Chongolo aitaka Wizara kudhibiti tembo wanaoharibu mazao Meatu

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kudhibiti changamoto ya tembo wanaoharibu mazao ya wananchi wilayani Meatu katika Mkoa wa Simiyu.
Meatu. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kudhibiti changamoto ya tembo wanaoharibu mazao ya wananchi wilayani Meatu katika Mkoa wa Simiyu.
Kauli hiyo ya Chongolo imekuja baada ya miezi mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoiagiza Wizara hiyo kushughulikia changamoto hiyo.
Katika maelezo yake alipokuwa ziarani Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu leo Jumatano Juni Mosi, 2022, Chongolo amesema kuwapo kwa changamoto hiyo hadi sasa ni ishara kwamba Wizara husika imekaidi au kudharau maelekezo ya Rais.
"Hatuwezi kuwa na watu wanaoagizwa na Rais juu ya kuchukua hatua hawafanyi wanakaa ofisini, hii inaleta matatizo kwa wananchi na inaonyesha dharau kwa aliyekuagiza," amesema.
Amewahakikishia wananchi ndani ya mwezi mmoja uongozi wa wizara hiyo utakwenda eneo hilo kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa CCM haitaridhia kuona wananchi wanateseka ilihali kiliomba ridhaa ya kuwaongoza vyema.