CCM yasitisha ziara kuomboleza msiba wa Lowassa

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akizungumza na wanahabari kuhusu kusitisha ziara yake kwa mikoa Mtwara na Lindi iliyokuwa imesalia.
Muktasari:
- CCM imesitisha ziara zake kufuatia kifo cha Waziri Mkuu mstaafu Lowassa. Vyama vingine vimeshauriwa kufuata mkondo huo. kwa siku tano za maombolezo.
Songea. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesitisha kwa muda ziara ili kuungana na wananchi kuomboleza kifo cha Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.
Kiongozi huyo mstaafu amefariki dunia jana Jumamosi Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
CCM imeshauri vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kusitisha kwa muda matukio yake ili kupisha msiba huo.
Lowassa aliyewahi kuwa kada wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti, alifariki dunia saa nane mchana JKCI alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua magonjwa ya kujiku nja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Msimamo wa CCM wa kusitisha ziara umetangazwa leo Jumapili Februari 11, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Paul Makonda alipozungumza na wanahabari katika ofisi ya chama hicho Mkoa wa Ruvuma.
"Nilianza ziara yangu Januari 19, 2024 jana nikaingia Mkoa wa Ruvuma ukiwa ni mkoa wa 18 kati ya 20 niliyopanga kuitembelea, lakini kwa masikitiko makubwa mwenyekiti wetu (Rais Samia Saluhu Hassan), ametangaza kuondokewa na mpendwa wetu Mzee Lowassa.
"Kutokana na msiba huo tulilazimika jana kufanya mkutano katika mazingira magumu, tusingeweza kuwaacha wananchi waondoke bila kusikiliza kero zao, lakini mwisho tumelazimika kuungana kwa vitendo kuombeleza msiba huu," amesema Makonda.
Amesema baada ya mashauriano, chama hicho kimeamua kuahirisha ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara, hadi itakapopanga ratiba nyingine ili kuungana na Watanzania katika kipindi hiki cha maombelezo.
"Ni busara na tuwaombe wananchi katika mikoa iliyobaki kuwa ziara yetu tutaipanga tena kwa wakati mwingine, nafahamu zipo shughuli za kisiasa zinazoendelea za ndugu zetu wa Chadema wana mipango, wangesitisha kwa muda.
"lakini Serikali yetu inashiriki mipango mingi ya kitaifa na mzee wetu Lowassa amewagusa watu wengi na watani zetu wanafahamu mchango wake katika Chadema, niwaombe tuungane katika kipindi hiki tusitishe shughuli zote za kisiasa ili tuungane kwenye maombelezo ya siku tano," amesema Makonda.
Amesema kama vyama vingine vina matukio basi visitishe kwa muda ili kuungana na Watanzania katika maombelezo ya siku tano yaliyotangazwa na Rais Samia.
Mwananchi lilimtafuta Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ambaye amesema chama hicho kitakuwa bega kwa bega katika kuomboleza na kuwa karibu na familia ya Lowassa kwa muda wote wa maombolezo uliotangazwa na Serikali.
Aidha, amefafanua kuwa maombelezo ya kitaiafa yameanza jana Februari 10, 2024 hadi Februari 14 na tukio lao la maandamano linaanza Februari 15 mkoani Mwanza.