Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi mpya Tanesco aanza na umeme Mbagala

Muktasari:

  • Tatizo la umeme kwa wakazi wa Mbagala huenda likaanza kuwa na ahueni baada ya megawati 50 kuongezwa katika mzunguko baada kukamilika kwa maboresho ya kituo cha kupoza umeme cha Mbagala.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange ametangaza awamu ya kwanza ya kituo cha kupoza umeme cha Mbagala kilichoboreshwa kimeanza rasmi kufanya kazi huku kikizalisha megawati 50 za umeme.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua kituo hicho kilichopo Mbagala, leo Jumanne, Mei 13, 2025, Twange amesema uwezo huo mpya wa kituo utasaidia kutatua changamoto za upatikanaji umeme za muda mrefu katika eneo hilo.

Mradi huu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6.4 (zaidi ya Sh16 bilioni) ikiwa ni sehemu ya kuimarisha gridi ya Taifa na upatikanaji wa umeme nchini.

“Nimetembelea maeneo mengi kutathmini hali halisi ya upatikanaji wa umeme,” amesema Twange huku akisisitiza dhamira ya Tanesco ni kuboresha uhakika wa nishati nchini kote.

Twange anatembelea mradi huu ikiwa ni mara ya kwanza kufika eneo hili tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo  Mei 6, 2025.

Twange alichukua nafasi ya kuliongoza shirika hilo linalojishughulisha na uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme akiziba pengo lililoachwa wazi na Gissima Nyamo-Hanga ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotolea wilayani Bunda, mkoani Mara.

Twange amesema awamu ya kwanza ya mradi huo imekamilika kwa asilimia 70, na wataalamu wa kiufundi tayari wamepelekwa kusimamia usambazaji wa umeme.

“Ikikamilika awamu ya pili itakuwa na  uwezo wa hadi megawati 120, na jumla ya uwezo wa MVA kufikia 170,” ameeleza.

Amesema hilo linafanyika sasa wakati mahitaji ya umeme katika eneo la Mbagala yanaendelea kuongezeka kila siku.

“Baada ya kukamilika kwa awamu zote, tunatarajia upatikanaji wa umeme wa uhakika. Kwa sasa mahitaji yamefikia megawati 50, ambazo zitasambazwa kuhudumia maeneo mbalimbali,” ameongeza Twange.

Amewahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa Tanesco ipo tayari kupokea mrejesho na kujitahidi kutatua changamoto zinazohusiana na upatikanaji wa umeme.

 “Tumeanzisha kituo cha huduma kwa wateja kwa ajili ya kushughulikia malalamiko. Ingawa baadhi ya matatizo yanatokana na shughuli za kibinadamu, yale yaliyo ndani ya uwezo wetu yanashughulikiwa kwa haraka,” amesema.

Awali, Meneja wa Mradi huo, Bernard Maiya amesema pindi ujenzi huo utakapokamilika kwa awamu zote uwezo wake utafikia MVA 170.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesifu maendeleo ya mradi huo huku akisema changamoto kubwa Mbagala imekuwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara.

“Kupitia uwekezaji huu wa Dola milioni 6.4, sasa tunashuhudia mabadiliko ya kweli. Timu ya Tanesco imefanya kazi kwa kasi zaidi ya ilivyotarajiwa, kwa kuanza kazi kabla ya awamu ya majaribio iliyopangwa kufanyika Juni,” amesema.

Diwani wa Charambe, Twahi Shabani naye alipongeza uzinduzi wa mradi huo akisema kituo hicho kitaondoa tatizo la kukatika kwa umeme.