Chalamila awashauri Dawasa kuzalisha umeme wao

Muktasari:
- Kutokana na matumizi makubwa ya fedha za kununua umeme kwa Dawasa kwa lengo la kuzalisha na kusambaza maji kwa wateja wao huku wameshauriwa kuzalisha umeme wao wenyewe ili kupunguza gharama.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameshauri Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dawasa, kuwa na chanzo chake cha kuzalisha umeme.
Chalamila ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 22,2023 alipotembelea mradi wa maji wa kisima cha Kigamboni.
Amesema kwa kuwa na chanzo hicho cha umeme itawaepusha kutumia Sh2 bilioni kwa mwezi kwa ajili ya nishati hiyo katika kuzalisha na kusambaza maji kwa wateja wao.
"Bilioni mbili ni nyingi sana kwa mwezi, hivyo mkiwa na chanzo chenu cha umeme mtaepusha fedha hizi na kwenda kufanyia kazi zingine ikiwemo kuanzisha miradi mingine ya maji.
Lakini pia umeme utakaobaki mtaweza kuwauzia Tanesco na hivyo kujiongizia kipato," amesema Chalamiala.
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu amesema wamelipokea hilo na kubainisha kwamba juhudi hizo zimeanza kwa mradi wao wa kidunda ambao kukamilika kwake utaweza kuzalisha Megawati 20.
Katika hatua nyingine Chalamila aliwahakikishia wakazi wa Dar es Salaam uwepo wa maji ya kutosha wakati mahitaji ya maji kwa mkoa huo yakiwa ni lita za ujazo 544 milioni ambapo yanayozalishwa ni lita za ujazo 590.
Amefafanua kuwa pamoja na uwepo wa malalamiko ya maji kutowafikia wananchi wengi, hiyo imechangiwa na mambo mengi ikiwemo usambazaji wa miundombinu ya kupeleka maji pamoja na uchakavu wa miundombinu hiyo.
"Wananchi waelewe kuwa kinachotakiwa kwanza ni eneo la kupata chanzo cha maji, kwani huwezi kuweka miundombinu ya kusambaza maji wakati hujui utayapata wapi.
Tunashukuru hilo limeshafanyika mpaka sasa na kazi inayoendelea ni kuwafikishia wananchi maji kwa kujenga miundombinu ya usambazaji," amesema Chalamila.
Akielezea maendeleo ya mradi wa Kigamboni, Kingu amesema wakati wanauzindua mradi huo Novemba mwaka jana, walikuwa wameshazambaza kilometa 25 lakini mpaka kufika sasa tayari wamesambaza kilometa 125.
"Niwahakikishie wananchi hadi kufika Novemba wote watakuwa wamefikiwa na huduma ya maji na tutafanya hivyo kwa kuwakopesha na kulipa ndani ya miezi sita," amesema Kingu.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo, amesema moja ya maswali wanayopokea kutoka kwa wananchi wa Kisarawe 2 ambapo tanki hilo lipo ni mitaa yake yote 11 kutofikiwa na huduma ya maji.
"Alipokuja Rais alisema wanachi wa karibu wafikiwe na maji, japo sisi wengine tunaelewa maelezo ya wataalam kuwa kuwepo kwa tanki la maji karibu hakumaanishi nyie ndio mpate maji wa kwanza.
Kwa wenzetu wananchi hili limekuwa gumu kuelewa utaalam huo, hivyo tunaomba Dawasa ifikishe huduma hii kwa maeneo hayo yaliyobaki hapa Kigamboni," amesema Bulembo.