Bwawa la Nyerere litakavyozalisha MW 2,115

Muktasari:
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limefafanua hatua kwa hatua kuhusu ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) litakalogharimu Sh6.5 trilioni na hatua zilizofikiwa mpaka sasa.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande ameeleza hatua kwa hatua kuhusu ujenzi wa bwawa la Nyerere (JNHPP) na faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.
Chande ameyasema hayo leo Desemba 22, 2022 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia tukio la kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo lililopo Rufiji, mkoani Pwani.
Maharage alisema ili umeme ufuliwe ni lazima maji yazungushe vinu na kwa eneo hilo wamechukua maji kutoka katika mito mikubwa mitatu ikiwemo mto Kilombero asilimia 65, mto Luwegu asilimia 19 na mto Ruaha mkuu ambao unachangia asilimia 15.
“Ujenzi wa mchepusho wa maji umefikia asilimia 97.97 asilimia 3.2 iliyobaki kumalizika ni kazi ya leo kufunga lango kuu la njia kuu ya mchepusho wa maji tukikamilisha na kuweka zege lango hilo lisitumike tena na maji kuanza kujaa basi kazi hiyo itakua imefikia asilimia 100,” amesema.
Amesema njia hiyo ya kuchepusha maji ina urefu wa mita 703 sawa na urefu wa viwanja saba wa mpira wa miguu na upana ni kipenyo cha mita 12 zaidi ya mara mbili ya kipenyo cha njia ya mwendo kasi handaki la Kilosa kwa manaa treni mbili zinaweza kupishana.
Chande amesema baada ya ujenzi wa kuchepusha maji hatua inayofuatia ni ujenzi wa tuta kuu ambao umefikia asilimia 89.51 asilimia 10.5 ni hatua ya kumazilia mageti ili bwawa linapojaa ili lisihabirike kwa usalama lazima mageti yafunguliwe kuruhusu maji kutoka.
Amesema ujenzi huo umetumia zege mpya na kiasi cha zege kilichotumika ni mita za ujazo milioni 1.75 ambayo ni zaidi ya madaraja 20 ya Tanzanite na kwmaba ukuta wa bwawa hilo una uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 32 ambayo ni zaidi ya maji yanayopatikana katika ziwa rukwa yakishajaa.
“Urefu wa tuta hili katikati ya tuta mpaka juu ni mita 131 sawa na ghorofa 42 ambazo kama zikijengwa na umbali wa tuta mpaka mwisho wa bwawa ni kilomita 100 sawasawa na kutoka Dar es Salaam na Chalinze,” amesema Chande.
Aidha Chande amesema shirika hilo lina maeneo saba ya wanayoyafanyia kazi na eneo la kwanza lina miradi ya kimkakati na eneo hilo ni muhimu sana,
“Tuna mpango wa kuwa na umeme wa megawati 5,000 hivyo ujenzi wa bwawa hili unakwenda kuongeza megawati 2,115.”