Silaa, mawaziri wengi waliotajwa kufika kutokana na wizara zao kutajwa kama za umeme, maji, barabara, afya, maliasili na utalii na wizara zao kwenye mabano, Jumaa Aweso (Maji), Innocent Bashungwa (ujenzi), Mohammed Mchengerwa (Tamisemi) na Dk Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Katika mkutano huo, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya chama hicho, Issa Ussi Gavu alisema
kama kuna sheria kandamizi na ambazo zinaleta shida kwa wananchi watazifanyia kazi kadri wananchi wanavyotaka,"na hatutaki kuwagawa kwa aina yoyote ile."
Katika kusisitiza hilo, Gavu alisema,"...sisi kama CCM tunaamini waajiri wetu ni ninyi wananchi, hivyo tutawasikiliza wananchi na tutayafanyia kazi na sisi kama chama tutaongoza nchi kwa kuwasikiliza wananchi na si vinginevyo ili keki ya Taifa iwanufaishe wote," amesema
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko alisema katika utawala wa awamu ya sita, mkoa huo umepokea zaidi ya Sh803 bilioni ambazo zimekwenda kwenye sekta ya afya, maji, madarasa, vifaa tiba, kilimo, umwagiliaji na mbolea za ruzuku.
Mrindoko aliwataka wananchi wa mkoa huo kijenga viwanda vya kuchakata mazao kama mahidi, mpunga na alizeti ili kuwaongezea fedha na kuchangia pato la taifa na mkoa.
"Lakini jingine, niwaombe sana wananchi wenzangu, tutunze misitu na vyanzo vya maji kwani tukiiharibu misitu, tutakuwa tunajitengenezea mazingira magumu sisi wenyewe," alisema Mrindoko
Awali, Mbunge wa Katavi (CCM), Issack Kamwelwe kati ya vijiji 18 vya jimbo lake ni vijiji viwili pekee havijafikiwa na huduma hiyo navyo vitaunganishwa hivi karibuni huku upatikanaji wa maji utakwenda kumalizika baada ya ujenzi wa chujip la maji katika Bwawa la Nsenkwa utakapokamilika.
Bwawa hilo limejengwa kwa ajili ya kuwa chanzo cha maji safi na salama kwa matumizi ya wananchi wa vijiji 16 katika Halmashauri ya Mlele mkoa wa Katavi ambao utawahudumia takriban wakazi 68,000.
Kamwelwe aliyewahi kuwa na waziri wa ujenzi na uchukuzi alisema utekelezaji wa ilani ya chama hicho jimbono humo kwenye sekta ya umeme, maji, afya zinakwenda vizuri huku barabara za jimbo hilo lenye kata sita nyingi zikiwa zimeunganishwa na lami.